Pwani wamuombea Rais Samia, Hayati Magufuli

Viongozi 200 wa dini wameshiriki katika maombi maalumu ya kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan na aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, Hayati Rais John Magufuli.

Viongozi hao wamefanya maombi ikiwa ni siku tatu kabla ya Rais Samia kuhitimisha mwaka mmoja akiwa madarakani.

Rais Samia aliingia madarakani Machi 19, 2021 kuchukua nafasi ya aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, John Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, 2021 kwa maradhi ya moyo.

Leo Jumanne Machi 15, 2022 viongozi hao wa dini ya Kiislamu na Kikristo wamefanya maombi mjini Kibaha yaliyoambatana na uzinduzi wa kongamano la pamoja la amani litakalofanyika kwa wiki mbili.

Paroko wa Kanisa Katoliki Parokia ya Tumbi, Benno Kikudo katika maombi yake amemshukuru Mungu kwa kazi aliyoifanya Hayati Magufuli wakati wa uhai wake.

Pia Padre Kikudo amesema wanamshukuru Mungu kwa namna alivyompa nguvu na ujasiri Rais Samia tangu alipoingia madarakani ambapo kwa kipindi kifupi Taifa limeona utendaji wake wa mambo mengi ikiwemo amani kuendelea vizuri.

Kwa upande wake Sheihk Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Hamissi Mtupa ameombea ujenzi katika miradi yote mikubwa na ile ya kimkakati iendelee vizuri.

"Ee Mwenyezi Mungu Subuhana, Tunaiombea miradi yote iliyopo mbele ya Rais Samia Suluhu ikiwemo madaraja makubwa, barabara, Bwawa la Mwalimu Nyerere, Reli ya SGR, Bandari kavu na uwekezaji wa ndani na nje ifanyie wepesi ili ikamilike kwa wakati" amesema Sheikh Mtupa

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amewaeleza viongozi hao wa dini kuwa chagamoto nyingi zinazotokea kwenye jamii ikiwemo migogoro ya ardhi zinatokana na watu wengi kutoheshimu sharia.

"Taratibu za jinsi gani tuongoze, tusimamie zipo hakuna sababu ya kua na migogoro ya wakulima, wafugaji kwenye matumizi mengine ya ardhi huku umewekwa utaratibu tatizo ni uadilifu, yaani hatupo waadilifu lakini tumefika hapa tulipofika kuna changamoto wengine wanafanya makosa kwa makusudi, wengine kwa kudanganywa" amesema Kunenge

Kunenge amesema ndani ya mwezi huu Mkoa huo utafungua maeneo ya viwanda vikubwa (industrial park) katika eneo la Kwala Kibaha na kwamba tayari wameshapata wawekezaji.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments