Wabunge wapendekeza mfuko wa maafa utengewe bajeti

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Dk Pindi Chana

Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria imeshauri mfuko wa maafa kutengewa bajeti yake itakayosaidia kutatua changamoto zinazotokana na maafa badala ya kusubiri hadi yatokee na kuanza kutafuta wadau kwa ajili ya kutoa huduma.

Hayo yamesemwa na makamu mwenyekiti wa kamati hiyo, Najma Giga katika semina ya wajumbe wa kamati hiyo kuhusu dhana na mfumo wa usimamizi wa maafa nchini iliyoandaliwa na ofisi ya waziri mkuu, sera, Bunge na uratibu.

“Kuna maafa ya kimaumbile ambayo huenda yakatokea kila mwaka  kutokana na mvua za masika  au mabadiliko ya tabianchi kwenye fukwe zetu. Tunajua kabisa kila mwaka mabadiliko ya tabia nchi yanapotokea sehemu ya ardhi inaliwa lakini ikitokea maafa ndio tunaanza kupambana kutafuta wadau,”amesema.

Kwa mujibu wa kitengo cha mawasiliano serikalini cha ofisi ya ya waziri mkuu sera, Bunge na uratibu, Najma amehoji kwanini serikali isione jinsi ya kuweka utaratibu maalumu kwa watu wanaosaidia shughuli hizo za maafa.

Akizungumza katika semina hiyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu,  Dk Pindi Chana amesema Serikali inaendelea kuweka mikakati madhubuti ya namna ya kujikinga na kukabiliana na maafa ili kuepuka madhara makubwa yanayoweza kujitokeza na kuhatarisha usalama wa raia pamoja na kuharibu miundombinu.

 “Hivi sasa mheshimiwa mwenyekiti nikuhakikishie elimu inayotolewa katika shule zetu za msingi Sekondari na  ngazi ya vyuo vikuu inalenga vijana wetu na jamii yetu  kujua Maafa kwa ujumla ili kujikinga wasipate madhara,” amesema Dk Pindi.

Kwa upande wake, naibu katibu mkuu ofisi ya waziri mkuu sera, Bunge na uratibu,  Kaspar Mmuya amefafanua kwamba Muswada wa Sheria ya Maafa utasaidia kuondoa changamoto zilizobainika kutokana na sheria ya zamani.

Pia amesema itasaidia wahusika kufahamu majukumu yao ili kuepusha mwingiliano wa majukumu wakati wa utekelezaji wa shughuli zote za maafa.

Akihitimisha wasilisho la dhana na mfumo wa usimamizi wa maafa katika semina hiyo mkurugenzi msaidizi kutoka Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Charles Msangi amesema Muswada wa Sheria ya Maafa umezingatia uwajibikaji wa wadau wote kwani ulifanyika utafiti ambao uliangalia majukumu ya kila mdau .

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments