Mwanamke huwaza mara 70,000 kwa siku

Mkurugenzi wa Taasisi ya Jakaya Kikwete (JKCI) Profesa Mohamed Janabi

 Imeelezwa kuwa mwanamke ana wastani wa mawazo 70,000 kwa siku na inaaminika asilimia 70 huwaza vitu vya kufikirika au hasi jambo linalowafanya wengi kutozalisha kinga mwili za kutosha.

Hivyo kutokana na maumbile yake, anashauriwa kuacha kushindana na mwanaume kwa kuwa hujiongezea msongo wa mawazo na hivyo kuwa hatarini kupata mshtuko wa moyo.

Hayo yamesemwa leo Ijumaa Machi 11, 2022 na mbobezi wa magonjwa ya moyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Jakaya Kikwete (JKCI), Profesa Mohamed Janabi wakati akitoa mada katika mdahalo wa wanasheria wanawake uliyofanyika katika mtandao wa Zoom kuhusu mradi wa Mwanamke Imara unaotekelezwa katika mikoa mitatu.

“Unapoweka mashindano unajiweka hatarini kiafya, kila kitu unachokifanya leo kuanzia chakula unachokula, aina ya mazoezi unayoyachagua, namna unavyolala, msongo wa mawazo na unapokosa muda wa kupumzika haya yote yanaathiri kesho yako na afya yako baadaye,” amesema.

Profesa Janabi amesema hivyo ni miongoni mwa vihatarishi vinavyomfanya mwanamke awe katika hatari zaidi ya kupata kiharusi kuliko mwanaume.

Mradi wa Mwanamke Imara una lengo la kutokomeza aina zote za ukatili wa kijinsia unaotekelezwa kwenye mikoa hiyo na mashirika manne ambayo ni Chama cha Wanawake Wanasheria Tanzania (TAWLA), WILDAF, KWIECO na TANLAP Kwa ufadhili wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID).

Post a Comment

0 Comments