Tasaf yatumia Sh10.465 bilioni Manyara

Mnufaika wa kaya masikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii nchini (Tasaf) wa Kijiji cha Magugu Wilayani Babati Mkoani Manyara, Neema Laizer (kushoto) akiwaonyesha baadhi ya viongozi wa Tasaf ngazi ya Taifa, vifaa mbalimbali vya nyumbani walivyotengeneza baada ya kuwezeshwa na Tasaf. Picha na Joseph Lyimo
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) kwa kipindi cha miaka miwili mkoani Manyara umetoa Sh10.465 bilioni kwa walengwa wa mpango wa kunusuru kaya maskini na kubadilisha maisha yao.

Mratibu wa Tasaf Mkoa wa Manyara, Rashid Shedafa ameyasema hayo mjini Babati mbele ya kamati ya uongozi ya kitaifa ya Tasaf.

Shedafa amesema walifanya uhaulishaji wa fedha kwa walengwa wa Tasaf awamu ya tatu kipindi cha pili ambapo zoezi lilianza Februari 2020 hadi Februari 2022.

Amesema kati ya fedha hizo Sh9.799 bilioni ni kwa ajili ya walengwa na Sh665.4 milioni kwa ajili ya ufatiliaji na usimamizi kwa ngazi ya mkoa na halmashauri.

Ameyataja mafanikio ya mpango wa Tasaf awamu ya tatu ni mahudhurio ya watoto shuleni yameongezeka sababu wazazi wameelimishwa, watoto walio chini ya miaka mitano wanahudhuria kliniki kwa ajili ya kupata huduma za afya.

Amesema walengwa wameweza kuboresha makazi yao na wengine wametoka nyumba za paa ya nyasi na kuhamia katika nyumba za paa ya bati.

Mwenyekiti wa kamati ya uongozi ya kitaifa ya Tasaf, Dk Charles Mwamwaja amesema umasikini ni vita kubwa wanatakiwa kuweka mikakati ya kupambana nao.

Dk Mwamwaja amewataka walengwa kutumia vizuri fedha wanayopewa ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tasaf Taifa, Ladislaus Mwamanga amewahakikishia kuwa watu wenye sifa ambao hawajaingizwa kwenye mpango wataingizwa.

Mnufaika wa mfuko wa Tasaf wa kijiji cha Minjingu, Neema Laizer amesema yeye ni mjane amefanikiwa kuanzisha mradi wa kutengeneza vifaa vya nyumbani vya ukili ikiwemo mapambo na mikeka na kufanikiwa kusomesha watoto wake.


Post a Comment

0 Comments