Kiongozi Wa Mwenge Agoma Kuweka Jiwe La Msingi Kituo Cha Afya

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa kwa mwaka 2022, Sahili Nyanzabara Geraruma amekataa kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa Kituo cha Afya cha Malatu kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Newala kwa kile alichoeleza kuwa mradi huo uliogharimu Sh250 millioni upo chini ya kiwango.

 Kiongozi huyo na wenzake watano wamefanya uamuzi huo leo Jumatano April 20, 2022 baada ya kufanya ukaguzi wa jengo na nyaraka katika mradi huo uliopo katika Kijiji cha Malatu wilayani Newala.

"Matumizi ya fedha za umma hayaeleweki, maelekezo ya Serikali hayajafuatwa, madirisha, marumaru na grili ziko chini ya viwango, Mwenge wa Uhuru hauko tayari kuweka jiwe la msingi" amesema Geraruma.

Pia, kiongozi huyo amesema amegundua kuwa nyaraka za mradi huo hazionyeshi fedha imetumikaje pia hazijasainiwa na wahusika katika ofisi ya Halmashauri.

Geraruma amesema kasoro nyingine ni mradi kuchelewa kukamilika ndani ya muda uliotakiwa ambapo ulitakiwa kukamilika Aprili 8, 2022.

Ofisa Afya wa Wilaya ya Newala, DkGeorge Matiko ameiambia Mwananchi kuwa mradi huo umefikia asilimia 94 ya utekelezwaji wake.

Baada ya kukataa kuweka jiwe la msingi Geraruma alimtaka Ofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) kufatilia suala hilo.

Mkazi wa Kijiji cha Malatu Juu, Jamal Ibrahim ameshauri Halmashauri hiyo ifanye utaratibu wa kurekebisha mapungufu hayo.

"Kwa kweli tumeangaliaa tumeona kweli kuna mapungufu maoni yangu warudie ili tupate huduma za kiafya haraka" ameshauri Jamali

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments