SINGIDA WATAKIWA KUFANYA VEMA KWENYE ANUANI ZA MAKAZI ASEMA DC PASKALI MULAGIRI

Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskasi Mulagiri akizungumza  wakati akifunga mafunzo ya uhabarisho wa anwani za makazi na postikodi kwa wadau mbalimbali yaliyofanyika wilayani hapa jana.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Singida Yagi Kiaratu akizungumza kwenye mafunzo hayo.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)  Wilaya ya Singida Mjini, Lucia Mwiru akizungumza kwenye mafunzo hayo.
Afisa Tarafa  Mungu Maji, Ally Mwendo akizungumza kwenye mafunzo hayo.
Mwenyekiti wa Dini mbalimbali Mkoa wa Singida Hamis Kisuke akichangia jambo kwenye mafunzo hayo
Meneja wa Mfuko wa  Pensheni kwa Watumishi wa Umma,   (PSSSF ) Mkoa wa Singida, Beda Mgonja akizungumza kwenye mafunzo hayo.
Mafunzo yakiendelea.
Wadau wakiwa kwenye mafunzo hayo.
Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Mkoa wa Singida, Oscar Kalimilwa akichangia jambo kwenye mafunzo hayo. Kulia ni Meneja wa PSSSF Mkoa wa Singida, Beda Mgonja.
Mchungaji Yona Mbogo wa Kanisa la Moravian Singida akichangia jambo kwenye mafunzo hayo.
Mafunzo yakiendelea.
Afisa Miliki kutoka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Mkoa wa Singida Israel Ngapona akichangia jambo kwenye mafunzo hayo.
  Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu (BAKWATA) Mkoa wa Singida Burhan Mlau akichangia jambo kwenye mafunzo hayo.

MKUU wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskasi Mulagiri amewaomba viongozi mbalimbali na wananchi wilayani hapa kutofanya makosa na kuichafua heshima waliyopewa ya kushiriki moja kwa moja zoezi la uandaaji anwani za makazi na postikodi.

Muragili alitoa ombi hilo wakati akifunga mafunzo ya uhabarisho wa anwani za makazi na postikodi kwa wadau mbalimbali yaliyofanyika wilayani hapa jana.

Wadau walioshiriki mafunzo hayo ni 275 wakiwemo watendaji wa kata, mitaa, maafisa elimu wa kata,wakuu wa shule, walimu wakuu, wenyeviti wa mitaa, vijiji, viongozi wa dini, wazee maarufu, wakuu wa idara na vitengo pamoja na madiwani.

"Tunapokwenda kutekeleza mambo yote tuliyojifunza hapa nawaomba tukayasimamie vizuri ili tuweze kufanikiwa na si vinginevyo" alisema Muragili.

Muragili alisema zoezi la uandaaji anwani za makazi na postikodi linahitaji ushirikishwaji wa hali ya juu katika ngazi zote hasa inayomuhusu mwananchi moja kwa moja ambapo aliwataka washiriki kuwa makini na kuziepuka dosari zote ambazo zinaweza kuharibu utekelezaji wa zoezi hilo.

Alisema kutokana na mafunzo hayo waliyopata na kuwepo kwa viongozi mbalimbali walioshiriki mafunzo anaamini zoezi hilo litakwenda kufanyika kwa mafanikio makubwa.

Aidha Muragili alisema ili zoezi hilo liweze kufanyika vizuri na kuweza kuonekana katika kiwango kinachohitajika linagharama kubwa ambazo haziwezi kuepukwa kwani zipo gharama ambazo zitabebwa na Serikali Kuu,Halmashauri na zipo gharama ambazo zitabebwa na wananchi hivyo wasiogope kuzipokea.

Alisema gharama hizo zikishuka kwenye ngazi ya mwananchi zinakuwa sio kubwa bali ni ndogo zaidi akitolea mfano wa kubandika vibao vidogo vya mitaa na vya namba za nyumba ambavyo vipo ndani ya uwezo wao ukilinganisha na kazi kubwa iliyofanywa na serikali ya kutoa mafunzo na mambo mengine.

Alisema kazi hiyo ya kuweka vibao hivyo vya mitaa lipo ndani ya uwezo wao na Serikali haiwezi kuweka vibao hivyo kila sehemu hivyo aliomba vibao hivyo vyenye rangi njano na maandishi meusi na nguzo zake viwekwe na watu wa mtaa husika kwa kuzingatia utaratibu watakao elekezwa na Manispaa ili viwekwe kwa mpangilio na kuwa na mandhari nzuri.

Baadhi ya wadau mbalimbali waliokuwepo kwenye mafunzo hayo wakitoa maoni yao akiwepo Meneja  wa Mfuko wa  Pensheni kwa watumishi  (PSSSF ) Mkoa wa Singida, Beda Mgonja akizungumza kwenye mafunzo hayo.    PSSSF Mkoa wa Singida Beda Mgonja alisema mpango wa anwani za makazi na postikodi una manufaa makubwa hapa nchini hasa katika mashirika yao ambayo yanafanya kazi na jamii.

"Sisi tunafanya kazi na jamii hasa wastaafu ambao mara kwa mara tumekuwa tukionana nao kwa ajili ya kuwalipa fedha zao hivyo mpango huu wa anwani za makazi utatusaidia kuwafikia kiurahisi kwenda nyumbani kwao na kuwapunguzia adha ya kuja ofisini kwetu ukizingatia wastaafu wengi ni wazee na wanakuwa hawana uwezo wa kutembea" alisema Mgonja. 

Akitoa mchango wake Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu (BAKWATA) Mkoa wa Singida Burhan Mlau alisema Anwani za makazi na postikodi zitawasaidia wageni wanaofika mjini hapa kuwapata jamaa na ndugu zao maeneo wanayoishi kwa kuwaelekeza boda boda mtaa na namba ya nyumba walipo tofauti na sasa ambapo hakuna majina ya mitaa wala namba za nyumba.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Singida Yagi Kiaratu alisema Manispaa imetambua umuhimu wa wadau mbalimbali kushirikishwa katika zoezi la uwekaji anuani za makazi na postikodi na kuwa watasaidia kutekeleza kwa wakati mpango huo ambao kwa wilaya hiyo ili kuifanya kazi hii kuwa shirikishi na hivyo kuleta wepesi katika utekelezaji ambapo kwa mkoa wa Singida wanatakiwa kukamilisha zoezi hilo Aprili 15 mwaka huu na kitaifa mwezi Mei.

Alisema Mpango huu una manufaa mengi  ikiwa ni pamoja na kuongeza ufanisi  katika utawala bora kwa kutambua makazi ya raia wote nchini, kuimarisha usalama, kuboresha utoaji huduma za Jamii na kuongeza pato la taifa kwa kuboresha ukusanyaji wa kodi mbalimbali.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)  Wilaya ya Singida Mjini, Lucia Mwiru alimpongeza Ofisi ya Mkurugenzi kupitia kamati ya kuratibu zoezi hilo na akaonesha imani yake kuwa kwa maandalizi hayo Halmashauri ya Manispaa ya Singida itaongoza katika kukamilisha mpango huo.

Na Dotto Mwaibale, Singida

Post a Comment

0 Comments