Kikosi kazi chapendekeza mchakato Katiba mpya kuanzia 2025, Rais Samia ajibu

Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na wajumbe wa Kikosi Kazi cha kuratibu Maoni ya Wadau wa Demokrasia ya Vyama vingi vya Siasa mara baada ya kupokea Taarifa yao Ikulu Jijini Dar es Salaam leo Jumatatu Machi 21, 2022. Picha na Ikulu

Kikosi kazi cha kilichoteuliwa na msajili wa vyama vya siasa nchini, Jaji Francis Mutungi kimependekeza mchakato wa kupata Katiba Mpya uanze baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku Rais Samia Suluhu Hassan akikiagiza kulifanyia kazi na kupeleka mapendekezo.

Mwenyekiti wa kikosi kazi hicho, kinachojumuisha wajumbe 25 kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo wanasiasa, asasi za kiraia, wanazuoni na wadau wa kamati za ulinzi na usalama Profesa Rwekaza Mukandara ameeleza hayo leo Jumatatu Machi 21,22 Ikulu Dar es Salaam.

Profesa Mukandara ametoa mapendekezo wakati akiwasilisha taarifa ya awali ya utendaji kazi wa kikosi hicho, kwa Rais Samia.

Kazi kubwa ya kikosi kazi hicho ni jukumu la kuangalia na kuchambua mwenendo wa hali ya demokrasia na namna ya kutatua changamoto zinazoikumba baadhi ya vyama vya siasa, ikiwemo mikutano ya hadhara.

Katika maelezo yake, Profesa Mukandara amesema sababu za kutoa pendekezo hilo ni pamoja na kutoa fursa ya kuanisha dira mpya ya maendeleo ya miaka ijayo, itakayotoa mwelekeo wa Katiba mpya.

Pia kuna suala la kukosekana kwa muda wa kutosha kuanza kutumia Katiba mpya ndani ya kalenda ya uchaguzi 2025. Kuna haja ya kutoa fursa ya kufanya marekebisho ya sheria ya uchaguzi na kanuni zake.

Jambo jingine ni kuna haja ya kutoa fursa ya kutosha ya kufanyia kazi masuala ya muda wa kati ikiwa ni pamoja na kuanisha masuala ya dira ya maendeleo, amesema Profesa Mukandara.

Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo, Rais Samia amesema “Hili la Katiba mpya mtakwenda kulifanyia kazi na mtaleta mapendekezo yatakayotangazwa Watanzania wote wayaelewe, Mimi nakubaliana kuwa ni jambo la muda mrefu lakini Watanzania wote waelewe, amesema Rais Samia na kuongeza:

Lakini kwanza tukayafanyie kazi haya marekebisho tuliyoyasema haya kipindi hichi cha muda wa kati halafu huko mbele tuone je tuna haja ya kurekebisha katiba yetu pengine kutakuwa na haja sio ya kuandika mpya, kurekebisha baadhi ya maeneo na hata kama tunaandika mpya lakini kazi kubwa inakuwa imefanyika kwenye marekebisho ambayo tunakuwa tumeyafanya kule ni kwenda kuingiza tuu kwenye hiyo katiba.

 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments