Mgogoro Meya, DED Watua Kwa Kinana

Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana ameeleza kusikitishwa na migogoro ya madiwani katika Halmashauri na Manispaa ya Moshi, Kilimanjaro ambayo imesababisha meya wa manispaa hiyo, Juma Raibu kung’olewa madarakani.

Kinana (pichani) ambaye yuko ziarani mjini hapa, ameitaka Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kuingilia kati mgogoro huo na kueleza mikakati ya chama hicho kurejesha heshima kwa kuzingatia misingi ya haki yenye utu, ubinadamu na kuheshimiana.

Kuhusu migogoro hiyo ambayo pamoja na mengine imesababisha madiwani kumkataa aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Moshi, Juma Raibu huku pia kukiwa na malalamiko ya madiwani dhidi ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Kastory Msigala kukiuka taratibu na kufanya maamuzi bila kuwashirikisha madiwani, Kinana alisema atazungumza na Waziri wa Tamisemi kufika mkoani humo kuitatua.

“Kuna mgogoro tena hapa mjini na mgogoro Moshi vijijini, mimi nitamuomba waziri wa Tamisemi aje hapa Kilimanjaro, achukue muda asikilize atende haki, CCM tuna utaratibu, maamuzi ni ya vikao si ya mtu, atakuja Waziri wa Tamisemi ili mji utulie, maana mlezi wenu ameomba muwe jiji halafu mna migogoro mingi,” alisema.

Awali mgogoro huo ulizuka baada ya kupigwa kura za siri katika baraza maalumu la madiwani ambapo kura za kumkataa liyekuwa Meya wa Manispaa ya Moshi, Juma Raibu ambapo za kumkataa zilikuwa 18 za kumkubali zikiwa 10 na kuondolewa madarakani Aprili 11, 2022.

Akisoma taarifa ya timu ya uchunguzi ya Mkoa, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Rashidi Gembe alisema Raibu anakabiliwa na tuhuma mbalimbali ikiwamo kutumia nafasi yake vibaya, kupokea rushwa na kuruhusu ujenzi holela katika eneo la CBD, mienendo mibaya na ukosefu wa adabu dhidi ya madiwani wenzake.

Raibu pia anatuhumiwa kutoa maneno ya kuwatambia madiwani wenzake kuwa yeye ni mteule wa kamati kuu ya CCM Taifa na si ngazi ya wilaya wala mkoa, kuchelewa vikao na kutokaimisha vikao kwa naibu meya hata akiwa nje ya ofisi na vikao vingine kulazimisha kuahirishwa kwa kuwa yeye hayupo na kwamba timu hiyo pia imebaini mwenendo mbaya wa Meya huyo.

Hata hivyo, Raibu amekatia rufaa suala lake ambapo akizungumza na Mwananchi jana, alisema suala la kuondolewa kwake kwa sasa liko katika hatua ya rufaa na wiki iliyopita alipeleka rufaa hiyo mwenyewe kwa waziri wa Tamisemi, kama kanuni za uendeshaji wa halmashauri zinavyoelekeza.

“Nilishawasilisha rufaa yangu kwa waziri mwenye dhamana Jijini Dodoma tangu wiki iliyopita na naamini italeta majibu mazuri. Nina imani hiyo kwa sababu rufaa yangu imejikita kwenye masuala ya sheria. Naomba wapiga kura wangu wawe na subira,”alisema.

Mbali na migogoro hiyo, Kinana amewataka viongozi wa CCM kuwa wasemaji wao katika Serikali.

“Wananchi wakiwa na migogoro wanakuja CCM, msivuruge heshima tuliyopewa na wananchi, lazima tuendelee kubaki kuwa sikio na macho ya wananchi, popote penye dhuluma lazima CCM ipige kelele kuwatetea wananchi,” alisema.

Alitaka sheria zinazohusu maisha ya wananchi waeleweshwe, washirikishwe ili kuzielewa badala ya kuwa mzigo kwao.

Akizungumzia uchaguzi ndani ya chama mwaka huu, Kinana alisema: “Niombe viongozi wa chama mtende haki, tunahitaji viongozi wanaokubalika, wenye ushawishi kwa wananchi na wanaoheshimika, niwasihi sana mtende haki, msiruhusu na kuendekeza rushwa.


Biashara mipakani

Akizungumzia biashara za mipakani, Kinana alitaka kurahisishwa na si kufanya maisha ya wananchi kuwa magumu.

Kuhusu wafanyabiashara wadogo, maarufu Wamachinga, alisema:

“Serikali iliposema tuweke miji yetu vizuri watu waondoe vitu barabarani, tuelewane, ukimwambia mtu aondoke barabarani aende Mabogini, anakwenda kumuuzia nani?” alihoji Kinana.

Awali akizungumza katika mkutano huo, Mbunge wa Moshi Mjini, Priscus Tarimo alimpongeza Kinana kwa kueleza kuwa wamachinga wanapaswa kusikilizwa na kupangiwa maeneo yenye watu ili wakafanye biashara.

Naye Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (Suki) CCM, Kanali mstaafu, Ngemela Lubinga alimuomba Kinana kusaidia Moshi kuwa jiji.

Akitoa taarifa ya chama, Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Jonathan Mabihya alisema katika uchaguzi ndani ya chama wamejipanga kupata viongozi bora.

 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments