****************
Na. John Mapepele
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewakata wachezaji wa timu ya soka ya wanawake chini ya umri wa miaka 17 kucheza kombe la dunia litakalofanyika nchini India mwaka huu, huku akiipa jina la Serengeti Girls na kutaka waendeleze kipigo kwa mchezo wa marudiano wa kufuzu kombe la dunia dhidi ya Botwana utakaofanyika machi 20, 2022 nchini Botswana.
Mhe. Mchengerwa ametoa kauli hiyo leo Machi 11, 2022 baada ya kuitembelea timu hiyo iliyo kaa kambini Zanzibar tangu Februari 23, 2022 ambako inaendelea na mazoezi kwa ajili ya mchezo wa marudiano na timu ya Botswana baada ya kuichabanga timu hiyo mabao saba kwa nunge.
Ameongeza kuwa watanzania wana matarajio makubwa na timu hiyo kuwa italinda na kutetea heshima Taifa letu ndiyo maana ameamua kuipa jina la Serengeti kwa kuwa hifadhi hiyo ina heshima kubwa duniani kubwa.
“Nimeamua kuwapa jina hilo la Mbuga yetu ya Serengeti kutokana na ukweli kuwa Mbuga yetu inaheshimika ni matarajio yetu kuwa mtaendelea kutuheshimisha hata katika mchezo unaokuja hivi karibuni na wapinzani wetu Botswana”amesisitiza Mhe. Mchengerwa
Mhe. Mchengerwa ametumia ziara hiyo kuzungumza na wachezaji na kuwapa hamasa na mbinu mbalimbali za kuweza kushinda na kuwataka wawe nidhamu ya kutosha, umahiri na moyo wa kujituma wakiwa mchezoni.
Aidha, Mhe. Mchengerwa amezungumza na benchi la ufundi pamoja na viongozi wa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) na na Shirikisho la Soka la Zanzibar (ZFF) na kuwataka kuendelea kushirikiana kikamilifu na Serikali katika kuendeleza mchezo wa soka kwa kuzingatia weledi wa mchezo huo.
Amepongeza hatua ya ushirikiano uliopo baina TFF na ZFF ambapo amesema ushirikiano unapaswa kuendelezwa katika michezo yote ili kuendelea kuibua na kunoa vipaji vya wachezaji ambao wataliwakilisha taifa la Tanzania kimataifa.
“Nimefarijika sana kuona vijana wetu wamekaa kambini hapa Unguja tangu tarehe 23 Februari 2022 huu ndio uzalendo na ushindi kwenye sekta zetu”. Amefafanua Mhe. Mchengerwa.
0 Comments