Jeshi la Uganda limekanusha kuwa mtoto wa Museveni amejiuzulu

Muhoozi Kainerugaba

Jeshi la Uganda limesema leo Jumatatu kwamba mtoto wa kiume wa Rais Yoweri Museveni, Luteni Jenerali Muhoozi Kainerugaba ambaye anatajwa kuwa ndiye atakayerithi miikoba ya baba yake kama rais ajaye wa Uganda, hajajiuzulu.

Muhoozi Kainerugaba alitangaza kwenye mtandao wa Twitter mnamo Machi 8 kwamba amestaafu kutoka kwenye jeshi baada ya utumishi wa zaidi ya miaka 20.

Hatua hiyo ilitafsiriwa na wengi kuwa ni ishara kwamba Kainerugaba, ambaye ni kamanda wa vikosi vya nchi kavu vya jeshi la Uganda, anajiandaa kuingia katika siasa katika njia ya kuelekea kuwania urais kwenye uchaguzi ujao wa 2026.

Msemaji wa Jeshi la Nchi Kavu la Uganda, Chris Magezi amesema: Jenerali hajajiuzulu kutoka jeshini. 

Chris Magezi amesema: "Tume ya Jeshi ambayo ni chombo kilichopewa mamlaka ya kushughulikia maombi ya kustaafu haijapokea maombi yake."

Sheria za Uganda zinawazuia wanajeshi wanaohudumu kushiriki katika siasa. Luteni Jenerali Muhoozi Kainerugaba, 47, mwenyewe hajasema kama anataka kuwania urais lakini wafuasi wake wamekuwa wakifanya kampeni za mitandaoni na mitaani za kupigia debe kugombea kwake.

Museveni, 77, rais wa nne barani Afrika aliyeongoza kwa muda mrefu zaidi, amekuwa akishutumiwa na upinzani na makundi ya kutetea haki za binadamu kuwa anatumia jeshi kuwadhoofisha wapinzani wake kwa kutoa vitisho, vipigo au kuwasweka jela.

Yoweri Kaguta Museveni
Katika ishara ya kile ambacho wakosoaji wanakitaja kuwa ni kuongezeka kwa ukandamizaji unaofanywa na serikali ya Museveni, mwandishi mashuhuri wa Uganda, Kakwenza Rukirabashaija aliwekwa kizuizini mwezi Disemba mwaka jana na baadaye kushtakiwa kwa makosa ya mawasiliano ya Twitter zake ambazo zilimkosoa Kainerugaba na baba yake, Rais Yoweri Museveni.


Kwa sasa Rukirabashaija, amekimbilia uhamishoni nchini Ujerumani.


 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments