JWTZ yasamehe vijana 853 wa JKT waliofukuzwa


 Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jenerali Venance Mabeyo amewasamehe vijana 853 wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) waliokiuka taratibu kwa kuanzisha mgomo na kuandamana kwenda Ikulu wakishinikiza kuajiriwa jeshini.

Aprili 8, 2021 vijana 854 ambao mmoja wao amefariki, walianzisha mgomo na kufanya maandamano kwenda Ikulu ya Chamwino Dodoma, kwa madai ya kutaka kumuona rais ili wadai kuandikishwa jeshini kama walivyoahidiwa na aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli.

Kutokana na hatua hiyo, Aprili 17, 2021 Jenerali Mabeyo akiwa katika hafla ya kuwatunuku kamisheni maofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) mjini Dodoma, alitangaza kuwafukuza vijana hao kwa kukiuka taratibu za jeshi kwa kuanzisha mgomo na kufanya maandamano.

Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 5, 2022 msemaji Mkuu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Luteni Kanali Gaudentius Ilonda amesema Jenerali Mabeyo ametoa msamaha kwa vijana hao na kuwataka kurejea kwenye makambi kwaajili ya kuendelea na mafunzo mara moja.

"Aprili 12, 2021 vijana wa kitanzania walikuwa wanaendelea na mafunzo ya JKT kwa kujitolea ambapo walikuwa 854, lakini walifukuzwa na kuondolewa kwa sababu ya makosa ya kinidhamu.

"Jeshi limepokea taarifa ya kijana mmoja kuwa ameshafariki hivyo kubaki vijana 853, hivyo Mkuu wa Jeshi ametoa msamaha kwa vijana wote na kutoa maelekezo ya kurejea kwenye makambi kwaajili ya kuendelea na mafunzo," amesema.

Amesema kabla ya msamaha huo, JWTZ lilifanya uchunguzi na utafiti wa kina na kujiridhisha kuwa vijana hao walishawishiwa kwa mambo mbalimbali.

"Vijana hawa walishawishiwa kutokana na utoto na kutokujitambua na baadhi kurubuniwa na kufuata mkumbo, JWTZ lilifanya utafiti mkoa kwa mkoa, wilaya kwa wilaya, kata kwa kata na kijiji kwa kijiji.

"Pia tulifanya utafiti ngazi ya kitongoji na familia kwa usiri mkubwa bila wao kufahamu, kwa taarifa hii vijana wote 253 wanatakiwa kupokelewa ifikapo Machi 12,mwaka huu katika kambi 841 JKT iliyopo Mafinga mkoa wa Iringa," amesema.

Aidha jeshi hilo limeeleza kuwa taratibu nyingine zitaelezwa baadae, hivyo wale wenye mpango wa kufanya udanganyifu wajihadahari kwani kwenye msafara wa mamba hata kenge wapo.

"Wapo watu watakaofika kufanya udanganyifu, wafahamu tuna majina yote picha zao pammoja na makundi ya damu, kama kuna waliopanga kufanya hivyo waache mara moja," amesema.

Ameongeza kuwa kwa wale wenye vitendo vya kuwarubuni vijana walioko kwenye kambi zao, kuacha mara moja kwani Jeshi liko imara katika kulinda mipaka ya nchi, Katiba pamoja na kumtii Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Vijana 854 wa JKT walioandamana kwenda Ikulu watimuliwa

Mkuu wa majeshi nchini Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo amesema vijana 854 wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) waliokiuka taratibu kwa kuanzisha mgomo na kuandamana kwenda Ikulu wakishinikiza kuajiriwa jeshini  wamesitishiwa mikataba yao na kurudishwa majumbani.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments