Mabilioni yawanufaisha wagonjwa wasiostahili


 Wakati gharama za misamaha kwa wagonjwa zikipanda takriban mara mbili, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), amebaini baadhi ilitolewa kinyume cha utaratibu.

Gharama hizo zimeongezeka kutoka Sh8.78 bilioni mwaka 2018/19 hadi Sh16.19 bilioni mwaka 2020/21, hali inayoiongezea Serikali mzigo unaoepukika.

Kwenye ukaguzi alioufanya katika mashirika ya umma kwa mwaka 202/21, CAG amesema Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ilitoa misamaha bila ruzuku yoyote kutoka Wizara ya Afya kwa huduma iliyotolewa na kuendelea kuongezeka kwa misamaha bila ruzuku kutoka serikalini kunaweza kuathiri ubora wa huduma.

Kichere alisema pamoja na kuongezeka kwa wanufaika, alibaini misamaha ya Sh2.59 bilioni ya kumwona daktari ilishughulikiwa moja kwa moja kupitia mfumo wa matibabu na daktari husika bila kupata kibali cha ofisa ustawi wa jamii.

“Hii ni kinyume cha taratibu za uendeshaji za kawaida za mwaka 2015 zinazotaka kabla ya msamaha kutolewa kwa wagonjwa wanaougua magonjwa sugu, mgonjwa anapaswa kuwasilisha kwa ofisa ustawi wa jamii aliyeidhinishwa fomu ya rufaa au barua ili kuangalia iwapo masharti ya msamaha yametimizwa kwa kuchunguza nyaraka husika, ikiwa ni pamoja na kitambulisho cha msamaha,” amesema Kichere.

Sera ya Taifa ya Afya ya mwaka 2017 inavitaka vituo vya afya na hospitali za umma kutoa huduma kwa baadhi ya wagonjwa bila malipo kwa kuzingatia hali yao ya kiuchumi bila kuathiri ubora wa huduma inayotolewa.

Katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), ukaguzi wa CAG umebaini hakuna ushahidi wa kuthibitisha uhalali wa wagonjwa waliosamehewa Sh97 milioni kwa mwaka 2020/21.

“Majalada ya wagonjwa waliosamehewa hayakuwa na taarifa muhimu kama vile barua ya Serikali ya Mtaa au taarifa nyingine yoyote inayoonyesha mgonjwa hana uwezo wa kulipa bili. Pia, nilibaini misamaha ya kiasi cha Sh120 milioni ilitolewa kwa wagonjwa bila kutathmini hali ya kiuchumi na hali ya ugonjwa,” amesema CAG.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments