Mbowe ateta na RC, RPC Iringa

Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Iringa (RC), Queen Sendiga

Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Iringa (RC), Queen Sendiga na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa (RPC), Allan Bukumbi.

Mazungumzo hayo yamefanyika leo Jumatano Machi 9, 2022 katika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Iringa.

Akizungumza baada ya kikao hicho, Mbowe amesema baada ya kumaliza kazi ya Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) salama jana, aliona ni vyema kukutana na viongozi wa mkoa wa Iringa ili kuwaaga.

“Tumezungumza na Mkuu wa Mkoa pamoja na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa vilevile,” amesema Mbowe.

Amesema mazungumzo yao yalihusu yale ambayo walizungumza na Rais Samia Suluhu Hassan hasa kuhusu mshikamano, kusaidiana, upendo na kuheshimia ili kuifanya Tanzania kuwa mahali bora pa kuishi.

Amesema kikubwa walichozungumza ni kutanguliza haki katika utendaji wa kazi.

Kwa upande wake Sendiga amesema imekuwa siku njema ambayo inaleta mwanga mwingine wa siasa nchini Tanzania.

“Lengo la ugeni huu mbali ya kusalimia ilikuwa ni kuhusu masuala ya amani, mshikamano, umoja wa Tanzania na kuweza kufanya siasa zenye faida kwa Watanzania,” amesema.

Sendiga amesema amemuahidi Mbowe kufanya siasa njema kwa kila mmoja kufanya siasa kwa upande wake na kuheshimiana.

“Masuala ya mkoa yanatatuliwa na wanamkoa, sio kwenye mtandao. Mkoa wa Iringa tutaanza kuitenda hiyo amani kwa vitendo kama ambayo mmeona amani na utulivu ndio ambalo Rais Samia analitazama,” amesema Sendiga.

Post a Comment

0 Comments