RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) kuandaa kanuni zitakazoelekeza jinsi ya kufanya mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Wajumbe wa Kikosi Kazi cha Kuratibu Maoni ya Wadau wa Demokrasia ya Vyama vingi vya Siasa leo tarehe 12 Machi, 2022, Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais (Ikulu), Bi. Zuhura Yunus leo Machi 12, 2022.
Kupitia taarifa hiyo, Mheshimiwa Rais Samia ametoa maelekezo hayo leo Machi 12, 2022 baada ya kupokea maazimio ya awali kutoka kikosi kazi alichokiteua cha kufuatilia hoja zilizojitokeza katika mkutano wa wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa uliofanyika jjiini Dodoma, Desemba 15 hadi 17, 2021.
Rais Samia amemwagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. Balozi Pindi Chana kushirikiana na Tanganyika Law Society (TIS) pamoja na Zanzibar Law Society (ZLS) kutengeneza kanuni hizo.
Kikosi kazi hicho chenye wajumbe 24 na ambacho kinawajibika moja kwa moja kwa Rais, kiliwasilisha maazimio hayo Ikulu jijini Dodoma.
Aidha, taarifa hiyo imeeleza kuwa maazimio hayo yamegawanyika katika makundi matatu ya muda wa utekelezaji ambapo azimio la muda mfupi ni la kanuni zitakazoelekeza jinsi ya kufanya mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha kuratibu Maoni ya Wadau wa Demokrasia ya Vyama vingi vya Siasa Profesa Rwekaza Mukandala pamoja na Wajumbe wa Kikosi Kazi hicho mara baada ya mazungumzo yao leo tarehe 12 Machi, 2022, Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.(Picha na IKULU).
Pia kuna baadhi ya maazimio ya muda wa kati ambayo ni pamoja na rushwa na maadili katika uchaguzi, ruzuku, elimu ya uraia, huku masuala yanayohusu Uchaguzi na Katiba mpya vikiwa ni mpango wa muda mrefu.
0 Comments