Aweso awataka watumishi sekta ya maji kuacha ubabe

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amewataka watumishi wa sekta ya maji kuacha ubabe na badala yake kuheshimiana kwasababu wao na wadau wengine wa sekta hiyo wanategemeana kufanikisha malengo ya Serikali.

 Aweso ameyasema hayo leo Alhamis Machi 10, 2022 katika mkutano wa wadau wa sekta ya maji nchini wakiwemo wasambazaji wa vifaa na makandarasi wa miradi ya maji.

“Ubabe tuachane nao tuheshimiane kwasababu wote tunategemeana, hatutegemei hilo kufanywa katika sekta ya maji,”amesema Aweso.

Ameagiza makandarasi wanaokamilisha kazi zao wapewe fedha zao kwa wakati badala ya kuchukua muda mrefu kuzifuatilia.

Hata hivyo, Aweso amesema suala la uaminifu linaumuhimu mkubwa na kutoa mfano wa mmoja wa makandarasi Wilaya ya Handeni ambaye alilipwa Sh600 milioni lakini hakufanya kazi.

Amesema alipoulizwa kwanini hafanyi kazi, mkandarasi huyo alisema kuwa ni kwasababu kuna wachawi.

“Kuna watu wanauwezo wa kufanya kazi lakini wamekuta hawapewi kazi. Haipendezwi kupandishana katika makarandika (ya polisi),”amesema

Amesema changamoto kubwa ya baadhi ya makandarasi ni uongo ambapo wanapoulizwa kwanini wamechelewesha kazi hutoa visingizio vya uongo.

Aidha, Aweso amesema Rais Samia Suluhu Hassan atakutana na wadau wote wa sekta ya maji ambao mkutano huo utamuhusisha pia Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba.

Amesema mkutano huo utafanyika jijini Dar es Salaam Machi 22, mwaka huu.

Pia amesema Serikali imetoa Sh41 bilioni kwa ajili ya kulipa makandarasi na kuwataka watendaji wa sekta hiyo kulipa madeni yote wanayodaiwa.

Meneja wa Wakala wa Maji Vijijini (Ruwasa), John Msengi amesema makandarasi wazawa wengi hawana mitaji na ndio maana wengi wao hata wakipewa malipo ya awali yanaisha kabla ya kumaliza shughuli iliyokusudiwa.

Mkurugenzi Mkuu wa Ruwasa, Clement Kivegalo amesema wako mbioni kutengeneza mfumo wa Tehama ambao utawezesha wakandarasi kujaza vyeti vya malipo (certificate) kwa kutimia mtandao na hivyo kurahisisha utendaji.

Naye Mwakilishi wa makandarasi, Jumanne Werema amesema miongoni mwa changamoto zinazowakabili makandarasi nchini ni ucheleweshaji wa malipo, ucheleweshaji wa misamaha ya kodi la Ongezeko la Thamani (VAT) na mikataba kutokuwa wazi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Anthony Sanga amesema wamechukua maoni na ushauri wao na kwamba watafanyia kazi na kuwajibu kwa maandishi.

 

Post a Comment

0 Comments