Hatihati timu za England, Hispania kukutana nusu au fainali Ulaya

Baada ya klabu za nchi moja kukwepa kukutana katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya-- England na Hispania-- ratiba iliyopangwa leo (Ijumaa) itazikutanisha timu nne kutoka nchi hizo mbili.

Kulikuwa na hatari kwa timu mbili za England-- kati ya Chelsea, Manchester City na Liverpool-- kukutana robo fainali, hali ambayo pia ingeweza kujitokeza kwa klabu tatu za Hispania-- Real Madrid, Villareal na Atletico Madrid.

Lakini ratiba iliyopangwa leo sasa itazikutanisha klabu nne za Hispania na England katika mechi za kuwania tiketi ya kucheza nusu fainali baada ya mabingwa watetezi wa soka Ulaya, Chelsea kupangwa na Real Madrid wanaoshikilia rekodi ya kutwaa kombe hilo mara 13, huku Manchester City ikipangwa na wazoefu wa michuano hiyo, Atletico Madrid.

Villareal ikiwa imepangwa kukutana na Bayern Munich na Liverpool dhidi ya Benfica, kuna uwezekano kwa timu tatu kati ya nchi hizo mbili kufika nusu fainali na ikiwezekana fainali kukutanisha klabu za nchi moja kama ilivyokuwa msimu uliopita.

Nusu fainali ya kwanza itazikutanisha Man City ama Atletico dhidi ya Chelsea ama Real Madrid na nyingine itazikutanisha Benfica ama Liverpool dhidi ya Villarreal ama Bayern Munich kuwania tiketi ya kwenda jijini Paris ambako fainali za mwaka huu imehamishiwa baada ya Russia kuivamia Ukraine.

Na ili hilo iwezekane, vigogo hao wa England na Hispania watalazimika kuiondoa Bayern Munich, ambayo imeshatwaa ubingwa huo mara tano, na Benfica ya Ureno iliyotwaa mara mbili.

Safari hii, Chelsea, iliyoishinda Manchester City katika fainali ya mwaka jana, itakuwa ikitetea kombe hilo katika mazingira tofauti na magumu baada ya mmiliki wake, Ramon Abramovich kuwekewa vikwazo na kulazimika kuiuza klabu hiyo. Itakutana na Real inayosaka taji hilo kwa mara ya 14 baada ya kuwa klabu ya kwanza kutwaa ubingwa huo mara tatu mfululizo chini ya Zinedine Zidane.

Abramovich, ambaye aliinunua Chelsea mwaka 2003 na kuiwezesha kutwaa ubingwa wa England na baadaye taji la Ulaya mara mbili, amewekwa vikwazo kutokana na kuwa mshirika mkubwa wa Rais Vladimir Putin wa Russia ambayo imeivamia Ukraine.

Pamoja na serikali ya Uingereza kutoa leseni maalum ya kumalizia mechi zake za msimu huu, Chelsea hairuhusiwi kuuza wala kusajili wachezaji wapya, kuongeza mikataba ya wafanyakazi wake,kuuza tiketi za mechi zake na hivyo mechi zake za Ligi Kuu na ile ya Ulaya hazitakuwa na mashabiki isipokuwa wenye tiketi za msimu, na hiruhusiwi kuuza bidhaa za chapa yake.

Hata hivyo, vigogo hao wa London wameshinda mechi mbili za England na moja ya Ulaya licha ya vikwazo kuanza kufanya kazi.

Inatarajiwa kuwa na mtihani mgumu mbele ya Real Madrid, ambayo haikutarajiwa kufika hatua hiyo baada ya kupangiwa Paris Saint Germain katika 16 bora.

Baada ya PSG kushinda kwa bao 1-0 jijini Paris, Real, inayofundishwa na Carlo Anceloti, iligeuza kibao nyumbani na kuwasambaratisha vigogo hao wa Ufaransa kwa mabao 3-1 na kufika robo fainali.

Vijana wa Thomas Tuchel wataanzia nyumbani London kati ya Aprili 5 na 6 na wiki moja baadaye kwenda Santiago Bernabeu jijini Madrid kumalizia kazi ya kutoka mashindanoni au kusonga mbele.

Timu nyingine yenye mtihani mgumu ni Man City ambayo itakutana na vijana wa Diego Simeone wanaopigana hadi mwisho baada ya Atletico Madrid kuiondoa Manchester United katika 16 bora.

Kocha Pep Guardiola ameshatwaa kila kitu England akiwa na City, lakini amekuwa hana mwisho mzuri katika michuano ya Ulaya. Mwaka jana City ilifungwa na Chelsea katika fainali, ikiwa ni baada ya kutolewa hatua ya robo fainali kwa misimu mitatu mfululizo kuanzia wa mwaka 2017-18 ilipokutana na Liverpool, Tottenham Hotspur na Olympique Lyon.

Liverpool ndiyo inaonekana ina mtihani mwepesi baada ya kupangwa na Benfica, ambayo haipewi nafasi kubwa ya kufanya maajabu licha ya kuiondoa timu ngumu ya Ajax Amsterdam katika hatua ya 16 bora baada ya kuvuka kundi lililokuwa na timu kama Barcelona.

Liverpool, mabingwa wa Ulaya wa mwaka 2019 na ambao wamerudi kwa kishindo kupigania ubingwa wa England wakizidiwa kwa pointi moja na Man City, wataanzia ugenini jijini Lisbon kuivaa Benfica.

Wanaivaa timu ambayo imepoteza matumaini ya kutwaa ubingwa wa Ureno ikishika nafasi ya tatu kwa kuwa na pointi 58 huku vinara Porto wakiwa na pointi 70.

Pamoja na kwamba Bayern Munich wamepangwa na Villareal, ambayo haina mafanikio makubwa katika michuano hiyo mikubwa ya klabu barani Ulaya, inaweza kuambulia kile kilichowakuta Juventus katika hatua ya 16 bora kama haitakuwa makini. Villareal ililazimishwa bao 1-1 jijini Lisbon na vigogo hao wa Italia, lakini ikashinda kwa mabao 3-0 jijini Turin na kufika hatua hiyo.

Awali mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa ilipangwa kufanyika Mei 28 jijini St Petersburg, Moscow lakini baada ya Russia kuivamia Ukraine ilihamishiwa Paris.

Hii ni mara ya tatu mfululizo kw afainali kuhamishwa baada ya mechi ya mwaka 2020 kukuhamishwa kutoka Instanbul na kupelekwa Lisbon na baadaye kuiondoa katika jiji hilo la Uturuki kwenda Porto mwaka jana.

Uwanja wa Stade de France, ambako fainali itachezwa, una uwezo wa kuchukua watu 80,000. Umeshatumiwa kwa fainali ya ligi hiyo mara mbili; mwaka 2000 wakati Real Madrid ilipoishinda Valencia, na mwaka 2006 wakati Barcelona ilipoilaza Arsenal.

 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments