Kizungumkuti Nauli za Mabasi, Daladala Nchini

Wakati wadau wa usafirishaji nchini wakipendekeza viwango vipya vya nauli, Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Usafiri Ardhini (Latra CCC) limeshauri nauli za sasa zibaki kama zilivyo.

Kaimu Mtendaji wa Latra CCC, Leo Ngowi alitoa ushauri huo jana, katika kikao kilichoitishwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), huku akieleza sababu za kutokubaliana na mapendekezo ya nauli yaliyotokana na bei za mafuta ya petroli na dizeli kupanda. Katika bei mpya za mafuta zinazotumika sasa, ya juu kabisa ni mkoani Kigoma ambako bei ya dizeli lita moja ni Sh2,936 na Sh 2,783 kwa Dar es Salaam.

Alisema mapitio ya mwisho ya nauli kufanyika mwaka 2013 isiwe kigezo cha kuongeza, bali hadi pale gharama halisi za uzalishaji zitakapoongezeka au kuondoa kabisa kiwango cha faida chini ya asilimia tano.

“Hoja ya kiwango pendekezwa kwa njia ya Dar es Salaam hadi Mwanza ni asilimia 36.84 (wastani wa ongezeko la Sh21,000)na Dar es Salaam hadi Singida ni asilimia 54.84 ya nauli zilizopo hivi sasa,” alisema Ngowi.

Ngowi alisema kwa hali ilivyo sasa pamoja na kampuni kuwasilisha maombi ya upandishwaji nauli, bado hawajaweza kutoza kiwango cha nauli zilizoidhinishwa na Latra hadi sasa.

“Hoja za Kampuni ya Happy Nation kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza kuwa kilomita 1,129 mapitio ya mwisho ya nauli ni mwaka 2013, nauli ya sasa ni Sh53.22 kwa kilomita (Sawa na Sh60,085 kwa Dar es Salaam kwenda Mwanza) na nauli pendekezwa ni Sh72.83 kwa kilomita ikiwa ni sawa na Sh82,225 kwa nauli mpya ya Dar kwenda Mwanza ambao ni umbali wa kilomita 1,129,” alisema Ngowi.

“Hoja za Kampuni ya ABC Upper Class, Dar es Salaam hadi Singida ni Sh72 kwa kilomita (Sawa na Sh48,096 ambapo umbali wa Dar kwenda Singida ni kilomita 688), hivyo kutokana na kupanda kwa gharama za uendeshaji na kushuka kwa thamani ya shilingi, mapitio ya mwisho ya nauli ni mwaka 2013, ambayo ni Sh53.22 kwa kilomita (Sawa na Sh36,464 ambayo ndio nauli ya sasa) na nauli pendekezwa ni Sh82.81 kilomita (Sh56,416).”

Akitoa mapendekezo ya baraza, Ngowi alipinga mamlaka kupokea maombi hayo, badala yake watoa huduma waelekezwe kutumia nauli himilivu kwa njia mbalimbali.

“Kwa mikoa ambayo bado nauli zilizoidhinishwa hazijatekelezwa ipasavyo, zishushwe ili kuendana na uwezo wa abiria,” alisema.

Kwa mapendekezo hayo ya wasafirishaji hiyo ina maana kwamba, kama nauli pendekezwa ya Sh82.81 kwa kilomita, abiria watatakiwa kulipa Sh15,252 kwa safari ya kutoka Dar hadi Morogoro ambayo ni kilomita 186.


Usafiri wa daladala

Akizungumzia mapendekezo ya Umoja wa Wasafirishaji Abiria Mkoa wa Dar es Salaam ya kupanda kwa nauli za daladala mara mbili ya nauli inayotozwa sasa, Ngowi alisema hawajaona hesabu zilizoidhinishwa na wakaguzi wa umma kuonyesha mapato na matumizi.

Alisema katika uchambuzi wa Latra CCC, imeona utoaji huduma za usafiri mijini (safari fupifupi) ni kwamba kuna idadi kubwa ya abiria ambao hupanda na kushuka, ujazaji mkubwa wa abiria zaidi ya ilivyoidhinishwa (waliokaa na wanaosimama) pamoja na wanafunzi wa chekechea hadi darasa la saba.

Watu wenye ulemavu, wagonjwa Alisema baada ya kutathmini walibaini hakuna taarifa iliyothibitishwa na mkaguzi wa hesabu juu ya utoaji wa huduma kwa njia yenye urefu wa kilomita 27.

Akieleza mapendekezo ya baraza hilo, alisema wasilisho hilo lirudishwe kwa mtoa huduma ili atumie gharama za kweli, pia ili kuziba mianya ya upotevu wa fedha, zitumike tiketi mtandao.

“Baraza linaomba, mamlaka isipokee maombi haya hadi yafanyiwe marekebisho, nauli zilizopo hivi sasa ziendelee kutumika hadi tujue gharama halisi ya utoaji wa huduma mijini,” alisema Ngowi.

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam, Kismat Vatfad alisema pamoja na mafuta kupanda, bado Latra wanashauri nauli kubaki kama ilivyo.

Alisema kiwango cha nauli kwa wanafunzi kinaweza kubaki kama kilivyo kwani wanapanda asubuhi na jioni, lakini watu wazima ni lazima kupandisha nauli.

“Hatuwezi kushindana na Serikali, tutaamua tu hatutagoma bali tutasitisha huduma, tunafanya biashara kwa hasara,” alisema.

Mkurugenzi wa Kampuni ya ABC, Severine Ngallo alisema wadhibiti wamekuwa hawafahamu tofauti ya thamani ya mabasi, ukaguzi wa hesabu unaozungumziwa walishaukamilisha na kuukabidhi.

“Hivi viwango vya nauli tunavyopendekeza sio vya leo au kesho, vinaweza kukaa hata miezi sita, sio suala la mafuta tu tunalofikiria, kigezo cha mafuta ni kitu kidogo sana, wala sio cha kuogopesha,” alisema Ngallo.

Mwenyekiti wa Chama cha Kutetea Abiria (Chakua), Hassan Mchanjama alisema, “ni kweli mafuta yamepanda lakini si kwa kupandisha nauli kama walivyofanya wao ni kuendelea kuwaumiza wananchi ambao kwa asilimia kubwa kipato chao ni cha chini.”

Alisema hawakubaliani na kiwango hicho kilichopendekezwa kwa kuwa ni kikubwa ikilinganishwa na uhalisia wa bei zilivyo.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments