Ruto azidi kupokea vipigo kisiasa

Safari ya kuelekea Uchaguzi Mkuu Kenya Agosti 9, mwaka huu ni ngumu kila upande, lakini upande wa Naibu Rais William Ruto unazidi kupata vipigo vya kisiasa.

Kiongozi wa chama cha Narc-Kenya, Martha Karua ni pigo jingine kwa Ruto. Martha ametangaza kuwa yeye na chama chake wameamua kumuunga mkono mgombea urais wa Azimio la Umoja, Raila Odinga.

Martha alitoa tamko hilo juzi (Machi 22), Serena Hotel, Nairobi, baada ya kusaini makubaliano na Raila.

Awali, ilidhaniwa kuwa Martha angechagua kusimama na Ruto baada ya awali kuonekana kutokubali kujiunga na Azimio la Umoja.

Martha ni mmoja wa viongozi wa Umoja wa Vyama vya OKA (One Kenya Alliance). Wengine katika umoja huo ni Gideon Moi, Moses Wetang’ula, Musalia Mudavadi na Kalonzo Musyoka.

Mwishoni mwa mwaka jana, Rais Uhuru Kenyatta aliitisha kikao na viongozi wa OKA kilichofanyika Ikulu ya Mombasa. Lengo lilikuwa kuushawishi umoja huo umuunge mkono Raila kwa sababu ndiye pekee anayeweza kumshinda Ruto.

ADVERTISEMENT

Gideon, Wetang’ula, Mudavadi na Kalonzo walihudhuria, isipokuwa Martha. Kitendo hicho kilitoa picha kuwa Martha na chama chake, Narc Kenya, hawakuwa upande wa Raila, bali kwa Ruto.

Hata Kalonzo na Gideon walipotangaza kusimama na Raila kwa ushawishi wa Uhuru, huku Martha na Narc Kenya wakiwa kimya, ilizidi kutengeneza minong’ono kuwa wao wanamuunga mkono Ruto.

Martha baada ya kujiunga na Azimio la Umoja, alisema: “Nipo hapa kuthibitisha kuwa Narc Kenya tunaunga mkono Azimio. Bila uadilifu katika uongozi ahadi ni sawa na bure.” Maneno hayo “bila uadilifu kwenye uongozi”, yametafsiriwa kuwa dongo kwa Ruto kuwa si mwadilifu.

Msemaji wa kampeni za Raila, Profesa Makau Mutua alisema ni furaha kwao kwa Martha na Narc Kenya kujiunga na Azimio. Mutua alimtaja Martha kama mwanasiasa mahiri na mwenye heshima kubwa Kenya.


Pigo lingine la Ruto

Martha na Narc Kenya wanajiunga na Azimio, kipindi ambacho imepita wiki moja tu tangu mbunge wa Sirisia, John Waluke aasi kambi ya Ruto na kurejea chama cha Jubilee, kinachoongozwa na Rais Uhuru. Jubilee ni chama kinachounga mkono Azimio la Umoja.

Ilikuwa Machi 18, mwaka huu, Waluke alipobisha hodi makao makuu ya Jubilee, akapokewa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Jeremiah Kioni, kisha akalipia fomu ya kuomba kuteuliwa tena kugombea ubunge jimbo la Sirisia, kwa tiketi ya Jubilee.

Kabla ya uamuzi huo, Waluke alikuwa mstari wa mbele kufanya kampeni za Ruto na aliwaongoza wabunge wengine wa Kaunti ya Bungoma, Didmus Barasa (Kimilili), Dan Wanyama (Webuye West) na Mwambu Mabongah (Bumula), kumuunga mkono Ruto katika Kaunti ya Bungoma.

Waluke hajarejea Jubilee peke yake, isipokuwa na wabunge wenzake, Barasa, Wanyama na Mabongah.

Na baada ya uamuzi huo, Waluke alisema kuwa Kaunti ya Bungoma ni ngome ya Jubilee. Kabla hajachepuka Waluke ndiye alikuwa Mwenyekiti wa Jubilee Kaunti ya Bungoma.

Hayo ni ya Waluke na wenzake kwenye Kaunti ya Bungoma, upande mwingine, Kaunti ya Turkana, Ruto amekutana na kipigo kingine baada ya wabunge watatu kujiunga na Jubilee, hivyo kuunga mkono Azimio.

Wabunge kutoka Turkana waliojiunga na Jubilee ni James Lomenen (Turkana Kusini), Ali Lokiru (Turkana Mashariki) na mbunge wa wanawake Turkana, Joyce Emanikor. Awali, wabunge hao walitangaza kumuunga mkono Ruto.

Tayari Lomenen, Lokiru na Joyce walikuwa wameshajiunga na chama kipya kilichoanzishwa na Ruto, cha United Democratic Alliance (UDA), na kuwa upande wa umoja wa Kenya Kwanza, lakini ghafla wamehamia Azimio kupitia Jubilee.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Jubilee, Kanini Kega alisema baada ya Lomenen, Lokiru na Joyce kujiunga “Turkana ni ukanda wa Jubilee.” Leo, nimewapokea Emanikor (Joyce), Lomenen na Lokiru Ali kwenye chama chetu. Wameachana na United Democratic Alliance (UDA).”


Kwa nini anakimbiwa?

Jibu la swali hilo limetoka kwa mwanasiasa mmoja tu aliyejiengua kambi ya Ruto na kujiunga Azimio -- Waluke. Kabla ya kuhamia Jubilee, Waluke alikosoa uamuzi wa Kenya Kwanza kumkaribisha Wetang’ula.

Alisema kitendo cha Wetang’ula ambaye ni Kiongozi wa Ford Kenya kujiunga na Kenya Kwanza, kungesababisha kudumaa kwa maisha ya kisiasa ya kwake binafsi na wenzake.

Zipo fununu kuwa Wateng’ula amekubaliana na Ruto kwamba atakuwa mgombea mwenza wa Kenya Kwanza. Wafuasi wengi wa Ruto hawakubaliani na Wetang’ula kuwa mgombea mwenza na baadaye Makamu wa Rais wa Kenya kama watashinda uchaguzi.


Pigo la Uhuru

Upande wa Uhuru, pigo alilopata hivi karibuni ni uamuzi wa mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria kutangaza hadharani kumuunga mkono Ruto, kwa maelezo kuwa wananchi wa Gatundu na Mlima Kenya wametendewa mema mengi na Naibu Rais.

Gatundu ni nyumbani kwa Uhuru, ambaye ameshaweka bayana kuwa anataka Raila ndiye awe Rais na si Ruto. Kuria alisema Ruto ndiye aliwaokoa wananchi wote wa Mlima Kenya katika unyanyasaji wa kisiasa, hivyo anasimama na UDA pamoja na Kenya Kwanza.

Ni pigo kwa Raila kwa sababu yalikuwa matarajio makubwa kwamba Kuria angechagua upande wa Azimio, hata hivyo ni maumivu kwa Uhuru kwa sababu akiwa Rais, anashuhudia mbunge wa nyumbani kwake anampinga na kumfuata mpinzani wake.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments