Meya Awataja Waliomng'oa


  Manispaa ya Moshi imeandika historia baada ya kumng’oa meya wake, Juma Raibu aliyeingia ofisini akiwa kwenye shangingi lakini akarudi nyumbani kwa bodaboda.

Kikao maalumu cha baraza la madiwani kilimuondoa Raibu jana baada ya kumpigi akura ya siri kutokana na tuhuma kadhaa alizonazo ambapo wajumbe 18 walimkataa na 10 wakaendelea kutaka aendelee lakini waliopinga wakawa wengi zaidi.

Akiwa ameliacha Toyota Landcruiser alilopanda asubuhi wakati anaingia ofisini, Raibu ambaye ni diwani wa Bomambuzi, aliandika kwenye ukurasa wake wa Whatsapp (status) “rasmi leo mimi sio meya wa Manispaa ya Moshi. Mungu awajaaliye wote tulioshirikiana katika mambo yote.”

Kabla ya kura kupigwa, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa, Rashidi Gembe alisoma taarifa ya uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili meya huyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk Stephen Kagaigai.

“Timu ya uchunguzi ilitekeleza majukumu yake kwa kuzingatia hadidu za rejea na kubaini mstahiki meya anatumia nafasi yake vibaya, anashiriki vitendo vya rushwa katika ujenzi holela katikati ya mji na ukosefu wa adabu dhidi ya madiwani anaowaongoza,” alisema Gembe.

Meya huyo pia anadaiwa kushiriki sherehe zinazokwenda kinyume na maadili ya Kitanzania hivyo kutokuwa kioo mbele ya jamii.

Akisoma matokeo ya kura za siri zilizopigwa, Gembe alisema “nikiongozwa na kanuni za kudumu za Halmashauri ya Manispaa ya Moshi za mwaka 2015, wajumbe halali walikuwa 28, kura za hapana ni 10 sawa na asilimia 35 .7 na kura za ndiyo ni 18 sawa na asilimia 64.3. Kwa mujibu wa kanuni ya 13.1, inayotaka azimio la kumuondoa madarakani meya kuungwa mkono na theluthi mbili ya wajumbe, natangaza kuwa wajumbe wameunga mkono azimio la halmashauri kumwondoa meya madarakani. Baraza litaongozwa na naibu meya katika kipindi chote cha mpito hadi atakapopatikana meya na kana meya hajaridhika, anaruhusiwa kukata rufaa.”

Baadhi ya madiwani wamesema wamefanya uamuzi huo ni wa kihistoria kumwondoa meya madarakani kutiokana na tuhuma zinazomkabili.

“Leo ilikiwa ni siku ya kumsafisha na kulisafisha jiji letu, tumefanya uamuzi wa kihistoria, na makamu mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Abdulrahaman Kinana anesema cheo kisikufanye ukajitanua, kisikufanye ukawadharau wengine, ametulekeza namna viongozi wanapaswa kufanya wanapowaongoza wengine, tunapaswa kusikiliza hotuba ya Kinana aliyoitoa jana (juzi) jijini Dar es Salaam,” alisema Zubery Abdalla, diwani wa Njolo.

Diwani wa Mjimpya, Abuu Shayo alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya meya kutuhumiwa.

“Tumeingiza kwenye historia Manispaa ya Moshi kumwondoa meya ambaye amekaa madarakani kwa mwaka mmoja kama na nusu, na tumemwondoa baada ya kuona hatufikishi mahali pazuri, ” alisema Shayo.

Alisema ripoti ya mkuu wa mkoa imeeleza kuna fedha zimetumika bila utaratibu. Vilevile, amekuwa akiwatukana madiwani na kuwaona kama wajinga akijua wamechaguliwa na wananchi jambo ambalo si hekima.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments