Augustine Mrema alivyoshinda ubunge Temeke, ajiuzulu kisha kuhamia TLP


 Baada ya Augustine Mrema kushindwa katika uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi uliofanyika Oktoba na Novemba 1995, aliendelea kubaki kuwa Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi.

Baada ya uchaguzi huo jumla ya kesi 128 zilizohusu uchaguzi mkuu huo zilifunguliwa Mahakama Kuu. Wafungua mashtaka walikuwa wanapinga matokeo ya majimbo hayo kwa madai ya haki kukiukwa wakati wa uchaguzi.

Mgawanyiko wa kesi hizo kikanda (idadi ikiwa katika mabano) ulikuwa kama ifuatavyo: Arusha (13), Dar es Salaam (21), Tabora (21), Ruvuma (9), Mtwara (1), Mwanza (14), Kilimanjaro (5), Mbeya (16), Kagera (10) na Dodoma (9).

Hata hivyo, Mahakama Kuu, Jumanne ya Februari 26, 1996 ilifuta kesi nane zilizohusu kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 1995 baada ya wafungua mashtaka kuwasilisha maombi ya kuondoa kesi hizo.

Kwa upande mwingine, Machi 25 kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa Jimbo la Kinondoni ilifutwa baada ya wakili wa upande wa mashtaka, Dk Masumbuko Lamwai kutoonekana mahakamani.

Richard Masanja na wenzake waliofungua kesi hiyo nao hawakufika mahakamani. Jaji aliyekuwa akiisikiliza kesi hiyo, Augusta Bubeshi akaifuta. Waliokuwa walalamikiwa katika kesi hiyo ni Peter Kabisa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Kisa cha Mrema kutimuliwa uwaziri, kuwania urais kupitia NCCR

Ingawa kesi nyingi zilifutwa, kesi iliyofunguliwa kupinga ushindi wa Mbunge wa Temeke, Ally Ramadhani Kihiyo, haikufutwa.

Kesi hiyo ilifunguliwa na waliokuwa wagombea wa NCCR-Mageuzi, Richard Tambwe Hiza na wa Chadema, Beatrice Mtui na watu wengine wanne ambao ni wananchi wa kawaida.

Ilipoanza kusikilizwa, shahidi wa kwanza wa upande wa walalamikaji alikuwa Richard Tambwe Hiza. Jumatano ya Mei 29, 1996 Kihiyo alilazimika kujiuzulu ubunge huku kesi dhidi yake ikingaali inaendelea Mahakama Kuu.

Wakili wake, William Erio alimweleza Jaji Dan Mapigano aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo kuwa amepata nakala ya barua ya mteja wake aliyomwandikia Spika wa Bunge na kutiwa saini na Katibu wa Bunge, George Mlawa ya kujiuzulu kiti hicho kwa sababu ya matatizo ya afya.

Siku hiyohiyo Spika wa Bunge, Pius Msekwa alitangaza rasmi kuwa kiti cha ubunge Jimbo la Temeke kiko wazi. Papo hapo Mrema alianza kutajwa kuwania kiti hicho.

Jumamosi ya Juni 1, 1996 Mrema akiwa Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi alisema hajaamua wala hajasema kuwa atagombea kiti hicho na kwamba alishangaa kusikia kuwa atagombea wakati yeye hajasema hivyo.

Siku iliyofuata, Jumapili ya Juni 2, wananchi kadhaa walipiga simu katika baadhi ya vyombo vya habari kueleza mapenzi yao kwa Mrema na kumtaka agombee jimbo la Temeke.

Hatimaye hukumu ya kesi dhidi ya Kihiyo ikasomwa Julai 25, 1996—hiyo ikiwa ni miezi minne tangu ilipoanza kusikilizwa.

Katika hukumu hiyo Jaji Mapigano alisema Chama cha Mapinduzi (CCM) na aliyekuwa mbunge wa jimbo la Temeke kwa tiketi ya chama hicho, Ally Kihiyo walitoa rushwa kuwashawishi wapiga kura katika uchaguzi uliompa ushindi Kihiyo.

Akitoa hukumu ya kesi hiyo, Jaji Mapigano alisema “imethibitishwa mahakamani” kuwa CCM na mgombea wake walitoa rushwa kwa wapiga kura na kwamba ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande wa walalamikaji na wale wa utetezi unaonyesha kitendo cha wananchi kupewa pilau, kanga na fedha ilikuwa ni kutoa hongo kwa lengo la kuchaguliwa.

Hukumu hiyo iliyosomwa kwa muda wa saa 3 na dakika 20, ilisema kuwa wananchi wa kata ya Bulyaga jimboni humo walipewa pilau kwenye mkutano ambao Kihiyo kabla ya kuhutubia aliwaambia huo ni mwanzo tu na akichaguliwa watafaidi zaidi.

Jaji alisema shahidi wa nne upande wa walalamikaji, Peter Odhiambo na shahidi wa 16, Selina Ngalipeka waliithibitishia mahakama juu ya vitendo vya rushwa na maji, kanga na fulana ziligawanywa kwa lengo la kumchagua Kihiyo.

Baada ya kiti cha ubunge wa Jimbo la Temeke kutangazwa kuwa wazi kutokana na kujiuzulu kwa Kihiyo, Jumapili ya Julai 7, 1996 Mrema alitangaza rasmi uamuzi wake wa kugombea ubunge wa jimbo hilo na kusema anataka kupata tiketi ya kuikosoa Serikali kupitia vikao halali.

Mrema alisema hayo wakati akifungua kongamano la siku moja la wanawake wa NCCR-Mageuzi lililofanyika katika ukumbi wa Imasco Center, Temeke. Alisema hawezi kuikosoa CCM akiwa mitaani. Mrema alipitishwa na chama chake kugombea kiti hicho.

Kwa upande mwingine, Jumatatu ya Julai 7, Kamati Kuu ya CCM ilimteua Abdul Omari Mtiro maarufu kwa jina la Cisco-Kid, kugombea ubunge wa jimbo hilo.

Kwa upande mwingine, Julai 10, Richard Hiza Tambwe, ambaye mwaka uliotangulia aligombea kiti hicho kupitia NCCR-Mageuzi, aliamua kugombea kiti hicho kwa mara nyingine kupitia Chama cha Wananchi (CUF) huku NCCR ikisema hatua hiyo ya Tambwe kugombea kupitia CUF imemfukuzisha uanachama.

Uchaguzi huo ulifanyika Jumapili ya Oktoba 6, 1996. Matokeo ya uchaguzi huo (idadi ya kura ikiwa katika mabano) yalikuwa kama ifuatavyo:

Augustine Mrema kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi (54,840), Abdul Cisco Mtiro wa CCM (33,113), Hiza Tambwe wa CUF (3,324), Alec Che Mponda wa TPP (515) na Mege Omar wa UMD (422).

Wengine ni Samson Msambara kwa tiketi ya Chadema (217), Legile Msonde wa UPDP (162), Ndembe Abdallah wa Pona (120), Rashid Mtuta wa NRA (114), Brighton Nsanya wa NLD (69), Shabaan Matembo wa UDP kuwa 67,

Rachel Mutayoba wa TLP (62) na Paul Mtema wa Tadea (54).

Baadaye kuliibuka mgogoro ndani ya NCCR-Mageuzi baina ya viongozi wa juu uliokigawa chama pande mbili. Kutokana na hali hiyo, Mrema alijiuzulu ubunge wa Temeke na kuhamia chama cha TLP pamoja na mael;fu ya wafusia wake.

Leo Herman Lwekamwa, aliyekuwa mwenyekiti na mwanzilishi wa TLP, alimkaribisha Mrema na wenzake, akiwamo Thomas Ngawaiya.

Lwekamwa akamkabidhi Mrema uenyekiti wa chama, yeye akabaki kuwa mwanachama wa kawaida. Chama ambacho hakikuwa na mbunge wala diwani kilipata uhai ghafla na katika uchaguzi mkuu wa 2000 kikapata wabunge watano na madiwani kadhaa.

Hata hivyo, TLP nako kuliibuka mgogoro kama ule wa NCCR-Mageuzi na Mrema akitumia vikao akawafukuza wanachama wengi ‘wakorofi’, akiwamo Lwekamwa aliyemkaribisha.

Kutokana na kujiuzulu ubunge Jumapili ya Julai 11, 1999 uchaguzi wa marudio ulifanyika na matokeo yalilirudisha jimbo la Temeke mikononi mwa CCM baada ya John Kibasso kupata ushindi wa kura 27,090, Tambwe Hizza wa CUF akiwa wa pili (25,742), Abbas Mtemvu wa TLP ( 14,701) na Suleiman Hegga wa NCCR-Mageuzi (866).

Uchaguzi mkuu uliofuatia, Oktoba 2000, ulishuhudia ushindani mkubwa katika jimbo la Temeke. CUF iliyomsimamisha Tambwe Hizza ilipewa nafasi kubwa ya kushinda, lakini mgawanyiko wa upinzani ulisababisha John Kibaso wa CCM apate kura 60,872 huku vyama vinane vya upinzani kwa ujumla, ikiwamo CUF, vikipata jumla ya kura 89,665.

Kuanzia hapo kura za Mrema katika chaguzi zilizofuata zikaanza kushuka na baadaye akarudi kugombe nyumbani Vunjo na kushinda.

Je, ni matukio gani yaliendelea baada ya hapo? Tukutane sehemu la mwisho ya mfululizo wa makala hii.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments