Recent-Post

Bagonza: Siku ya wanawake ni kupambana na ukandamizaji

 Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza amesema Siku ya Wanawake Duniani ni tunda la harakati dhidi ya mifumo iliyokuwa ikiwakandamiza.

Amesema hayo leo, Machi 08, 2022 kwenye kongamano la Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) linaloendelea mkoani Iringa alikoalikwa kama mgeni rasmi.

Katika maelezo yake Askofu Bagonza amefafanua kwamba ukandamizaji huo haukubagua rangi, uchumi, elimu, dini wala itikadi na mifumo yote ya ukandamizaji duniani, inapoanza kufanya kazi huwa haibagui.

“Kwa hiyo ni wito wangu kwenu kwamba tunapozungumzia haki za kina mama tunahitaji kuungana bila kutazama tofauti zetu kwa sababu walioanzisha siku hii hicho ndicho kilichowaunganisha, kutokomeza ubaguzi na ukandamizaji,” amesema.

Hata hivyo ametaja sababu mbili kubwa za kuhudhuria kongamano hilo na kukubali kuwa mgeni rasmi zikiwamo tofauti za kiitikadi zilizoanza kujitokeza siku za hivi karibuni hivyo kuhitaji juhudi kubwa kuanza kujenga na kuliunganisha upya Taifa.

“Sababu ya pili ni tukio la kihistoria kwa Taifa kumpata Rais wa kike kwa mara ya kwanza anayeadhimisha mwaka mmoja tangu alipoingia madarakani mwezi huu. Nimeona nishiriki na nyinyi kumshukuru Mungu kwa kutupatia funzo kwa njia ya ajabu kwani aliyewekwa kama mgombea mwenza sasa ni Rais wetu. Tunamshukuru Mungu mama yuko ofisini si kwa mapenzi yetu bali mapenzi ya Mungu,” ameeleza Askofu Bagonza.

Post a Comment

0 Comments