MAJALIWA: VYOMBO VYA HABARI VIFANYE KAZI KWA KUZINGATIA WELEDI NA MAADILI

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimsikiliza Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Mhandisi Upendo Mbelle wakati akimpa maelezo kuhusu maeneo ya vituo vipya vya kurushia matangazo ya Radio TBC Taifa na TBC fm kwenye maeneo ya Ngara (Karega), Mlimba (Morogoro) Ludewa (Njombe) na Ruangwa (Lindi), Aprili 14, 2022 Ruangwa Mkoani Lindi. Wa pili ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akifungua kitambaa kushiriria uzinduzi wa Kituo cha kurushia matangazo ya Radio TBC Taifa na TBC fm Ruangwa Mkoani Lindi kwa niaba ya vituo vingine vya maeneo ya Ngara (Karega), Mlimba (Morogoro) Ludewa (Njombe) na Ruangwa (Lindi)- (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)



Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimsikiliza Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Mhandisi Upendo Mbelle (Kushoto) wakati akimpa maelezo kuhusu mtambo uliopo kwenye kituo cha kurushia matangazo ya Radio TBC Taifa na TBC fm kilichopo Ruangwa (Lindi), Aprili 14, 2022 Ruangwa Mkoani Lindi. Wa pili Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa TBC Dkt. Ayoub Ryoba, Mkuu wa Mkoa wa Lindi Zainab Telack, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Justina Mashimba (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye wakiwashuhudia Mkurugenzi Mkuu wa TBC Dkt. Ayoub Ryoba na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Justina Mashimba wakikabidhiana hati za vituo vya kurushia matangazo ya Radio TBC Taifa na TBC fm kwenye maeneo ya Ngara (Karega), Mlimba (Morogoro) Ludewa (Njombe) na Ruangwa (Lindi), Aprili 14, 2022 Ruangwa Mkoani Lindi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) 

Mkurugenzi Mkuu wa TBC Dkt. Ayoub Ryoba (Kulia) na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Justina Mashimba (Kushoto) wakikabidhiana hati za vituo vya kurushia matangazo ya Radio TBC Taifa na TBC fm kwenye maeneo ya Ngara (Karega), Mlimba (Morogoro) Ludewa (Njombe) na Ruangwa (Lindi), Aprili 14, 2022 Ruangwa Mkoani Lindi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)  

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza baada ya kuzindua vituo vipya vya kurushia matangazo ya Radio TBC Taifa na TBC fm kwenye maeneo ya Ngara (Karega), Mlimba (Morogoro) Ludewa (Njombe) na Ruangwa (Lindi), Aprili 14, 2022 Ruangwa Mkoani Lindi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema ili kuhakikisha wananchi wanapata habari sahihi vyombo vya habari havina budi kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na weledi pamoja na kutanguliza uzalendo na maslahi ya Taifa.

Pia, Waziri Mkuu amesisitiza kwamba Serikali itaendelea kusimamia matumizi ya mitandao ya kijamii ili pamoja na kuongeza upatikanaji wa habari kuwepo na uzingatiaji wa maadili na weledi. “Ni matarajio yetu kuwa moja ya majukumu yenu ni kulisemea Taifa letu.”

Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Aprili 14, 2022) wakati akizindua vituo vya Kurushia Matangazo ya Redio vya Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) Wilayani Ruangwa – Lindi kwa niaba ya vituo vingine vya wilaya za Ludewa (Njombe), Mlimba (Morogoro) na Ngara (Kagera).

Amesema Serikali itahakikisha uhuru wa vyombo vya habari nchini unaimarishwa na kulindwa, wamiliki na wanahabari wanatakiwa wazingatie maadili na weledi katika kazi zao ili wananchi waendelee kupata taarifa sahihi kwa urahisi zaidi na kwa wakati.

Waziri Mkuu amewasisitiza wamiliki wa vyombo vya habari wahakikishe wanahabari wanapatiwa mikataba ya ajira inayozingatia sheria za ajira sambamba na kufanya utafiti wa habari ili kuepuka upotoshaji kwa kuchapisha au kutangaza taarifa zinazolenga kuchonganisha jamii.

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata habari mbalimbali zikiwemo za burudani, vituo vya televisheni na redio vinatakiwa kuacha tabia za ubaguzi katika kurusha matangazo hususan kazi za sanaa.

Amesema nia ya Serikali ni kuendelea kuuhabarisha, kuuelimisha na kuuburudisha umma kwa njia ya redio, televisheni na mitandao ya kijamii. “Nitumie fursa hii kuwapongeza TBC na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa kutekeleza jukumu hili kwa vitendo.”

Waziri Mkuu amesema Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2020/2021 – 2025/2026) umeainisha vipaumbele vyake katika uwekezaji wa miundombinu ya utangazaji ya TBC, ikiwemo upanuzi wa usikivu wa redio, pamoja na miundombinu.

“Kadhalika, Ilani ya Uchaguzi ya CCM (Ibara 125) inaielekeza Serikali kuwekeza katika uimarishaji wa miundombinu ya utangazaji kwa TBC. Hivyo, kuzinduliwa kwa matangazo ya Redio katika vituo vya Ruangwa, Ludewa, Kilombero (Mlimba), Ngara na maeneo ya jirani ni utekelezaji wa ahadi za CCM kwa wananchi kwa kipindi cha 2020 hadi 2025.”

Pia, Waziri Mkuu ameielekeza TBC, UCSAF na TANESCO kukaa pamoja na kuhakikisha wanatatua changamoto zinazokabili baadhi ya vituo kama vile Ludewa, Mbinga na Kisaki kwa lengo la kuwapatia wananchi wetu huduma ya Habari na Mawasiliano. “Kukatika katika kwa umeme kunaharibu mitambo.”

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema mradi wa ujenzi wa kituo hicho umegharimu shilingi milioni 430 kwa udhamini wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF). Pia vituo vingine vitatu vilivyozinduliwa leo navyo ujenzi wake umedhaminiwa na UCSAF.

Amesema maeneo mengine ambayo miradi inaendelea kutekelezwa kwa ushirikiano wa TBC na UCSAF ni katika wilaya za Ngara (Kagera), Kyela (Mbeya), Ruangwa (Lindi), Kilombero/Mlimba (Morogoro), Ludewa (Njombe), Mlele (Katavi), Makete (Njombe), Uvinza (Kigoma), Mbinga (Ruvuma) na Ngorongoro (Arusha).

Naye, Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Justina Mashimba amesema serikali kupitia mfuko huo utaelendelea kuboresha mawasiliano na usikivu wa huduma za radio kwa kuwafikia wananchi kote nchini.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dkt. Ayoub Ryoba amesema, Shirika hilo limejipanga kuhakikisha wanaendelea kuuhabarisha umma wa wa Tanzania kwa uhakika na weledi kwa kuzingatia maslahi mapana ya nchi huku akiishukuru Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika uboreshaji wa miundombinu ya shirika hilo.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments