Moto wateketeza ofisi za Tamesa Moshi

Moto mkubwa ambao chanzo chake bado hakijajulikana, unaendelea kuteketeza majengo na vifaa mbalimbali vya ofisi za Wakala wa Ufundi na Umeme (Tamesa) mjini Moshi na juhudi za kuizima ili usisambae zaidi zinaendelea.

Mashuhuda mbalimbali wameliambia gazeti hili kuwa moto huo ulianza saa 11:30 alasiri leo Machi 25,2022 katika ofisi hizo za Tamesa ambazo zimeshikana pia na Bohari ya Mafuta ya Serikali na ofisi za Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) mkoa wa Kilimanjaro zilizopo katikati ya mji wa Moshi.

Gazeti hili limeshuhudia jitihada mbalimbali za uokoaji zikiendelea ambapo waokoaji walikuwa wanajitahidi kuhamisha magari ya serikali na vifaa ili visifikiwe na moto huku wafanyakazi wa duka la samani lililoshikana na Tamesa, wao walifanikiwa kutoa samani na kuziweka barabara ya Kristu Mfalime kuelekea mzunguko wa magari wa Bonite.

Moshi mkubwa mweusi na moto ulionekana angani katika eneo hilo na wasiwasi ulikuwa kama moto huo utashindwa kudhibitiws kwa wakati, unaweza kusambaa hadi kwenye bohari ya mafuta ya serikali na ofisi za Tanroads.

Hakuna kiongozi yeyote wa Serikali aliyepatikana kuzungumzia moto huo, lakini Afisa Mtendaji wa Kiwanda cha Sukari cha TPC anayeshughulikia Utawala, Jaffar Ally aliliambia gazeti hili kwa simu kuwa tayari wametuma gari la Zimamoto kwenda Moshi kusaidia kuzima moto huo.

"Ni kweli nimepokea simu kutoka kwa mkuu wa wilaya ya Moshi juu ya moto huo mkubwa na tayari tumeshatoa gari letu limeelekea huko,"alisema Ally. Mji wa Moshi na mkoa mzima wa Kilimanjaro kws sasa hauna gari la zimamoto la Serikali na wanategemea zaidi gari za Zimamoto kutoka TPC.

Post a Comment

0 Comments