Dar wapewa sifa kugombea uongozi CCM

Wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam wametakiwa kujisajili kwenye mfumo wa kadi za kielektroniki kwani asiyefanya hivyo hataruhusiwa kugombea nafasi yeyote ya uongozi ndani ya chama hicho.

Hayo yamebainishwa na Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Adam Ngalawa wakati wa mkutano mkuu maalumu wa chama hicho ambapo Mbunge wa Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM katika jimbo hilo.

Ngalawa amesema ni muhimu kila mwanachama kuhakikisha anajisajili katika mfumo wa kadi za kielektroniki kwani hawataruhusiwa kugombea bila kuingia katika mfumo huo.

"Kabla ya uchaguzi tunaomba wanaCCM wote mjisajili kadi katika mfumo wa kielektroniki, kwasababu ambao hamtajisajili na mfumo huu hamtaweza kuingia kwenye uchaguzi," amesisitiza.

Amesema wakati chama kikijiandaa kuanza kufanya uchaguzi wa viongozi wake kuanzia ngazi ya mashina hadi taifa, wanachama wanapaswa kujiandaa kisaikolojia.

"Kila mtu ana haki ya kuchukua fomu na kugombea nafasi yeyote anayoona inafaa, lakini ni muhimu kujiandaa kisaikolojia kwa sababu wajumbe ndio wanachagua.

"Ukikosa ukapata 0 au 1 usilalamike, shukuru Mungu kwa kila jambo kwasababu uchaguzi ni mpango wa Mungu, na hua tayari ameshamchagua anayetaka aongoze. Hivyo ukikosa jipange upya kwaajili ya uchaguzi mwingine," amesema Ngalawa.

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kheri James amesema zipo kazi kubwa zimefanyika katika Jimbo hilo katika maeneo ya miundombinu, afya na ustawi wa jamii na kubainisha kuwa wanaendelea kupokea fedha kutoka serikalini kwaajiliya kuendeleza miradi ya maendeleoa Ubungo.

"Hali ya ulinzi na usalama Ubungo ni shwari kabisa na miradi inaendelea vizuri. Tunaridhishwa na utendaji wa Kitila, anafahamu wajibu wake kwa kusikiliza kero za wananchi na kuzisemea," amesema James.

Kwa upande wake mbunge wa Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo amesema katika moja ya tafiti waliyoifanya imebaini kuwa asilimia 43 ya wananchi wa jimbo hilo wametaka changamoto ya ubovu wa miundombinu ya barabara kutatuliwa.

Amesema kutokana na maoni hayo waliyafanyia kazi na wamefanikiwa kuboresha barabara za mitaa na malengo yao hadi kufikia mwaka 2025 asilimia 50 za barabara ziwe za lami.

"Wakati naingia nilikuta barabara za lami 20, changarawe 48 na za udongo 32, lakini lengo sisi hadi kufikia 2025 tuwe na asilimia 50 ya barabara za lami na mpaka sasa barabara zenye hali nzuri  zimefikia asilimia 23, " amesema

Kwa upande wa elimu, Profesa Mkumbo amesema moja ya changamoto waliyonayo ni ukarabati wa madarasa yaliyochakaa huku akibainisha katika bajeti ya mwaka 2022/23 wameelekeza nguvu katika ujenzi wa vyoo.

 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments