RC atoa agizo kwa ofisa elimu Kilimanjaro

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai amemwagiza ofisa elimu wa Mkoa huo, kufanya mchakato wa kuipandisha hadhi shule ya Sekondari Kwambegu iliyopo Wilaya ya Same, kuwa na kidato cha Tano na Sita

Kagaigai ametoa maagizo hayo wakati alipofanya ziara ya kukagua miradi ya madarasa yaliyojengwa kwa kutumia fedha za Uviko 19 kwa ajili ya kupunguza msongamano wa wanafunzi ambao amesema ameridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo.

Amesema kutokana na shule hiyo kuhudumia kata 14 inayo hadhi ya kuwa na kidato cha Tano na Sita ili wanafunzi watakaoamaliza kidato cha nne katika kata hizo waweze kujiunga na kidato cha Tano.

"Nimeambiwa kuna kata 14 zinazoizunguka kata hii, Ofisa Elimu wa Mkoa ukiwa chini ya Katibu Tawala wa Mkoa,angalieni uwezekano wa kuifanya hii shule ipate kidato cha tano,"amesema Kagaigai

"Kwa hiyo Ofisa Elimu chini ya Katibu Tawala mfuatilie muone uwezekano huu wa kupata kidato cha tano kwenye eneo hili kwa ajili ya kuhudumia na kusaidia kata hizi 14 zinazozunguka shule hii hapa,"

Pamoja na mambo mengine ameipongeza Wilaya hiyo kwa kusimamia vyema ujenzi wa miradi ya madarasa ambapo amesema madarasa yamejengwa kwa viwango vinavyotakiwa na kuwasisitiza wanafunzi kuweka bidii katika masomo.

Akizungumza Mkuu wa shule hiyo, Godwin Kitale amesema shule ilianza mwaka 2017 ina jumla ya wanafunzi 670 ambapo mwaka jana wanafunzi wote 185 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza  wamejiunga na shule hiyo.

"Shule hii ilianza mwaka 2007 na imekuwa ni msaada kwa kata zote 14 zinzoizunguka shule hii kwa kuwapunguzia watoto wetu kutembea umbali mrefu,"amesema Mwalimu Kitale

Post a Comment

0 Comments