Dk Mwigulu aelezea ugumu ziara za Rais Samia Ulaya

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba ameelezea ugumu wa ratiba ya ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoifanya katika nchi za Ufaransa, Ubelgiji na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) akisema hakukuwa na ratiba ya chakula cha mchana ‘lunch’.

Dk Mwigulu ametoa kauli hiyo leo Jumatano Machi 2, 2022 wakati akizungumzia mafanikio ya ziara ya Rais Samia aliyoifanya katika nchi hizo siku chache zilizopita.

“Mimi nilivyoambatana na Rais nimeona kwamba anavyokuwa kwenye ziara hizo anakuwa na ratiba ngumu na anazitekeleza kwa ajili ya manufaa ya Watanzania,

“Ni ziara ngumu, nimeambatana naye hizi siku zote, sikumbuki siku hata moja ambayo tulikuwa hata na ratiba ya lunch (chakula cha mchana) kwa hiyo ni kazi mfululizo, kuamka mapema kulala kwa kuchelewa na mikesha inayoambatana na ukamilishwaji wa masuala yanayohusu masilahi mapana ya nchi” amesema

Waziri Mwigulu, Waziri wa Nishati, January Makamba na Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Bishara, Dk Ashatu Kijaji leo walikuwa wanazungumzia mafanikio ya ziara ya Rais Samia aliyoifanya katika nchi za Ufaransa, Ubelgiji na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Awali Dk Mwigulu amebainisha baadhi ya mambo yaliyofanyika kwenye ziara hiyo ya Rais Samia kwenye nchi tatu hasa katika sekta ya Uwekezaji, Fedha na Nishati.

Amesema kuwa ziara hiyo imesaidia kusainiwa mikataba mbalimbali na kuwavutia wawekezaji kuja nchini kuangalia fursa zilizopo.

Dk Mwigulu ambaye aliambatana na Rais Samia kwenye ziara hiyo, amesema kuwa katika ziara hiyo, mikataba sita ya miradi ya mikopo nafuu na misaada ilisainiwa.

Kuhusu wawekezaji, Dk Mwigulu amesema kuwa Baraza la Mawaziri linatarajia kukutana Machi 4 kwa ajili ya kuratibu namna ya kuwapokea wawekezaji ambao wanatarajiwa kuingia nchini ndani ya wiki mbili kuangalia fursa zilizopo.

 Kutangaza fursa za uwekezaji, vivutio

Akizungumzia namna ambavyo ziara hiyo ilivyosaidia kutangaza fursa za uwekezaji na vivutio vilivyopo nchini, Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji amesema Tanzania imepata nafasi ya kutangaza fursa zinazopatikana nchini katika jengo refu kuliko yote duniani la Burj Khalifa lililopo katika Jiji la Dubai.

Dk Kijaji amesema bendera ya Tanzania na picha ya Rais Samia kupandishwa kwenye jengo hilo refu zaidi duniani ni moja ya mafanikio ya kuitangaza Tanzania huku akibainisha kuwa fursa na vivutio mbalimbali vitaendelea kupandishwa kwenye jingo hilo.

“Wote tumeona kilichotokea kule Jiji la Dubai, kuonyesha umuhimu wa ziara ya Rais aliyoifanya, ndani ya Jiji la Dubai walionyesha bendera ya Tanzania kwenye jengo refu zaidi duniani kama zawadi kwa Rais na Taifa letu’ amesema Dk Kijaji na kuongeza

“Jana tena usiku wakarusha bendera ya Taifa letu ikiwa na picha ya Rais wetu. Katika kuendelea kuitangaza na kuuza fursa tulizonazo, Watanzania watarajie siku ya leo wataona pia bendera yetu ikiendelea kupandishwa kwenye jengo lilelile na leo hii tutakuwa na picha ya Mlima Kilimanjaro” amesema

Sababu picha ya Rais, bendera kupandishwa Dubai hii hapa

Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji amesema kuwa bendera ya Tanzania kupandishwa kwenye jengo refu zaidi duniani la Burj Khalifa jijini Dubai ni zawadi kwa Rais Samia Suluhu Hassan na Taifa.

 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments