Wafungwa wanaomaliza vifungo kupewa mitaji

Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mbeya ,Kamishna Msaidizi, Adriano Mduda .

 Mbeya. Jeshi la Magereza Mkoa wa Mbeya limesema litaanza kuwawezesha kiuchumi wafungwa wanaomaliza kutumikia vifungo kwa kuwapa nafasi ya kushiriki kwenye miradi ya ujenzi katika taasisi za Serikali, kilimo na ufugaji.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Magereza mkoa huo, Kamishna msaidizi, Adriano Mduda leo Ijumaa Machi 11, 2022 wakati akisema wameona ni vyema kuwepo kwa utaratibu huo kutokana na uzoefu wa ushiriki wao kwenye miradi ya uzalishaji mali katika magereza mkoani hapo.

''Kwa sasa kuna baadhi ya miradi ambayo inasimamiwa na Magereza Mbeya. Ujenzi wa hospteli za Chuo cha Biashara (CBE) Kilimo na mifugo, ambayo inafanywa na wafungwa ambapo sehemu ya fedha tunazopata kupitia miradi hiyo tunazitunza kwa ajili ya kuwasaidia wanapomaliza muda wao magerezani '' amesema.

Asema upande wa kilimo katika msimu huu gereza la kilimo Songwe  zimelimwa eka 800 za mahindi huku 150 zikiwa za kilimo cha umwagiliaji kiwango ambacho ni kikubwa na kupelekea kuweza kulisha Magereza mengine nchini.

''Kutokana na uzalishaji huo kuwa mkubwa tuna mikakati ya kuanzisha mradi wa kiwanda cha usindikaji unga wa sembe na kusambaza katika masoko mbalimbali jambo ambalo litaingiza kipato ambacho sehemu kitawanufaisha ''amesema.

Mduda ameeleza kufurahishwa kwake na agizo la Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera kutaka kila halmashauri zote kutenga fedha kwa ajili ya kuwasaidia wafungwa wanaomaliza muda wao magerezani.

''Kimsingi hoja ya Mkuu wa Mkoa imekuja wakati mzuri kwani utaunga mkono mipango yetu ya kusaidia kundi hili maalum linaporejea kwenye jamii zetu likawe chachu ya kubuni na kuanzisha miradi ya Maendeleo''amesema.

Hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera aliagiza halmashauri zote kutenga fedha kwa ajili ya kuwezesha wafungwa wanaomaliza muda wa kutumikia vifungo ili wanaporudi kwenye jamii waanzishe miradi na kuwa mifano ya kuigwa.

Homera alitoa agizo hilo Machi 8 mwaka huu wakati akizungumza na viongozi mbalimbali wa Serikali kwenye maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani ambapo kimkoa ilifanyika Wilaya ya Mbeya.

''Wakuu wa wilaya, wakurugenzi kwenye bajeti zenu hakikisheni mnaona namna ya kusaidia kundi hilo maalum la wafugwa wanaomaliza muda magereza kupata mitaji ili wasirejee tena magerezani ''alisema.

Mkazi wa Mbeya, Adamson Samson amesema Serikali imefanya jambo jemakwa kuwakumbuka watu walio katika kundi hilo kuwawezesha kupata fedha za mitaji na kwamba itawasaidia kutorejea kwenye uharifu.

 Na Hawa Mathias

Post a Comment

0 Comments