KIONGOZI WA MBIO AWATAKA WATENDAJI WA SERIKALI KUTANGULIZA UZALENDO KATIKA MAJUKUMU YAO

Mkimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa akikagua ubora wa madirisha katika mradi wa ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa shule ya sekondari Nanungu wilayani Namtumbo.

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2022 Sahil Geraruma akizungumza na Wanafunzi wa shule ya Sekondari Nanungu(hawapo pichani)kabla ya kufungua vyumba vinne vya madarasa katika shule hiyo vilivyojengwa chini ya mpango wa maendeleo na ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Covid-19, ambapo amewataka wanafunzi na walimu wa shule hiyo kutunza madarasa hayo ili yaweze kudumu kwa muda mrefu,kushoto Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Vita Kawawa.

Wanafunzi wa shule ya Sekondari Nanungu wilayani Namtumbo wakiimba wimbo maalum wakati Mwenge wa Uhuru ulipofika katika shule hiyo kwa ajili ya kufungua vyumba vinne vya madarasa vilivyojengwa chini ya mpango wa maendeleo na ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Covid-19.

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Sahil Geraruma akizindua mpango wa anuani za makazi ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma,kushoto Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Vita Kawawa.

KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2022 Sahil Geraruma,amekeme tabia ya baadhi ya wataalam na watendaji wa Serikali kutanguliza maslahi binafsi pindi wanapopewa dhamana ya kusimamia na kutekeleza miradi ya maendeleo.

Badala yake,amewataka kuwa wazalendo,waaminifu na kutambua kuwa nafasi walizonazo ni kwa ajili ya kuitumikia jamii na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kusababisha miradi kushindwa kuleta tija iliyokusudiwa.

Geraruma ametoa kauli hiyo jana,mara baada ya kukagua ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa katika shule ya Sekondari Nanungu Halmashauri ya wilaya Namtumbo vilivyojengwa chini ya mpango wa maendeleo na ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Covid -19.

Alisema,kuna tabia imejengeka kwa baadhi ya watendaji wa umma kushindwa kusimamia na kutekeleza vyema miradi kutokana na kasumba ya kutanguliza kwanza maslahi binafsi.

Alisema,hali hiyo imesababisha miradi mingi kujengwa chini ya kiwango na kushindwa kulingana na fedha zilizotolewa na Serikali hivyo kusababisha baadhi ya miradi kutodumu kwa muda mrefu.


Amewaagiza watendaji waliosimamia ujenzi wa madarasa hayo kuhakikisha wanafanya marekebisho ya kasoro ndogo ndogo zilizojipo ikiwamo sehemu ya fishabodi ili wanafunzi waendelee kuyatumia mara shule zitakapofunguliwa.

Awali akisoma taarifa ya ujenzi wa madarasa hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Namtumbo,Mkuu wa shule hiyo Judith Ndomba alisema serikali kuu ilitenga kiasi cha Sh.milioni 80,lakini hadi kukamilika kwake wametumia Sh.79,660,500.

Ameipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kwa jitihada zake za kuboresha elimu hapa nchini kwa kujenga mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments