KINANA APONGEZA ZIARA YA RAIS SAMIA MAREKANI, ATAJA FAIDA ZAKE.

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kupitia Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Tanzania Bara Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana kimesema kinampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika mwaka mmoja.

Aidha kimesema kinampongeza Rais Samia kwa kufanya ziara katika nchi ya Marekani ambapo pamoja na mambo mengine ametumia ziara hiyo kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa mashirika makubwa ya fedha likiwemo Shirika la Fedha Duniani(IMF) pamoja na Benki ya Dunia.

Tunampogeza Rais Samia kwa kipind cha mwaka mmoja ameleta maendeleo makubwa sana katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu na sasa anaendelea na ziara nje ya nchi, amekutana na viongozi mbalimbali.

Amekutana na Makamu wa Rais wa Marekani na sote tunafahamu Marekani ni nchi kubwa duniani, ni mshirika wetu wa maendeleo, Rais Samia ameonana na Rais wa Benki ya Dunia.Hii benki ya dunia ndio inatoa mikopo yenye riba nafuu.

“Na ukikopa fedha katika benki ya dunia unarudisha kwa miaka 30, hivyo ni fedha ambazo ukizipata unafanya maendeleo na kurudisha polepole, Rais amekutana na Rais wa Shirika la Fedha Duniani na sio linatoa fedha tu bali linatoa hati kwa nchi ili kukubalika kukopa, ukipata hati hiyo unaweza kugonga mlango na ukapokelewa,”amesema Kinana alipokuwa akizungumza na wanachama wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro.

Ameongeza kuwa Rais Samia akiwa nchini Marekani amekutana na viongozi wa ngazi mbalimbali kwenye mashirika makubwa duniani na miongoni mwao wamo viongozi wa sekta ya utalii .”Tunafahamu nchi yetu pia tunategemea utalii, hivyo tunampongeza Rais Samia kwa kazi nzuri anayoifanya.

Katika hatua nyingine Kinana amewakumbusha wanachama wa CCM na wananchi wote kwa ujumla kuwa leo Aprili 26,2022 ni siku ya Muungano kati ya kati ya Tanganyika na Zanzibar , muungano ambao umefikisha miaka 58.

Kuna nchi nyingi duniani ambazo ziliungana lakini leo muungano wao umevunjika.Muungano pekee uliobakia ni wa kwetu, sababu kubwa wananchi wa pande zote mbili wana ushirikiano hata kabla ya kuungana.

Nchi hizi mbili za Jamhuri ya Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika ziliungana , muungano wetu umekuwa wa mfano na sio kwamba haukuwa na matatizo lakini yameshughulikiwa na serikali zote mbili, yameshughulikiwa na mabunge yetu, yameshughulikiwa na vyama vyetu.

Leo muungano umekuwa imara zaidi, baada ya miaka miwili utakuwa umefikisha miaka 60, tunawakumbuka viongozi wetu ambao wameunganisha nchi hizi, wamefanya kazi kubwa na kutukuka,amesema Kinana

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tanzania Bara, Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana, akizungumza mbele ya Wana CCM mkoa wa Kilimanjaro,katika kikao cha ndani leo Aprili 25,2022. Ndugu Kinana amesema anampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanya kazi kubwa ya kuwaletea wananchi maendeleo katika kipindi cha mwaka mmoja tu alichokaa madarakani.

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tanzania Bara, Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana akipewa zawadi ya Mkungu wa Ndizi kutoka kwa Wana CCM kabla ya kuzungumza nao katika kikao cha ndani leo Aprili 25,2022. Katika kikao hicho Ndugu Kinana amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanya kazi kubwa ya kuwaletea wananchi maendeleo katika kipindi cha mwaka mmoja tu alichokaa madarakani. Na Said Mwishehe.Kilimanjaro

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments