Latra Kilimanjaro Yawaonya bajaji Wanaopandisha Nauli

Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra), mkoani Kilimanjaro imesema itawachukulia hatua kali za kisheria madereva bajaji watakaopandisha nauli kiholela mkoani humo.

Jana ,Mamlaka ya Udhibiti wa huduma za Nishati na maji (EWURA) ilitangaza  kuwa mafuta yatapanda bei ambapo bei mpya ya petroli ni Sh 2,861 kutoka Sh 2,540 ikiwa ni ongezeko la Sh321 huku dizeli bei mpya ikiwa ni Sh2,692 kutoka Sh2,403 ambapo ni ongezeko la Sh289.

Hata hivyo, Mwananchi Digital leo Aprili 6 limeshudia baadhi ya madereva bajaji wakitoza wananchi wakiwemo wanafunzi nauli ya Sh1,000 tofauti na ilivyokuwa awali ambapo abiria alikuwa akitozwa Sh500 kutoka Msaranga kwenda Moshi Mjini.

Akizungumza na Mwananchi, Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini, Mkoani humo, Paulo Michael amesema Mamlaka hiyo haijatangaza juu ya upandishwaji wa nauli na kusema kwa sasa kinachofanyika ni ukiukwaji wa sheria.

"Suala la upandishwaji wa nauli, Mamlaka haijatangaza,kwa hiyo rai yangu ni kwamba wadau wasubiri na wawe wavumilivu mpaka tamko rasmi la mamlaka kuhusu kupanda kwa nauli, kwa sasa kupandisha nauli ni kinyume cha sheria.

"Bajaji kwanza hatuzitambua kama vyombo vya kusafirisha abiria kama daladala, mazingira ya bajaji ni kama Taxi anatakiwa akodishwe, kwa hicho wanachokifanya kama daladala kwa mujibu wa sheria hairuhusiwi.

Wakichukua kigezo kwamba wanapandisha nauli wakati wanafanya kazi kama daladala ni makosa, hawaruhusiwi kufanya kazi kama daladala, tukimkuta anafanya kazi kama daladala alafu anapandisha nauli tutamkamata na kumchukulia hatua kwa kukiuka leseni yake,"amesema Paulo

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi mkoani humo, wamesema wameshangaa kuona wanapandishiwa nauli, wameiomba Serikali kuchukua hatua kwa wanaopandisha nauli.

Matrona Kennedy, Mkazi wa Manispaa ya Moshi amesema wakati anatoka nyumbani asubuhi kwenda kazini, alisimamisha bajaji lakini dereva bajaji akampa masharti kwamba kama hana Sh1,000 haweze kupanda usafiri huo.

“Nimeshangaa asubuhi nauli imepanda gafla madereva bajaji wanaringa, wanakuuliza kama huna Sh1,000 huwezi panda bajaji wakati sisi tumeshazoea kupanda bajaji kwa Sh500 kutoka Msaranga kuja Moshi mjini.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments