Waandishi wa habari watakiwa kulainisha tafiti

Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia nchini Tanzania (COSTECH) imewataka waandishi wa habari kuandika habari za sayansi kwa kutumia lugha rahisi katika matokeo ya tafiti zinazofanywa na watafiti hapa nchini ili ziweze kuwafikia walengwa wakiwemo wananchi ili waweze kufanya maamuzi.

Rai hiyo imetolewa leo Jumatano Machi 16, 2022 na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dk Philibert Luhunga wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari na watafiti wa Kanda ya Kaskazini yanayofanyika mkoani Arusha.

Mafunzo hayo yamelenga kuwapa mbinu waandishi wa habari 25 kutoka mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro ya namna ya kuripoti babari za ubinifu, sayansi na teknolojia.

"Watafiti wamekuwa wakifanya kazi kubwa za kitafiti ambazo zina matokeo mazuri lakini matokeo haya huandikwa kwa lugha ya kisayansi zaidi na kuchapishwa kwenye machapisho ya kimataifa, hivyo tunaomba waandishi waweze kuyatafsiri matokeo haya kwa lugha nyepesi zaidi ili yaweze kutumiwa na jamii," amesema Dk Luhunga

Amesema endapo tafiti hizo zikiandikwa kwa lugha rahisi na zikawafikia walengwa wakiwemo wananchi itawasaidia kufanya maamuzi mbalimbali na katika kutatua changamoto zao za kila siku.

Mratibu wa mafunzo hayo kutoka (COSTECH), Deusidedith Leonard amesema mafunzo hayo yatasaidia kuziba pengo kati ya waandishi wa habari, wahariri pamoja na watafiti katika kuwasilisha taarifa za sayansi na teknolojia kwenye jamii.

"Mafunzo haya yatatoa fursa ya kubadilishana uzoefu wa kubaini mbinu bora ambazo zitatuwezesha kufikisha taarifa za Kitafiti kwa lugha rahisi na kutafsiriwa vizuri ili ziweze kuwafikia walengwa wakiwemo watunga sera, wafanya maamuzi, wazalisha mali na wananchi kwa ujumla,"amesema Leonard

Kwa upande wake mwezeshaji mkuu wa mafunzo hayo, DkBakari Msangi amewataka watafiti hao kuandika kwa ufupi machapisho ya tafiti zao ili iweze kumpa nafasi msomaji kusoma kwa urahisi bila kuchoka.

"Chapisho linapokuwa fupi linamvutia mtu kusoma, wanadamu wana shughuli nyingi, hawana muda wa kusema wanasoma tuu, unakuta mtu anafikiria mambo mengi, mimi nawashauri hawa wanaofanya tafiti zao wafanye chapisho fupi linaloweza kusomwa na watu wengi,"amesema Dk Msangi

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments