Agenda kuu wanazozibeba mafahali wa siasa Raila, Ruto

 

Mchuano kati ya Naibu Rais wa Kenya, William Ruto na Kiongozi wa Upinzani, Raila Odinga ni mkali mno kuelekea Uchaguzi Mkuu Kenya, unaotarajiwa kufanyika Agosti 9, mwaka huu.

Raila, kwa uungwaji mkono anaoupata, ukijumlisha na umaarufu wake wa kisiasa, anaamini safari hii hakuna wa kumzuia kuingia Ikulu ya Kenya, iliyopo Nairobi.

Ni kwa kujiamini huko, Raila anatumia wimbo wa mwanamuziki maarufu wa Afrika Kusini, marehemu Lucky Dube, unaoitwa “Nobody Can Stop Reggae” – “Hakuna anayeweza kuizuia Reggae”. Kwamba kwa sasa Raila ni Reggae, kwa hiyo hazuiliki!

Ruto anamjibu: “Raila anasema hakuna anayeweza kuzuia Reggae, na anasahau kuna Mungu wa mbinguni. Pamoja na kupoteza bure miaka yetu minne kwa ajili ya BBI, tutaweza kukamilisha agenda zetu kubwa nne nikishachaguliwa kuwa Rais.”

Muda gani umepotezwa? Ni agenda gani hizo? Majibu ni kuwa Machi 2018, Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta alikutana na kufanya mazungumzo na Raila kwa lengo la kumaliza uhasama wa kisiasa uliokuwa umetawala. Mkutano huo ni maarufu Kenya kwa jina la “handshake”.

Baada ya handshake kuzaliwa, nayo ikazaa BBI (Building Bridge Initiative), yaani mpango wa kujenga daraja. Nayo BBI, ikashawishi mabadiliko ya Katiba, lakini yakakwama. Ni hapo Ruto anaposema Raila amewapotezea muda Wakenya.

Muda umepotezwa kivipi? Jibu ni hili; Ruto alijitenga na mapatano ya Uhuru na Raila, kwa kile kinachodhaniwa kwamba ni wivu kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka huu. Ruto aliona Uhuru alikuwa anamsafishia njia Raila. Akasusa kila kilichoanzishwa nao, ikiwemo BBI.

Ruto anasema kuwa Wakenya walikuwa na nafasi kubwa ya kunufaika kupitia agenda kubwa nne, lakini shabaha ya nchi ilibadilika tangu Uhuru na Raila walipokutana na kupeana mkono, kwani walijielekeza kwenye BBI na mabadiliko ya Katiba.

Ahadi ya Ruto ni kuwa akishachaguliwa kuwa Rais wa Kenya katika Uchaguzi Mkuu unaokuja, atahakikisha anatekeleza agenda nne kubwa ambazo anadai zimetelekezwa tangu Machi 2018, Raila na Uhuru walipokutana.

Agenda hizo nne anazozisema Ruto ni nguzo kuu za ilani ya uchaguzi ambayo Uhuru aliitumia kuomba kura katika Uchaguzi Mkuu Kenya 2017. Nguzo hizo ni mosi, Usalama wa chakula, pili, Nyumba za bei rahisi kwa kila raia, tatu, Huduma sawa za afya, vilevile Viwanda na ajira.

Wakati Ruto akitamba kukamilisha agenda kubwa nne, Raila yeye anazo zake 10. Kila kitu kuhusiana na agenda 10 za Raila, kipo kwenye ilani ya uchaguzi ya Azimio la Umoja, linaloungwa mkono na wanasiasa wengi wakubwa Kenya, akiwemo Rais Uhuru.

Raila anaamini kwamba kupitia agenda zake 10, endapo atachaguliwa kuwa Rais wa Kenya baada ya Uchaguzi Mkuu ujao, ataweza kuipaisha nchi kiuchumi na kuboresha ustawi wa maisha ya Wakenya.

Katika agenda hizo 10, namba moja ni Inua Jamii, Pesa Mfukoni. Huu ni mpango wa Raila wa kutoa fedha kuanzia Sh122,000 mpaka Sh20 milioni kila mwezi, kwa familia zenye uhitaji mkubwa wa msaada.

Raila anatetea mpango huo kuwa hautakuwa kwa ajili ya kutoa fedha pekee, bali utawezesha mno ukuaji wa uchumi, kwani watakaopewa pesa, watamudu kufanya manunuzi na kusababisha mzunguko mzuri wa kifedha.

Agenda ya pili ya Raila, anaiita “BabaCare”. Huu ni mpango wa Raila kutoa huduma sawa za afya kwa Wakenya. Baba ndio jina ambalo Raila huitwa Kenya, kwa hiyo ameamua kuupa mpango wa huduma ya afya jina la BabaCare.

Kazi Kwa Wote ni agenda ya tatu ya Raila. Lengo lake ni kuhakikisha Wakenya wanakuwa na ustawi mzuri wa kijamii, hususan katika kipato. Kupitia agenda hii, shabaha yake ni kila Mkenya awe na fursa ya kufanya kazi na kutengeneza kipato.

Agenda ya Uchumi Kwa Akina Mama ni agenda ya nne. Nayo ni mahsusi kwa ajili ya kuwajengea wanawake uwezo mkubwa wa kiuchumi. Halafu kuna agenda ya vijana, inayoitwa Hashtag Inawezekana. Hii ni ya tano.

Katika agenda ya Hashtag Inawezekana, Raila anaweka mkakati wa kuhakikisha vijana wanakuwa jirani na siasa kwa sababu wao ndio wapo karibu na kesho. Anasema akichaguliwa kuwa Rais wa Tano wa Kenya, atawekeza zaidi kwa vijana ili wajiandae kuongoza taifa lao.

Namba sita ni “Waste not a Single Child”. Agenda hii ni mpango wa Raila kuhakikisha hakuna mtoto atakayesahaulika katika kupata elimu bora. Saba ni Fukuza Njaa. Hii inahusu mpango wa kilimo bora kitakachozalisha chakula cha kutosha kwa Wakenya.

Agenda ya nane ni Maji Kwa Kila Boma, kwamba kila nyumba itapata maji safi na salama. Tisa ni “One County, One Product”, ni kuhusu kila kaunti Kenya iwe inazalisha kitu kimoja ambacho kitajenga uchumi.

10 ni “The Principle of Administrative Continuity”, ambayo maana yake ni kujenga mfumo endelevu wa kiuongozi. Hapa Raila anafafanua kuwa Afrika kumekuwa na tatizo la masuala muhimu kuachwa kila utawala unapobadilika. Raila nasema ataweka mpango kwamba utabadilika utawala lakini mipango na miradi vitaendelea.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments