Uboreshaji wa mazingira ya utoaji wa elimu na ufadhili wa mafunzo ya ujuzi katika mwaka mmoja wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan madarakani

Wanafunzi wa shule ya sekondari Karibuni wakijifunza matumizi ya Kompyuta zilizotolewa na Shirika la BRAC - Maendeleo Tanzania kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa.

 Tangu aingie madarakani Machi, 2021 Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameonyesha kwa vitendo azma yake ya kuboresha sekta ya elimu nchini.

 Serikali yake ya Awamu ya Sita imeendelea kuweka kipaumbele katika kutenga na kuelekeza fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi inayolenga kuinua na kuboresha elimu nchini.

Vilevile Serikali imetoa fedha kufadhili programu za mafunzo ya ujuzi kuwezesha watanzania kupata ujuzi na stadi za kazi ili wawezi kuajiriwa au kujiajiri wenyewe katika shughuli za uzalishaji mali.

Sekta ya Elimu inapewa kipaumbele cha juu nchini kutokana na mchango wake mkubwa katika kufanikisha maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla. Mhe. Rais amekuwa akisisitiza mara zote kwamba kila mtoto wa kitanzania ana haki ya kupata elimu ambapo Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imekuwa ikifanya jitihada za makusudi kuhakikisha inaboresha miundombinu ya elimu ili kuongeza upatikanaji wa elimu bora na kwa usawa nchini. Jukumu hili la kusimamia na kuboresha miundombinu ya elimu linatekelezwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Mamlaka ilianzishwa kwa Sheria ya Mfuko wa Elimu Na.8 ya mwaka 2001 ikiwa na jukumu la kusimamia uende-shaji wa Mfuko wa Elimu wa Taifa.

TEA ilianzishwa kwa lengo la kuongeza nguvu za Serikali kugharamia miradi ya elimu yenye kuinua upatikanaji wa elimu bora kwa usawa katika ngazi zote za elimu kwa Tanzania Bara na elimu ya juu kwa Tanzania Zanzibar.

Mamlaka ya Elimu Tanzania inatambua umuhimu wa kushirikisha wadau wa elimu katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu yake kikamilifu. Katika mwaka 2021 iliandaa Kongamano la kwanza la wadau wa elimu kwa lengo la kujadili namna wadau watakavyoweza kuchangia katika miradi ya elimu nchini.

Wadau hao walitoka katika taasisi za umma na taasisi binafsi ambapo Mamlaka ilitumia fursa hiyo kuwatambua na kuwatunuku vyeti wachangiaji wa sekta ya elimu nchini.

Mkutano huo umenza kuzaa matunda ambapo TEA imesaini Makubaliano Maalum ya Ushirikiano (MoU) baina yake na Shirika la BRAC-Maendeleo Tanzania kwa ajili ya kushirikiana katika kuboresha miundombinu ya elimu nchini.

Kutokana na makubaliano hayo jumla ya Kompyuta 120 (Mpakato 60 na Vishikwambi 60) zenye thamani ya Sh. Milioni 132.6 zimetolewa katika shule tatu za Manispaa ya Temeke ambazo ni Wailes, Miburani na Karibuni kwa ajili ya mradi wa TEHAMA unaofahamika kama Skills for Their Future unaolenga kutoa mafunzo ya kidijitali kwa vijana wa shule za sekondari ili kuwawezesha kupata fursa mbali mbali za kuboresha maisha yao.

pic3

Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Bahati I. Geuzye.

TEA pia inashirikiana na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) katika utekelezaji wa Mradi wa kuboresha miundombinu ya Shule zilizopo katika maeneo jirani na Hifadhi za Taifa.

Mradi huu wenye thamani ya Sh. Bilioni moja unatekelezwa kwa muda wa miaka mitatu. Taasisi ya Asilia Giving inafadhili mafunzo ya Utalii na Huduma za ukarimu kwa wanafunzi wanaotokea katika jamii zinazozunguka hifadhi za Taifa.

Wanafunzi 35 wamefadhiliwa masomo katika Chuo cha VETA cha Hoteli na Utalii kilichopo Arusha (VHTTI). Mamlaka pia imepokea tani tano za mabati kutoka Kampuni ya Yalin Global Company Limited yenye thamani ya Sh. milioni 12 ambayo yaligawiwa katika shule za msingi Ugindoni na Rahaleo katika Manispaa ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam na shule tatu za msingi za Maleshi, Majengo na Kazaroho zilizoko Halmashauri ya Wilaya ya Babati Mkoani Manyara.

Kwa kushirikiana na Taasisi ya Flaviana Matata TEA, imetekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba za walimu katika shule ya Msingi Msinune iliyopo Wilaya ya Chalinze Mkoani Pwani.

Taasisi ya Flaviana Matata imechangia Shilingi milioni 100 katika mradi huo. Utekelezaji wa Miradi kwa ufadhili wa Mfuko wa Elimu Katika kipindi cha mwaka mmoja tangu Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imeendelea kutekeleza kwa mafanikio makubwa miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo, nyumba za waalimu, maabara za sayansi katika shule za sekondari kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa.

pic5

Nyumba nne za walimu katika Shule ya Sekondari Kassim Majaliwa iliyoko kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi.

Miradi hii inalenga kusaidia kuinua ubora wa elimu na upatikanaji wake kwa usawa nchini kama ambavyo Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2021/22-2025/26 umejielekeza kuboresha mifumo ya elimu, kuwianisha elimu na mahitaji ya soko la ajira, ikiwa ni pamoja na kuchochea uvumbuzi na matumizi ya teknolojia.

Mfuko huu wa Elimu wa Taifa unaendeshwa kwa fedha zinazotengwa kila mwaka na Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na wafadhili wengine yakiwemo mashirika ya umma na ya binafsi. Katika kipindi cha mwaka mmoja tangu mwezi Machi, 2021, kiasi cha Sh. Bilioni 12.2 zimetumika kugharimia miradi ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya elimu inayofadhiliwa na Mfuko wa Elimu wa Taifa.

Katika fedha hizo Sh. bilioni 9.3 zimetumika katika ujenzi wa madarasa, nyumba za walimu, maabara, matundu ya vyoo, miundombinu kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum, ofisi za walimu na mabweni.

Miradi mingine ya ujenzi wa vyumba 210 vya madarasa katika shule 70, maabara 2 za sayansi, matundu 1920 ya vyoo kwenye shule 80 inaendelea katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Mbali na ujenzi huo, TEA pia imefanikiwa kufanya ukarabati na ujenzi katika shule 11 kongwe za Sekondari katika awamu ya pili.

Shule zilizonufaika ni Shule ya Sekondari Pugu, Tanga-ufundi, Kilakala, Same, Mwenge na Msalato. Zingine ni shule ya sekondari Kondoa, Korogwe, Nganza, Tabora wavulana na Bwiru wasichana.

Maboresho ya miundombinu katika shule hizo yamejumlisha ujenzi na ukarabati wa mabweni, maabara, mabwalo ya chakula, miundombinu ya maji na umeme, vyumba vya madarasa pamoja majengo ya utawala. Sh. Bilioni 1 zimetumika kwenye ukarabati huo wa awamu ya pili.

Katika kuunga mkono jiti-hada za Serikali za kuhamia Dodoma na ongezeko la watumishi wa umma na wananchi kuhamia katika Mji Mkuu wa nchi Dodoma, Mamlaka ya Elimu Tanzania iliona kuna umuhimu wa kuboresha na kukarabati baadhi ya shule za msingi ili kukabiliana na ongezeko la wanafunzi katika Mji huo Mkuu.

Mradi huo ulilenga kukarabati na kupanua miundombinu ya shule za msingi Kizota, Medeli, Kisasa na Mlimwa C ukarabati huo umegharimu Sh.Bilioni 1.9. Utekelezaji wa Miradi kwa ufadhili wa Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) Mamlaka ya Elimu Tanzania imeendelea kutekeleza miradi ya kukuza ujuzi kupitia Mfuko wa Kuend-eeza Ujuzi (SDF).

Mfuko huu unaratibiwa chini ya Pro-gramu ya Kuendeleza Elimu ya Ujuzi na Mafunzo ya Stadi za Kazi Zenye Kuleta Tija katika Ajira (Education and Skills for Productive Jobs- ESPJ) na Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Kukuza na Kuendeleza Ujuzi Nchini (National Skills Develop-ment Strategy-NSDS).

TEA imeendelea kutekele-za majukumu yake sanjali na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2021/22 - 2025/26 ambao umejielekeza katika kuboresha mifumo ya elimu, kuwianisha elimu na mahitaji ya soko la ajira, ikiwa ni pamoja na kuchochea uvumbuzi na matumizi ya teknolojia. Hili linatekelezeka kupitia usimamizi na uratibu wa ufadhili wa programu mbalimbali kupitia mfuko wa SDF.

Mfuko wa SDF unalenga kukuza ujuzi kwa watanzania na kuwawezesha kujiajiri au kuajiriwa kwa urahisi na kuchangia uchumi wa Taifa. Katika kipindi cha mwaka mmoja tangu Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani jumla ya wanufaika 19,264 wamepata fursa ya mafunzo kutoka katika sekta sita za kipaumbele zilizoainishwa na mpango.

Sekta hizo ni; Kilimo na Kilimo Biashara, Utalii na Huduma za Ukarimu, Uchukuzi, Ujenzi, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na Nishati.

Hitimisho

Mamlaka ya Elimu Tanzania ina jukumu la kutekeleza miradi ya kuboresha miundombinu ya elimu nchini ili kuendeleza elimu na mafunzo kulingana na mipango na sera za kitaifa kwa lengo la kukidhi mahitaji ya kijamii na kiuchumi kupitia ufadhili wa miradi.

Pia kuishauri Serikali juu ya vyanzo vingine vya uhakika vya mapato kwa ajili ya Mfuko wa Elimu wa Taifa na kuhamasisha upatikanaji wa rasilimali fedha za kutosha na endelevu.

Madhumuni ya Mfuko wa Elimu wa Taifa ni kuongeza nguvu za Serikali katika kugharamia miradi ya elimu, ili kuinua ubora wa elimu na upatikanaji wake kwa usawa.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments