Raila Odinga anapanda, Wiliam Ruto amebaki palepale


Sifa ya Mlima Kenya ni pambo la barafu na theluji kwenye vilele vyake. Ukiwa na kimo cha futi 17,058, unabeba hadhi ya kuwa mlima wa pili kwa urefu Afrika nyuma ya Kilimanjaro, Tanzania.

Karne ya 15, jamii ya kabila la Wakikuyu ilihamia eneo la kuzunguka Mlima Kenya. Kabila hilo, kwa imani yao ni kuwa maeneo yote ya mlima huo yana upako mtakatifu. Wakikuyu huuita mlima huo kwa jina la Kirinyaga, wakimaanisha “mlima wenye nuru”.

Kwa mujibu wa imani hiyo ya Wakikuyu, Mungu wao ambaye humwita Ngai, aliumba Kirinyaga (Mlima Kenya), kisha akampa zawadi mwasisi wa kabila hilo, Gikuyu, ardhi yote chini ya Kirinyaga, halafu akampandisha mpaka kileleni. Ndiyo maana Wakikuyu walifanya Mlima Kenya kuwa makazi yao tangu Karne ya 15.

Wakikuyu huamini kuwa Ngai (Mungu), alimwelekeza Gikuyu kuwa wakati wowote angepatwa na shida, angepaswa kutoa sadaka, halafu anyooshe mikono kuielekea Kirinyaga (Mlima Kenya), kisha Ngai angetokea kutatua tatizo husika. Hiyo ni sababu ya Wakikuyu kuuchukulia Mlima Kenya kwa utakatifu wa hali ya juu.

Kutoka Karne ya 15 mpaka 21, hesabu mpaka Novemba 2019, Wakikuyu wanaoishi Mlima Kenya wamefikia 8.5 milioni. Hiyo ni kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi Kenya, iliyofanyika mwaka 2019 chini ya Mamlaka ya Taifa ya Takwimu Kenya (KNBS).

Watu hao kwa sasa ndio ambao wanatajwa kushikilia turufu ya urais kwenye Uchaguzi Mkuu Agosti 9, mwaka huu, kati ya Naibu Rais, William Ruto na Kiongozi wa Upinzani, Raila Odinga. Na swali gumu kwa sasa ni nani ataibuka kuwa shujaa wa siasa za Mlima Kenya baada ya Rais Uhuru Kenyatta kukaa pembeni?

Uhuru yupo madarakani kwa nguvu kubwa ambayo aliipata kutoka Mlima Kenya. Tangu mwaka 2013, Uhuru amekuwa kiranja wa siasa za Mlima Kenya, akifuata nyayo za baba yake, Jomo Kenyatta, Rais wa Kwanza wa Taifa la Kenya. Vilevile, Mwai Kibaki, Rais wa Pili wa nchi hiyo, alijijengea ushujaa katika siasa za Mlima Kenya kwa wakati wake. Wote hao ni Wakikuyu.

Wakili mashuhuri Kenya, Ahmednasir Abdullahi, ametoa maoni yake kuwa ili mtu ashinde urais Kenya Agosti mwaka huu, atahitaji kupata kura milioni 10 mpaka 11. Akasisitiza kwamba iwe Raila, iwe Ruto, kama mmojawapo hataungwa mkono Mlima Kenya, hatavuka kura milioni nne.

Hoja ya Wakili Ahmednasir ndiyo imechagiza mvutano kati ya Raila na Ruto uwe mkubwa. Mmoja kati yao atakayeweza kushawishi mamilioni ya wapiga kura Mlima Kenya, moja kwa moja atakuwa amejitengenezea nafasi kubwa ya kuapishwa kuwa rais baada ya Uhuru kumaliza muda wake.

Tayari Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Mlima Kenya (My Kenya Foundation wameshajitokeza na kutangaza hadharani kuwa watamuunga mkono Raila. Tamko la Mt Kenya Foundation lilisababisha Ruto naye afanye ziara eneo hilo kujaribu kutafuta kuungwa mkono.

Wakati huohuo, viongozi wa Chama cha Jubilee eneo la Mlima Kenya wamesema kuwa matumaini yao makubwa ya kunyanyuka na kushinda majimbo yapo kwa Rais Uhuru, mara akifanya ziara kwenye miji ya eneo hilo. Uhuru ndiye Kiongozi wa Jubilee.

Uhuru na Ruto ndio waasisi wa Jubilee, na wao ndio walikuwa viongozi wa juu wa chama hicho, kabla ya Ruto kuamua kutoka na kuanzisha chake kipya, United Democratic Allience (UDA), ambacho kimekuwa kikipata umaarufu mkubwa siku za karibuni.

Februari 26, mwaka huu, Uhuru akihutubia kongamano la kitaifa la Jubilee, alisema kuwa chama chake hakijafa na atafanya kampeni nzito ya kuhakikisha muungano wao wa Azimio la Umoja, unashinda uchaguzi.

Msimamo wa Uhuru una nafasi kubwa ya kuamua nani atapata nini Mlima Kenya. Japo eneo hilo lenye kaunti 10 kati ya 47 za nchi hiyo, lina makabila mengine kama Wameru, Waembu na Wamasai, lakini idadi kubwa kabisa ni Wakikuyu, ndiyo maana Uhuru kwa sababu ni Mkikuyu, inadhaniwa ataweza kuzielekeza kura nyingi kwa Raila. Kabla ya tofauti zilizojitokeza kati ya Ruto na Uhuru, ilidhaniwa kuwa uchaguzi ungekuwa mwepesi kwa Ruto na Jubilee. Ripoti ya sensa ya watu na makazi Kenya, ilionesha kuwa ngome za Ruto na Uhuru, zilibeba watu karibu nusu ya Kenya nzima. Majimbo ngome za wanasiasa hao waliowahi kuunda “upacha wa kisiasa”, yana watu milioni 22. Wakenya wapo zaidi ya milioni 47, hiyo ni kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2019.

Ngome za Raila, Nyanza, Mashariki na Pwani, idadi ya watu ni milioni 16.4. Kiongozi wa Wiper Democratic Movement-Kenya (WDM-K), Stephen Kalonzo Musyoka, ngome yake inayozunguka kabila la Wakamba, idadi ni watu milioni 3.5.


Nani ni nani?

Kwa hesabu ya idadi ya watu kulingana na sensa ya mwaka 2019, jumlisha siasa za ukabila Kenya na jiografia, ni rahisi kutamka kuwa Raila atashida urais Kenya Agosti 9, mwaka huu.

Anza kwa kuchukua ngome zake zenye watu milioni 16, piga hesabu milioni 8.5 Mlima Kenya, hapo ni zaidi ya watu milioni 24.5. Idadi hiyo ya watu inazidi nusu ya watu wote wa Kenya, kama walivyorekodiwa kwenye sensa ya mwaka 2019.

Ruto anabaki anategemea eneo la Rift Valley, ambalo lina watu zaidi ya milioni 12.8. Ruto ni Mkalenjin. Na Rift Valley ni nyumbani kwa makabila mawili, Wakalenjin na Wamasai. Na mgawanyiko wa kisiasa uliopo Kenya kwa sasa, hutegemei Ruto ataungwa mkono kwa kishindo Rift Valley.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments