Recent-Post

Mbowe Alia Ubaguzi Katika Mfumo Wa Elimu

Mjadala wa lugha gani itumike kufundishia katika mfumo wa elimu, mara nyingi umekuwa ukiibua hisia mbalimbali miongoni mwa wadau wa elimu nchini.

Aghalabu mitazamo huwa ni miwili, ama Kiingereza kiendelee kutumika kama ilivyo sasa katika ngazi za sekondari na vyuo vya elimu ya juu, au tugeukie Kiswahili ambacho kwa sasa kinatumika katika ngazi ya elimu ya msingi pekee.

Mitazamo hiyo imezaa kambi mbili kuu kubwa ambazo mara zote zimekuwa zikiparurana kwa hoja.

Hivi karibuni, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alitoa msimamo wa chama chake, akisema kikifanikiwa kushika dola, lugha itakayotumika ni Kiingereza ili kuondoa alichokiita ubaguzi wa kiajira unaotokana na vijana wengi wa Kitanzania kutoijua lugha hiyo .

Alia ubaguzi

Akiwa wilayani Hai mkoani Kilimanjaro siku chache baada ya kutoka gerezani alipokuwa mahabusu, Mbowe alisema elimu ya Tanzania imejaa ubaguzi wa makundi kati ya wenye uwezo na masikini, huku akieleza kuwa ubaguzi huo unajidhihirisha hata katika ajira hususan kwenye taasisi na kampuni kubwa.

Akihutubia mamia ya wafuasi wake na wananchi waliojitokeza kumpokea katika viwanja vya Bomang’ombe, Mbowe alisema elimu inayotolewa kwa sasa haimjengi Mtanzania kuingia katika soko la ajira kutokana na mfumo wake ulivyo na kwamba inahitaji mabadiliko.

“Kumekuwa na ubaguzi katika elimu kwani viongozi wetu wamekuwa wakituhutubia tujifunze Kiswahili ni lugha yetu ya Taifa, lakini leo Kiswahili hicho kinazungumzwa kwenye shule zetu za kata, viongozi wote na watu wenye uwezo wanasomesha watoto katika shule za mfumo wa Kiingereza; huu ni ubaguzi,” alisema.

Kiongozi huyo anasema Chadema kikiingia madarakani, kitahakikisha watoto wote wanafundishwa kwa lugha ya Kiingereza, kwa kuwa ndiyo lugha ya kimataifa.

Anasema katika dunia inayokwenda kwa kasi huku ikichagizwa na mabadiliko ya teknolojia, maarifa ya lugha ya Kiingereza ni ya lazima na kwamba Kiswahili kitabaki kuwa kama somo la ziada.

Anatoa mfano wa namna Wakenya wanavyotamba katika soko la ajira, kwa sababu ya uwezo walionao katika kutumia Kiingereza.

‘’Vijana wa Kenya wamelikamata soko kubwa hata katika nchi zenye uchumi mzuri ndani ya Afrika tofauti na Watanzania, ambao licha ya kuwa na uwezo, wanakwamishwa na suala la lugha,’’ anaeleza.

Ilivyo sasa nchini, wanafunzi wa shule za awali hadi darasa la saba, wanafundishwa kwa lugha ya Kiswahili, huku Kingereza kikiwa kama somo.

Pia kuna shule za mchepuo wa Kingereza katika ngazi hiyo ya elimu, hata hivyo, nyingi zinamilikiwa na watu au taasisi binafsi. Wanafunzi hao wote wanapomaliza darasa la saba, wanalazimika kutumia Kiingereza kama lugha ya kufundishia.

Wasomi wamjibu

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Aman Chipalo anapingana na mtazamo wa Mbowe, akisema lugha inayofaa kwa kufundishia nchini Tanzania ni Kiswahili, ambacho kinasaidia wanafunzi kuwa na uelewa mpana wa masomo.

Anasema wanaotaka Tanzania ifundishe kwa lugha ya Kiingereza, wanatakiwa kufanya utafiti kwanza ili wajenge hoja zao kwa mapana zaidi.

“Tafiti zilishafanyika kwamba, mwanafunzi anajifunza vizuri zaidi akifundishwa kwa lugha yake ya kwanza. Sisi Tanzania hasa maeneo ya vijijini lugha ya kwanza ni zile za makabila yetu baada ya hapo ni Kiswahili, hivyo tunapaswa kufundisha kwa lugha yetu ya Taifa,” alisema Chipalo.

Msomi huyo anabainisha kuwa, katika nchi zilizoendelea elimu inatolewa kwa lugha mama isipokuwa barani Afrika, ambapo nchi nyingi zimeendelea kukumbatia lugha za kikoloni katika mifumo ya ufundishaji.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Linkoping cha Sweden Dk Hawa Mnyasenga, anasema lugha inayofaa kufundishia ili mtoto aweze kuelewa anachofundishwa ni ile aliyoizoea na ambayo inazungumzwa na wengi.

Anasema kama Kiswahili kingetumika kufundishia na kuwekewa mkazo, watu wangeelewa zaidi kuliko ilivyo sasa, kwa sababu ndiyo lugha inayotumika hata kwa mawasiliano.

“Nilishakuwa mwalimu wa sekondari kwa miaka kadhaa nikifundisha masomo ya sayansi hapo Tanzania. Niliona ugumu wa wanafunzi wa kidato cha kwanza wanavyohangaika kuelewa lugha ya Kiingereza na mada ya nadharia za sayansi kwa wakati mmoja. Yaani mwalimu unakuwa na mambo mawili kwa wakati mmoja, kwanza mtoto afahamu lugha ndipo aje ajue unachomfundisha” anasema Dk Mnyasenga.

Anafafanua kuwa licha ya Kiswahili kuonekana kuwa kichanga kwa kukosa baadhi ya misamiati, changamoto hiyo inaweza kutatuliwa kwa kuiga mifano ya baadhi ya nchi zilizoamua kufundisha kwa kutumia lugha zao na hatimaye kufanikiwa kwa kiwango kikubwa.

“Hapa Sweden lugha ya kufundishia kuanzia chekechekea ni Kisweden, ingawa kuna kozi chache zinazofundishwa kwa Kiingereza hasa vyuo vikuu kuanzia shahada ya pili na shule chache sana zinazofundisha Kiingereza; wenzetu waliamua tangu mwanzo,” anasema.

Naye mhadhiri wa Chuo Kikuu cha St John cha jijini Dodoma, Fredrick Golden, alikosoa ufundishaji kwa lugha ya Kiingereza, akisema unachelewesha maendeleo ya nchi.

Anatoa mfano wa vijana wengi wenye uwezo wanavyofeli mitihani, kwa sababu ya kutojua lugha.

‘’Lugha inachelewesha wanafunzi na kuwafanya washindwe kwenye mitihani. Masomo wanayosoma kwa lugha ngeni yangeweza kutafutiwa misamiati ili yafundishwe kwa Kiswahili ambacho walianza kukijua wakiwa nyumbani kabla ya kwenda shule, ‘’ analeza.

Anaongeza: ‘’Huwachukua wanafunzi zaidi ya miaka miwili angalau kuanza kuelewa lugha wanayofundishiwa, hivyo wanajikuta wametumia muda mwingi kujifunza vitu ambavyo hawavijui jambo linalosababisha waingie kwenye mitihani kwa kukariri masomo ili wafaulu lakini si kuwa na uelewa.’’

Kwa mujibu wa Golden, masomo ya Kiswahili yakifundishwa kuanzia ngazi ya awali hadi vyuo vikuu, Tanzania itakuwa na wasomi wengi kuliko ilivyo sasa.

‘’Wanaotaka Kiingereza ndiyo kitumike kufundishia, wakajifunze kwa nchi kama Japan, Korea, Ujerumani na Russia. Nchi hizi zimeendelea kwenye sayansi kuliko mataifa mengine yanayofundisha lugha za kigeni,’’ anabainisha.

Lugha mbili inawezekana

Kwa upande mwingine, wapo wasomi wanaopigia chapuo matumizi ya lugha zote mbili akiwamo Profesa Kitila Mkumbo ambaye Februari mwaka huu alizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu jijini Dodoma na kueleza kuwa lugha zote mbili zinaweza kutumika katika mfumo wa elimu, kwa sharti kuwa ziwe zinafahamika kwa wanafunzi.

“Lugha gani si hoja. Kwa Tanzania lugha zote mbili zinaweza kutumika. Ukienda Afrika Kusini kuna lugha rasmi 11 na watoto wote wanazisoma. Maoni yangu watoto wajifunze lugha zote mbili,” alieleza.

Alisema kwa utaratibu huo, inawezekana mitihani ikatungwa kwa lugha zote na mwanafunzi akawa na uhuru wa kuchagua lugha anayoitaka.

Alisema Watanzania wasidanganyike, kwani watoto wana uwezo wa kujifunza lugha zaidi ya moja na kwamba kitaalamu mtoto kuanzia miaka mitatu hadi 10, anaweza kujifunza lugha hadi saba bila changamoto yoyote.“Hoja ni watoto wetu wote wawe na uwezo wa kutumia lugha zote mbili halafu atachagua ipi sasa atafanyia mitihani. Ila tusiwafanye Watanzania wakawa wafungwa wa lugha ya Kiingereza,” alifafanua msomi huyo aliyebobea kwenye saikolojia ya elimu, huku akiongeza kuwa Watanzania wasidanganyike kuwa Kiswahili pekee kinawatosha.

Kwa upande wake, mdau wa elimu Richard Mabala, aliwahi kuzungumza na Mwananchi na kueleza kuwa Kiingereza kinaweza kufanya vizuri zaidi kwa mazingira ya Kitanzania kama kitafundishwa kama lugha ya pili au ya tatu.

‘‘... lakini sio kuwa lugha ya kufundishia kwa sababu kimekuwa kikwazo cha wanafunzi kukosa ujuzi na kuishia kukariri,’’ alisema Mabala.

Post a Comment

0 Comments