Farid: Moto? Mbona bado kabisa!

Wakati mashabiki wa soka nchini wakiendelea kumjadili kwa namna alivyobadilika ndani ya muda mfupi, winga nyota wa Yanga anayetumika pia kama beki wa kushoto, Farid Mussa amesema gari limewaka, ila moto bado kabisa haujakolea.

Farid alisema anatambua ana kazi kubwa ya kuonyesha uwezo mkubwa alionao kisoka, hivyo sifa anazopewa kwa sasa hazimtoi kwenye reli kwa vile anaamini bado hajafikia uwezo na kipaji alichonacho.

Nyota huyo aliyetoa asisti kwenye mchezo uliopita wa kirafiki kwa Taifa Stars iliyoifumua Afrika ya Kati kwa mabao 3-1, alisema amekuwa akisikia sifa dhidi yake, lakini imezidi kumchochea kufanya zaidi huku akijifunza mambo mapya kila uchao.

“Nimekuwa nikipenda kuwa bora, hakuna namna nyingine zaidi ya kuumia kwa kujifunza na kufanya mazoezi kwa juhudi, huwezi kufanya jasho bure, naamini kuwa bado nina safari ndefu na shauku yangu kucheza katika kiwango cha juu zaidi,” alisema.

Nyota huyo wa zamani wa Azam, aliyewahi kucheza soka la kulipwa klabu ya CD Tenerife inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Hispania ‘LaLiga 2’, amekuwa kwenye kiwango bora kwa sasa tangu alipoanza kutumika kama beki wa kushoto kutokana na uwezo wake wa kushambulia na kuifanya Yanga iwe na nguvu kubwa kushoto.

Kwa mujibu wa kocha msaidizi wa Yanga, Cedrick Kaze ambaye alitambua kipaji cha Farid tangu akihudumu kwa Wananchi awamu yake ya kwanza, alisema nyota huyo ni kati ya wachezaji wenye uwezo wa kusikiliza maelekezo na kuyafanyia kazi kwa haraka na anaweza kufika mbali.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments