Wazazi wa mwanafunzi Mtanzania wasimulia alivyonusurika Ukraine


 Siku sita za milio ya silaha kali za kivita na hali ya taharuki katika miji mbalimbali ya Ukraine imemsababishia madhara ya kisaikolojia mwanafunzi Hairat Muhina (20), aliyewasili juzi nchini baada ya kupitia machungu ya aina yake katika historia ya maisha yake.

Binti huyo ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Tiba cha Kharkiv (KNMU), aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) juzi na kupokewa na familia yake kwa machozi ya furaha, lakini hali yake ikabadilika ghafla.

Akizungumza na Mwananchi jana nyumbani kwake, baba mzazi wa Hairat, Kapteni Hanafi Muhina alisema “Usiku (juzi) baada ya kutoka uwanja wa ndege, tulipofika hapa nyumbani alibadilika. Alikuwa analia sana, tukaona hali ile haikuwa ya kawaida, leo (juzi) ameamka pia hayuko sawa na yuko chumbani muda wote hataki kutoka wala kuzungumza,” alisema.

Mwananchi halikuweza kuzungumza na binti huyo kutokana na hali aliyokuwa nayo, ingawa baba yake alisema awali aliwaeleza kuwa hakulala siku tano mfululizo.

Muda wote alikuwa akisikia milipuko umbali wa mita kama 300 kutoka maeneo aliyokuwa akiishi kwenye handaki.

Muhina anasema siku tatu baada ya bintiye kuondoka mji wa Kharkiv, wanajeshi wa Russia waliokuwa wanatumia parachuti waliingia katika mji huo wa pili kwa ukubwa na kusababisha uharibifu mkubwa.

“Tumebaini ile hali ya mapigano imemuathiri kisaikolojia, kwa sababu hajawahi kusikia wala kushuhudia mabomu na silaha zikipigwa. Nasema hivyo kwa sababu alipokuwa kule, alishuhudia majengo ya nyumba za jirani yakilipuliwa kwa mabomu.

“Alikuwa anapiga picha anatutumia, kila wakati anasema baba, ‘wamelipua tena nyumba jirani’, hivyo tunawatafuta wataalamu wa saikolojia waweze kumsaidia,” alisema Muhina, ambaye pia ni rubani wa ndege.

Je, aliwezaje kuondoka eneo alilokuwa akiishi, akijibu swali hilo, Muhina anasema ubinti huyo alimweleza kuwa uongozi wa chuo chao ulisitisha masomo siku moja kabla ya shambulio la Russia, kwa maelekezo ya kuendelea kusoma kwa njia ya mtandao hadi hali ya utulivu itakaporejea nchini humo.

Hivyo, baada ya tangazo hilo, familia iliamua kumkatia tiketi Hairat kumwezesha kurejea nchini kupitia Shirika la Ndege la Qatar.

Anasema Februari 25, Hairat na wenzake watano kati ya tisa wanaosoma chuoni hapo, walifanikiwa kupata usafiri wa treni kutoka Kharkiv hadi mji wa Lviv ulioko magharibi mwa Ukraine, ambapo walitumia siku mbili njiani.

“Lakini kabla ya kuondoka aliniandika meseji, ‘baba ninawapenda sana wazazi wangu, kama nimewakosea naomba mnisamehe, ninaanza safari ya kuja, lolote linaweza kutokea.’”

“Meseji ilinitoa machozi. Niliumia sana na alisambaza meseji hiyo kwa ndugu zake wengine, niliona mwanangu amekata tamaa ya kuishi,” alisema Muhina.

Hata hivyo, Muhina anasema hata baada ya kufanikiwa kufika mpaka wa Poland, binti huyo alimwambia hali ilikuwa ngumu zaidi kutokana na msongamano wa watu uliokuwapo.

“Tulikuwa tunawasiliana nao kila baada ya saa moja, kwa sababu walipoondoka Kharkiv walibeba begi la vyakula vikavu kama mikate na kuku walikuwa wakila njiani, lakini sisi huku nyumbani hatukuwa na amani na hatukuwa na muda wa kumpuzika kabisa, nashukuru amefika yuko salama,” anasema Muhina.

Hivyo, Februari 28 waliamua kuondoka mpaka wa Poland na kuelekea mpaka wa Hungary na wakafanikiwa kuvuka.

Muhina alisema wanafunzi wenzake wanne aliofika nao Hungary, aliwaacha hapo baada ya wao kukosa tiketi, lakini baadaye alikutana na wanafunzi wengine watatu waliosafiri ndege moja hadi Tanzania.

“Tunashukuru Jumanne jioni aliondoka na ndege ya Qatar iliyoanza safari yake katika mji wa Bucharest na asubuhi jana (juzi) akaingia nchini,” alisema Muhina.

Muhina anasema kwa sasa kila akimtazama Hairat na akikumbuka ujumbe wa simu aliokuwa akimtumia, anaonekana ni mtu aliyekuwa ameshakata tamaa.

“Na hii ndiyo inanipa mwanga kuwa ameathirika sana kisaikolojia, ujumbe mfupi aliokuwa akiandika na kuusambaza kwetu sisi familia, ulituonyesha amekataa tamaa kabisa ya kuendelea kuishi, alipoteza matumaini hata sasa naona kama haamini kama amesalimika,” alisema.

Anasema binti huyo alikuwa akiishi peke yake Kharkiv, nyumba ambayo ilikuwa umbali wa kilomita mbili kutoka chuoni.

“Baada ya kusikia milipuko ya mabomu siku ya kwanza, alihamia nyumba ya jirani zake Watanzania na wakajiunga kwenye group la WhatsApp kwa ajili ya kupata mawasiliano zaidi ya namna ya kujiokoa,” anasema Muhina.

Samiha Muhina, dada wa Hairat anasema “kwa sasa tumeamua kumuondoa kwenye mitandao ya kijamii, akaunti yake ya Instagram tumeizuia hadi baadaye atakapokuwa sawa.”

Muhina ametoa rai kwa Serikali iendelee kuwasiliana na mamlaka husika ili kuwaokoa na kuwasaidia Watanzania wengine waliokwama warejee nchini.

Msimamo wa Tanzania

Wakati vita hivyo vikiendelea, Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi 35 kati ya nchi 193 wanachama wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ambazo hazikupigia kura azimio la Umoja wa Mataifa kulaani uvamizi wa Russia dhidi ya Ukraine.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine alisema “Tunafahamu kuhusu hilo na tutalijibu baadaye.”

Katika kikao cha dharura kilichofanyika juzi, nchi 141 kati ya 193 zilipigia kura kukubali azimio hilo, 35 hazikupiga kura na tano zilipinga azimio hilo.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments