Ripoti Ya Mto Mara Yaibua Maswali: Mwenyekiti Wa Uvccm(M) Singida Nae Asema

M/kt,Uvccm(M) Singida Dr.Denis Nyiraha
Wakati taarifa ya kamati maalum iliyochunguza mabadiliko ya maji katika mto Mara ikitaja kinyesi cha mifugo na uozo wa mimea kuwa chanzo, wadau mbalimbali wameonyesha mashaka na kushauri uchunguzi wa kina wa kimaabara ufanyike kuondoa hofu kwa umma.

Machi 19, 2022 Mwenyekiti wa kamati maalum ya kitaifa iliyoundwa na Serikali kuchunguza mabadiliko ya maji ya mto huo, Profesa Samuel Manyele alisema chanzo ni kiwango kikubwa cha kinyesi cha mifugo mtoni pamoja na uozo wa mimea ndani ya mto hasa mimea vamizi kama vile magugu maji na matete.

Maswali yaibuka

Hata hivyo, kauli hiyo imeibua maswali kadhaa, ikiwamo kama kuna uwezekano wa kinyesi cha mifugo kuua samaki na viumbe wa majini.

Pia wapo waliouliza uwepo wa mabadiliko hayo hivi sasa, ilhali mifugo hiyo ikielezwa kuwapo kwa muda mrefu na pia uwezekano wa mifugo hiyo kutoa kiasi kikubwa cha kinyesi kiasi cha kuhatarisha usalama wa mto huo unaomwaga maji yake Ziwa Victoria.

Inawezekanaje Kinyesi, Mkojo Wa Ng'ombe Walio Hai Na Hawaumwi ( Organic Materials) Vipelekee Vifo Vya Samaki ?? Kama Ndvyo Basi Kamati Ituambie Chemical Na Biological Effect Ya Kinyesi Na Mkojo Afu Huo Mkojo(21lts) Na Kinyesi(25kg) kwa Ng'ombe, Walikuwa Wanautoa Sehemu moja Tu !

Maswali hayo yamekuja wakati awali ripoti iliyotolewa na Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB) Machi 12, ikionyesha kuwapo kwa kiwango kikubwa cha mafuta yaliyosababisha kukosekana kwa hewa ya oksijeni kwenye maji ya mto na kusababisha samaki kufa.

Akitoa uzoefu wake, Lawrence Kitogo ambaye ni mvuvi katika ziwa Victoria mkoani Mwanza alisema kinyesi cha mifugo hutumika kurutubisha mazalia ya samaki.

“Utafiti unaweza kubainisha kama kinyesi kinaua, ila ninavyojua kinyesi hicho hutumika kama chakula cha mifugo. Kwa wanaofuga samaki hutumia kinyesi hasa cha kuku kurutubisha mabwawa kabla ya kuanza kuweka samaki,” alisema.

Kauli hiyo iliungwa mkono na mfugaji mwingine wa samaki, Lucas Malembo aliyesema: ‘Kinyesi cha mifugo hutumika kama mbolea kwenye mazalia ya samaki na kinasaidia kurutubisha mimea ya majini.”

Kutokana na sintofahamu hiyo, Chadema kimeiomba Serikali kufanya uchunguzi wa kina wa kimaabara kujua ukubwa wa tatizo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza jana, mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, John Heche alisema Serikali inatakiwa kuchunguza suala hilo kwa kina kwa sababu linahusu maisha ya watu.

“Mto Mara ndio chanzo kikuu cha maji kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya binadamu na mifugo katika wilaya za Tarime, Serengeti, Rorya na Butiama. Uchunguzi wa kina wa kimaabara lazima ufanyike kuwaondoa hofu wananchi ambao bado wanatilia shaka kuwa madhara yalitokana kinyesi, mikojo ya mifugo na uozo wa mimea,” alisema Heche

Mbunge wa Viti Maalum, Neema Rugangira pia alikosoa matokeo ya utafiti huo akisema bado yanafikirisha na kushauri iundwe kamati nyingine kufanya uchunguzi.

“Muhtasari wa ripoti ya uchunguzi kuhusu vifo vya samaki kwenye mto Mara umeniacha na Maswali mengi, majibu tuliyopewa yananitia wasiwasi kwani nimetumiwa siku mbili nikijielimisha kwa kuwasiliana na wabobezi kuoka ndani na nje ya nchi, hivyo nashauri uliundwe kamati nyingine ijumuishe wabunge,” aliandika katika ukurasa wake wa Twitter.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM wilaya ya Tarime Godfrey Francis alisema ripoti hiyo imejaa ubabaishaji huku akimshauri Waziri anayehusika na mazingira kuacha kuitumia.


Jafo, Sagini watetea ripoti

Akizungumza na wakazi wa kijiji hicho, mbunge wa Butiama, Jumanne Sagini alisema: “Serikali haiwezi kuua watu wake, kama kungekuwa na shida lazima ingesema; ndio maana kabla hatujajua tatizo Serikali ilizuia matumizi ya maji ya mto Mara.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma jana Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dk Seleman Jafo alitetea ripoti ya uchunguzi wa maji ya mto Mara akisema baadhi ya watu wanaipotosha kutokana na kuisoma vipande vipande.

Ili kuondoa mkanganyiko na upotoshaji, Dk Jafo aliagiza ripoti hiyo iandikwe kwa lugha nyepesi ili iwafikie wananchi wengi.

Chanzo Mwananchi

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments