Jafo aunda timu kuchunguza madai ya sumu Mto Mara

Serikali imetangaza kuunda timu maalumu itakayochunguza sababu ya maji katika Mto Mara kuwa meusi na kuua viumbe hai, wakiwemo samaki.

Akizungumza jana baada ya kufika katika mto huo kuona hali hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Suleiman Jaffo alisema timu hiyo ya kitaifa ataiunda leo ili ianze kufanya kazi mara moja.

“Nimejionea mwenyewe hali si shwari hapa kwa sababu harufu iliyopo hapa si ile ninayoikuta kila nikija Mara, kwa hiyo lazima Serikali ifanye jambo, tena kwa haraka, ili tupate majawabu nini chanzo na kipi kifanyike kabla watu hawajaathirika,” alisema Jafo.

Alisema timu hiyo anayoiunda itajumuisha wataalamu mbalimbali, wakiwepo wa miamba na kemikali, ambao watatakiwa kujua kama mabadiliko hayo yamesababishwa na kemikali au miamba.

Awali, Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria wa Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC), Redempta Samuel alisema timu ya wataalamu ilifika katika eneo la mto huo tangu Machi 10, 2022 kwa ajili ya kufanya uchunguzi.

Alisema hadi sasa wamekwishachukua sampuli 32 kutoka katika maeneo mbalimbali ya mto huo na katika Ziwa Victoria na uchunguzi unaendelea kujua tatizo ni nini.

Waziri Jaffo alishindwa kuingia ndani ya mto huo kama ilivyokuwa imepangwa kutokana na upande wa pili wa daraja la Kirumi kuzingirwa na magugu maji.

Wakati hali ikiwa hivyo, Mgodi wa Dhahabu wa North Mara umekanusha taarifa zinazouhusisha na uchafuzi wa mto huo.

Kwa takriban siku tano Mto Mara umekumbwa na mabadiliko yaliyosababisha idadi kubwa ya samaki kufa, huku maji yakibadilika rangi na kuwa meusi.


North Mara yakanusha

Kutokana na taarifa za uchafuzi wa mto huo, Mgodi wa North Mara umekanusha taarifa zinazouhusisha na uchafuzi huo.

Taarifa iliyotolewa na Meneja wa Barrick nchini, Georgia Mutagahywa kwa vyombo vya habari jana, imesema mbali na eneo husika kuwa umbali wa kilomita 80-85 chini ya mgodi, zebaki si sehemu ya orodha ya vitendanishi vya mgodi huo.

“Wala haitokei kiasili katika eneo hilo na hivyo basi, kama kuna zebaki yoyote iliyopatikana katika mto, haiwezi kuhusishwa na mgodi,” alisema.

Kwa mujibu wa Georgia, Mamlaka ya Bonde la Maji ya Ziwa Victoria mara kwa mara imekuwa ikichukua sampuli za maji katika maeneo yaliyo jirani na migodi na mgodi wenyewe una mpango madhubuti wa ufuatiliaji wa maji ya ardhini na hakuna ushahidi wa kuwepo zebaki au uchafu mwingine wowote kwenye maji ndani au karibu na maeneo ya uzalishaji.

“Serikali ya Tanzania iliunda timu ya wataalamu inayoongozwa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ambayo imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara ili kuhakikisha hakuna uchafuzi wa mazingira au maji, unaotokea katika mgodi huo na katika maeneo yanayouzunguka,” alisema.

Alifafanua kuwa mgodi huo pia umefikia lengo muhimu la uhifadhi wa taka zitokanazo na mchakato wa uchenjuaji wa madini.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments