Recent-Post

Kasoro uchaguzi CCM, makatibu waonywa

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimetoa onyo kwa makatibu wa wilaya zilizobainika kuwa na kasoro kwenye mchakato wa uchukuaji wa fomu katika uchaguzi wa ndani wa chama hicho.

Wakati uchaguzi wa ndani wa chama hicho ukiendelea kumebainika kasoro kadhaa, ikiwamo uibaji wa fomu na kuzificha katika baadhi ya maeneo na kukwamisha uchaguzi huo kufanyika kama ulivyopangwa.

Onyo hilo limetolewa juzi na Katibu Mkuu wa chama hicho, Daniel Chongolo alipokuwa kwenye ziara ya kufuatilia mchakato huo.

Chongolo mbali ya kutoa onyo aliweka bayana kuwa chama hicho siyo mali ya mtu binafsi, bali ni cha wanachama wote huku akizitaja Wilaya za Ubungo, Babati, Mbeya na Tabora kuongoza kwa kasoro hizo.

“Mimi kama Mkurugenzi wa uchaguzi huu, sitakubali tabia hizi kwani tunaweza kujitengenezea bomu wenyewe, nawaagiza makatibu wa wilaya zote nchini na maeneo yote ambayo tumebaini yana changamoto ya watu kunyimwa fomu za kugombea ndani ya chama,” alisema Chongolo.

“Tunarudisha shughuli ya kutoa fomu, tunataka wale wote wenye dhamira ya kuchukua fomu wachukue bila kuwekewa vizuizi, hiki si chama cha mtu,” alisema Chongolo.

Alitaka watu waruhusu demokrasia ifanye kazi kwa kila mtu kwa kutumia haki yake, na kwamba nafasi ya uongozi inapangwa na Mungu na si kama wanavyotaka wao.

“Tangu tupate uhuru chama chetu kina historia kubwa na watu wanapaswa kurudi na kujifunza, waache makundi na wachague watu watakaokuja kukisaidia,” alisema.

Alisema viongozi wa chama ngazi zote wanapaswa kutimiza majukumu yao kwa mujibu wa katiba ya chama na wanachama waache ubinafsi wa kuchagua nani wa kuwania nafasi ndani ya chama.

“Dhamana tulizonazo hazijatupa haki ya kufanya maamuzi kwa ubinafsi, maeneo ambayo tumegundua yana hiyo changamoto napiga marufuku kuwanyima fomu wanachama, naagiza fomu ziendelee kutolewa kwa watu wote, mchakato wa uchaguzi usitishwe, wanachama wote wenye nia wapate haki ya kuchukua fomu na kugombea.

“Makatibu wa wilaya nchi nzima hakikisheni katika chaguzi hizo vitumike vitabu vilivyohakikiwa kupiga kura na sio vinginevyo,” alitoa angalizo.

Alibainisha kuwa chama kitafuatilia na endapo kitabaini majina ya watu wasiokuwemo kwenye utaratibu wa daftari la wanachama, wakurugenzi au makatibu wa uchaguzi watawajibika.

Wakati Katibu Mkuu wa Chama hicho akiagiza kazi hiyo ya utoaji fomu kuendelea, tayari baadhi ya maeneo wameshakamilisha uchaguzi huku mengine yakirudia kama ilivyoagizwa.

Hali inavyoendelea mikoani

Mkoani Dodoma katika kata za Godegode na Kimagai wilayani Mpwapwa, walianza kutoa upya fomu za kugombea baada ya idadi ya watu waliojitokeza kuwa ndogo lakini nyuma yake kumekuwa na malalamiko.

Mmoja wa viongozi wa CCM wilaya ya Mpwapwa ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini kwa madai kuwa yeye si msemaji, alieleza sababu idadi ya watu wanaojitokeza kuchukua fomu za kugombea kuwa ndogo. “Watu wanalalamika kuhusu kunyimwa nafasi, lakini kiuhalisia hakuna watu wanaokuja kwa wingi kuchukua fomu, matokeo yake tunapata wakati mgumu kuwapata viongozi, sasa tunarudia tena kwa kuongeza muda,” alisema kiongozi huyo ambaye ni msaidizi katika ofisi ya wilaya.

Akizungumzia uchaguzi huo, Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Julius Peter alisema mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu za kugombea nafasi za uongozi unaendelea katika matawi yote 12,581.

Alisema tayari chaguzi zimeanza katika ngazi ya matawi ambako baadhi ya changamoto ambazo zimejitokeza (bila kuzitaja) tayari zimeanza kutatuliwa kwa mujibu wa katiba, kanuni, taratibu na tamaduni za chama.

“Mwitikio wa wanachama kuchukua fomu kuomba uteuzi katika nafasi mbalimbali ni mkubwa, tunaamini tutakamilisha chaguzi zetu salama na kwa ufanisi mkubwa,” alisema Peter.

Aliwaelekeza viongozi wa CCM katika ngazi zote kuendelea kutoa elimu kuwezesha wanachama wenye sifa kugombea ili kupanga safu bora ya uongozi watakaokivusha chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Naye Katibu wa CCM mkoani Arusha, Gerald Munisi alisema kumekuwepo na hamasa kubwa ya wana CCM kujitokeza kuchukua fomu na kwa mara ya kwanza, katika nafasi za mabalozi tu katika mashina mengi kuna wagombea zaidi ya watatu.

“Tumefanya tathmini ya awali tumeona chama kuimarika sana mkoa Arusha, wagombea wengi wamejitokeza kugombea nafasi katika mashina na tunatarajia wengine wengi kujitokeza kugombea katika matawi na jumuiya na baadaye nafasi nyingine ngazi ya wilaya na mikoa,” alisema.

Alisema tayari vikao vya kuchuja majina ya wagombea vimeanza katika kata mbalimbali na baadaye zitafanyika chaguzi.

Kwa upande wa Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro, Elias Mpanda alisema wanachama wameendelea kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali ambapo muitikio umekuwa mkubwa.

Naye Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Jonathan Mabihya alisema uchaguzi unakwenda vizuri na hajapokea malalamiko yoyote mpaka sasa kuhusiana na uchaguzi huo.

“Uchaguzi bado unaendelea na unakwenda vizuri, hatujapokea malalamiko yoyote mpaka sasa, lakini tunaendelea kufuatilia kwa karibu ili kuhakikisha unamalizika salama na wanapatikana viongozi bora ambao watakitumikia chama kwa uaminifu,” alisema Mabihya.

Kwa upande wa Mkoa wa Tabora, licha ya changamoto zilizoonekana awali ikiwemo wanachama kusita kugombea, uchaguzi ngazi ya mashina unaendelea vema baada ya viongozi wa ngazi mbalimbali kufanya kazi ya kuwaelimisha na kuwahamasisha wanachama.

Kutoka Zanzibar

Katika hatua nyingine, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amewataka wana CCM kuwachagua viongozi makini katika ngazi za mashina, akisema ndiyo viongozi wapambanaji katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2025.

Dk Mwinyi ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, aliyasema hayo baada ya kupiga kura za kuwachagua mabalozi na wajumbe katika Shina namba moja la Migombani Mjini Unguja, Mkoa wa Mjini Magharibi.

“Ni vyema wakachaguliwa watu makini ambao wanaweza kusaidia kufanya kazi ndani ya chama hicho na msidharau chaguzi hizi maana viongozi wanaopatikana sasa ndio wenye watu watakaokisaidia chama katika uchaguzi mkuu,” alisema Dk Mwinyi.

Dk Mwinyi pia alishukuru kwa kupewa fursa ya kushiriki kikamilifu katika kumchagua balozi wa Shina namba moja la Migombani na alitumia nafasi hiyo kukiombea CCM kifanikiwe katika chaguzi zake zote zinazoendelea.

“Nashukuru kwa kunipokea vema kama mwanachama mpya, kwani tangu baada ya Uchaguzi Mkuu wa dola uliopita nimekuwa mkaazi rasmi wa Shehia hii.

“Hili ndilo shina langu na leo nimefurahi kushiriki uchaguzi katika shina hili, tutambue kwamba tunaowachagua mwaka huu ndio watakaokuwa wapambanaji wetu kwenye uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2025,” alisema.

Alisema muhimu kila mmoja kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi ili kupata viongozi bora.

 

Post a Comment

0 Comments