Tanga yaweka mikakati kukabili dawa za kulevya, wahamiaji haramu

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na maendeleo ya mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan.

 Mkoa wa Tanga umeweka mikakati ya kupambana na changamoto ya wahamiaji haramu, bidhaa za magendo na uingizwaji dawa za kulevya katika maeneo ya mpakani.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima amesema hayo leo Jumatano Machi 9, 2022 wakati akitaja maendeleo na mikakati ya mkoa huo alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari  kuelekea mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan madarakani.

Malima ametaja mikakati hiyo ni pamoja kuimarisha doria maeneo ya mpakani na kuhamasisha wananchi kutowaficha wageni ambao hawaeleweki wanaofika katika maeneo yao.

Amesema mkoa huo ndiyo mlango wa wahamiaji haramu ambao wanaingia kutoka Kenya wakiingia kupitia Wilaya ya Mkinga na kwamba katika uteuzi Rais Samia amelizingatia suala la usalama ambapo amemteua Kanali Kanali Maulid Surumbu na timu yake na wakuu wengine wa ulinzi na usalama wa kuongeza nguvu za doria ya maji na nchi kavu kwa hiyo tatizo limepungua kidogo.

Kama ilivyo kwa mikoa ya mipakani, Tanga inayo changamoto zake, sisi siyo tofauti na wengine, tuna changamoto zetu kama hizo hata. Hata nilipokuwa Mara tulikuwa na changamoto kama hizo, kimsingi tuna maeneo matatu hivi kama suala la uhamiaji haramu, uingizwaji dawa za kulevya kama mirungi magendo na bidhaa zilizotoka nje ya nchi ambazo hazilipiwi kodi au bidhaa zilizo chini ya viwango.

Hayo ni kwa upande wa masuala ya mpakani, katika masuala ya ndani hususani masuala ya uhalifu na ukatili wa jinsia ambavyo ni sugu vinaonekana pia kwenye maeneo mengine lakini sisi kwa Mkoa wa Tanga tumekuwa na mikakati ya makusudi ya kupambana na changamoto zote za ulinzi na usalama kwa kiasi kikubwa,” amesema Malima.

Malima amesema lakini suala hilo kwa sasa limepungua kiasi si kama ilivyokuwa miaka miwili au mwaka mmoja na nusu uliopita ambapo changamoto mojawapo kubwa katika ulinzi na usalama ambayo wanapambana nayo ni uhamiaji haramu.

Pamoja na mambo mengine, amesema lakini suala hilo lina mikataba na makubaliano ya kimataifa na kwamba Tanzania si wageni katika eneo hilo ambapo wanaliangalia baina ya Tanzania na Kenya Tanzania na Ethiopia na Somalia kidiplomasia na mikataba mingine.

Kwa hiyo wahamiaji haramu wanakuja na tunajaribu kutowaingiza kwa wingi lakini wanapoingia bado tunafanya taratibu zote za kidiplomasia na mikataba ya kimataifa katika kuwachukua, kuwahifadhi na baadaye kuwarudisha wanapotoka,” amesema Malima.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments