Sh339 milioni kumaliza kero ya maji Kigembe

 Wakazi zaidi ya 3,937 wa kijiji cha Kigembe, wilaya ya Kasulu wataondokana na adha ya upatikanaji wa huduma ya majisafi katika kijiji hicho mara baada ya Serikali kutoa zaidi ya Sh339 milioni kwa ajili ya ujenzi wa mradi mkubwa wa maji.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao wamesema tangu kuanzishwa kwa kijiji cha Kigembe mwaka 1976, wamekuwa wakitumia maji ya visima na madimbwi ambayo si salama kwa afya zao.

Mtendaji wa kata ya Kigembe, Idd Manioza amesema wananchi hao wamekuwa wakitumia maji pamoja na mifugo hasa katika kipindi cha kiangazi katika mito na chemichemi zilizopo kijijini hapo na kusababisha magonjwa mbalimbali ya mlipuko kwa watumiaji.

Amesema mradi huo wa maji utakapokamilika utaweza kusaidia wananchi wake kwa kufata maji karibu lakini majisafi na salama na kuepukana na magonjwa ya mlipuko kama homa ya matumbo, kichocho na kipindupindu.

Mkazi wa kijiji cha Kigembe, Wilbada Shabani amesema mradi huo ukikamilika utasaidia kufanya shughuli za kimaendeleo maana watakuwa na muda wa kutosha tofauti na awali muda mwingi walikuwa wakitumia kutafuta maji.

“Wake zetu wamekuwa wakishindwa kufanya majukumu mengine ya nyumbani ya kuangalia familia na shughuli za uzalishaji mali kwa maendeleo ya kijiji chetu na kushinda kutafuta maji kwaajili ya matumizi ya nymbani hivyo kama mradi huu utakamilika utasaidia kutatua kero hizo,” amesema Shabani.

Mkazi mwingine wa kijiji cha Kigembe, Husna Ramadhani amesema mradi huo ukikamilika utasaidia watoto kusoma kwa uhuru kwani baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwahusisha watoto kwenda kuchota maji na kushindwa kwenda shule kwa wakati.

Akizungumzia mradi huo Meneja wa Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira (Ruwasa) Wilaya ya Kasulu, Mhandisi Edward Kisalu amesema mradi unatarajiwa kukamilika mwezi Machi na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

Amesema mradi huo ulianza kujengwa kijiji hapo mwaka 2021, ambapo umeambatana na ujenzi wa tanki lakuhifadhia maji la lita za ujazo 100,000 pamoja na ujenzi wa vituo kumi vya kuchotea maji.

Mradi huu utatumia umeme jua (solar) ambapo hadi utakapokamilika utagharimu zaidi ya kiasi cha Sh339 milioni na kuhudumia watu zaidi ya 3,937 wa kijiji cha Kigembe na kwamba malengo ya mradi huo ni kuwapunguzia wananchi adha ya kufata maji umbali mrefu na kuwapunguzia magonjwa ya mlipuko,”amesema Kisalu.

Aidha Serikali wilayani humo pia inatekeleza mradi wa ujenzi wa tanki la kuhifadhia maji lenye lita za ujazo 500,000 ambapo ujenzi huo unafadhiliwa na shirika la Maendeleo la Ubelgiji (ENABEL), kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania.

Kisalu amesema mradi huo umeanza kutekelezwa mwaka 2021 na wanatarajia kukamilika Aprili, 2022 na mradi huo utahudumia maeneo ya kasulu mji ambapo ni mitaa mitano ya zaidi ya watu 25,000 ambapo itakuwa ni ongezeko la asilimia nne kati ya wakazi wote wa wilaya nzima ya Kasulu ambao ni 784,902.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments