Mbowe aongoza Kamati Kuu Chadema


        Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe leo Jumatano Machi 16, 2022 ameongoza kikao cha kamati kuu ya chama hicho baada ya kutoka gerezani alikokaa kwa miezi nane.

Machi 4, 2022 Mbowe na wenzake watatu walitoka gerezani baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na kesi iliyokuwa imefunguliwa dhidi yake na wenzake watatu katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi jijini Dar es Salaam.

Kikao hicho kinaendelea hivi sasa jijini Dar es Salaam ambapo wajumbe na viongozi waandamizi wa chama hicho wanashiriki na baadhi ya wajumbe akiwamo Tundu Lissu, Godbless Lema wakishiriki kwa njia ya mtandao.

Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi wa Itikadi, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema ajenda za kikao hicho ni pamoja na Mbowe kupokea taarifa za mwenendo wa chama tangu alivyokuwa gerezani hadi sasa.

Mrema amesema miongoni mwa ajenda za kikao hicho pia ni pamoja na mwenendo wa kisiasa nchini, maandalizi ya mkutano wa baraza kuu la Chadema utakaofanyika mwezi ujao.

 Ajenda nyingine ni pamoja na Mbowe kupokea taarifa za mwenendo wa chama tangu alivyokuwa gerezani hadi sasa.

“Leo ndio mara ya kwanza kwa Mbowe kushiriki kikao hiki baada ya kukaa gerezani miezi nane, ni kikao muhimu kwetu kwa sababu aliyekuwa akiendesha kikao kwa kipindi hicho ni makamu mwenyekiti wa Chadema Bara, Lissu.

“Ni kikao cha kumjulisha mwenyekiti (Mbowe), hali ya siasa, mwenendo wa chama na masuala mengine yanayoendelea. Baada ya kikao tutatoa taarifa rasmi kwa umma, yale yaliyojadiliwa na uamuzi uliofikiwa na kamati kuu,” amesema  John Mrema.

Wajumbe wengine waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na John Mnyika (Katibu Mkuu), Salum Mwalimu (Naibu Katibu Mkuu-Zanzibar), Benson Kigaila (Naibu Katibu Mkuu Bara). Wengine ni Suzan Kiwanga, Grace Kiwelu, Mchungaji Peter Msigwa, Catherine Ruge ambaye ni Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha).

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments