Recent-Post

Majaliwa aanza kutafuna mfupa

             

Kaya 86 zilizo na jumla ya watu 453 zimekubali kuondoka hifadhi ya Ngorongoro kwa hiari yao, huku wengine wakiendelea kujiandikisha.

Majina hayo yalikabidhiwa jana kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ikiwa ni utekelezaji wa mazungumzo ambayo aliyafanya na wadau wa uhifadhi kwenye vikao vilivyofanyika Februari 14 na 17, mwaka huu katika tarafa za Loliondo na Ngorongoro, wilayani Ngorongoro, Mkoa wa Arusha.

Katika mazungumzo yake na viongozi wa kimila wa kabila la Wamasai wilayani humo, Waziri Mkuu alisema Serikali imechukua hatua kadhaa dhidi ya wananchi walioamua kuhama kwa hiari.

Aliwaeleza viongozi hao kwamba Serikali imetenga eneo la kilomita za mraba 400,000 wilayani Handeni (Tanga) ambalo kati ya hizo, kilomita za mraba 220,000 zitatumika kwa kujenga nyumba, kupima viwanja na kutenga maeneo ya malisho.

“Tumepima viwanja 2,406 ambapo kati ya hivyo, viwanja 2,070 tumeandaa kwa ajili ya makazi na kila kimoja kina ukubwa wa ekari tatu. Tumeanza na nyumba za kuanzia 101 za vyumba vitatu vya kulala kwa wale wanaotaka. Tuna viwanja 336 kwa ajili ya huduma kama shule za msingi na sekondari, zahanati na vituo vya afya. Ujenzi wa mifumo ya maji kazi inaendelea.

“Umeme wa REA pia utakuwepo. Huku mlipo hakuna umeme. Haya tutayafanya na Mheshimiwa Rais Samia amesisitiza tuyafanye ili wananchi msipate bughudha,” alisema.

Aliwaeleza viongozi hao wa kimila kwamba Rais ameridhia eneo lao la kufanyia ibada za kimila, liendelee kutumika kwa sababu ni jambo jema.

“Maeneo yote ya kimila, wananchi waruhusiwe kuendesha mila zao. Mkuu wa Mkoa simamia hili, alimradi mkuu wa chuo apewe taarifa mapema kwamba mnakuja lini kufanya shughuli yenu,” alisema.

Waziri Mkuu alisema Rais alipofanya ziara mkoani humo aliliambia Taifa kuwa kuna hatari ya kutoweka kwa hifadhi ya Ngorongoro ndani ya muda mfupi, hivyo akatoa maagizo viongozi waende kuwasikiliza wananchi juu ya hatua za kuchukua ili tunu hiyo isipotee.

Hifadhi kulindwa

Awali kabla ya kueleza msimamo wa Serikali kuhusu ongezeko la watu katika hifadhi ya Ngorongoro, Majaliwa alisema Watanzania wanasubiri kusikia kutoka kwa watu wa jamii ya Kimasai kama uhifadhi wa Ngorongoro utaendelea kulindwa kama unavyolindwa wa Mikumi, Ruaha, Serengeti na kwingineko au jamii hiyo itachagua kuua uhifadhi huo kwa maslahi ya watu wachache.

Hata hivyo, kwa kauli moja Malaigwanan wote walisema wanachagua kulinda uhifadhi wa Ngorongoro.

Alieleza umuhimu wa hifadhi ya Ngorongoro kitaifa na kimataifa akisema Watanzania wanajivunia kuwa katika nchi iliyobarikiwa kuwa na hifadhi hiyo.

“Mwenyezi Mungu ameiumba Tanzania akaipa eneo lenye msitu mkubwa na mlima ambao hudidimia kwenda chini, ambapo huko chini wanaishi wanyama wa kila aina ambao hawapatikani nchi nyingine, yanapatikana maji, mimea mbalimbali. Eneo hilo linaitwa Kreta ya Ngorongoro” alisema Majaliwa.

Tamko la Malaigwanan

Mwenyekiti wa Malaigwanan, Isack Ole Kisongo alisema wao kwa pamoja hawana mpango wa kubishana na Watanzania, kwani hivi sasa jamii ya Wamasai imesambaa nchi nzima na kwamba shughuli za kimaendeleo zinawahusu wote.

“Sisi Wamasai tumewahi kupisha eneo la Monduli ili jeshi liwepo, maeneo mengine mengi watu wamepisha maendeleo, watu wamepisha reli, watu wamepisha barabara, watu wamepisha viwanja vya ndege, wamepisha mto Rufiji ili maendeleo yapatikane, kuna nini Ngorongoro? Kwa nini kuna kelele? Hapo Mheshimiwa Waziri Mkuu nakuhakikishia kuna kikundi cha watu wachache kinachotumika kwa manufaa yao binafsi,” alisema Kisongo.

Mtazamo tofauti

Mratibu wa asasi ya Tanzania Land Alliance National Facilitation Land Coalitions (Mweupe) Bernald Baha alisema hoja zinazotumika kuondoa watu Ngorongoro zinahitaji utafiti shirikishi ili kufikia maamuzi ya pamoja.

“Hoja ya ‘maslahi ya Taifa’ imekua ikitumika vibaya kwa nia ya kuhalalisha kuhamisha wafugaji. Wananchi walipoteza eneo la ardhi kubwa kwa upande wa Serengeti na hivi sasa eneo hilo limeendelea kupunguzwa na kusababisha shida kubwa kwa wananchi.”

Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Laata Mekusi alisema wahifadhi wamekuwa wakitumia juhudi mbalimbali kupotosha kwamba wao ndio wahifadhi sahihi.

“Ukweli ni kwamba sisi ndio wahifadhi wa asili, wakazi hawali nyama za wanyamapori na ndiyo maana si tishio na hawa wanyama sisi ndiyo wahifadhi, tuna mikakati mbalimbali hata kujenga korido maalumu ambayo wanyama watapita.”

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa alisema kama watu hao wameanua kuondoka kwa hiari yao, ni jambo lisilokuwa na tatizo huku akitoa tahadhari kuwa ili kufanikisha hilo ni lazima Serikali ijiridhishe kuwa inaowahamisha ni wakazi wa eneo hilo kweli.

“Kama wataondoka wote pia kwa hiari ni jambo zuri, ila wanakwenda wapi, wanakaaje ni vitu ambavyo vinatakiwa kuwekwa wazi, pia wabunge inabidi wafuatilie...’’ alisema.

Post a Comment

0 Comments