Watu 20 wauawa baada ya boti kuteketea mtoni Kongo DR


Kwa akali watu 20 wamepoteza maisha baada ya boti waliokuwa wakisafiria kuteketea kwa moto katika bandari moja iliyoko viungani mwa mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kinshasa.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo, Didier Tenge amenukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa, ajali hiyo ilitokea jana nyakati za adhuhuri katika Bandari ya Ngafura, pembeni ya Mto Congo.

Duru za habari zinaarifu kuwa, boti hiyo ya mizigo iliyokuwa imebeba bidhaa zenye kushika moto kwa wepesi ilikuwa inaelekea katika mkoa wa Équateur ulioko kaskazini magharibi mwa nchi, wakati wa mkasa huo.

Waziri Tenge ameeleza kuwa, watu 11 wamepata majeraha ya kuungua katika ajali hiyo, na wanatibiwa katika hospitali moja iliyoko karibu na eneo la tukio.
Mikasa na ajali za boti huripotiwa mara kwa mara DRC

Amesema amesikitishwa mno na mkasa huo, na kusisitiza kuwa ni kinyume cha sheria za nchi hiyo kwa boti na meli za mizigo kubeba abiria.

Akthari ya wananchi wa DRC hutumia usafiri wa boti kutokana na mfumo mbaya wa barabara za nchi hiyo ya katikati mwa Afrika. Ajali za boti huripotiwa mara kwa mara nchini humo.

Hivi karibuni, watu wasiopungua 55 waliaga dunia baada ya boti iliyokuwa imewabeba kuzama katika Mto Congo, kaskazini mwa mkoa wa Mongala.

                                            

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments