MKURUGENZI WA UFUNDI TFF ATUA KATAVI KUSAKA VIPAJI.

Mkurugenzi wa ufundi wa shirikisho la mpira wa miguu nchini (TFF) Oscar Mirambo leo Aprili 20,2022 amekutana na mkuu wa mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindiko ofisini kwake katika ziara yake mikoani kusaka vipaji kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 katika mchakato wa kutengeneza timu bora ya taifa.

Akizungumza mbele ya mkuu wa mkoa wa Katavi, Mirambo amesema lengo la TFF ni kutengeneza timu ya taifa yenye sura ya taifa kwa kuhakikisha inajumuisha vijana kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Hata hivyo amegusia dhamira ya Rais wa TFF Wallace Karia kuwa ni kuhakikisha miundombinu ya michezo inaboreshwa hivyo ahadi aliyoitoa ya kutengeneza eneo la kuchezea (pitch) katika uwanja wa Uhuru uliopo mjini Mpanda mkoani humo iko palepale.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko amesema ujio wa kiongozi huyo katika mkoa wa Katavi ni mwanzo mzuri wa kuinua sekta ya michezo katika mkoani humo na kulihakikishia TFF kuwa mkoa una wachezaji wengi wazuri na huenda kama wataendelezwa wapo wenye uwezo wa kuchezea vilabu vikubwa nchini na hata nje ya nchi.

"Nitoe wito kwa wananchi wangu ndani ya mkoa wa Katavi kwamba suala la michezo nalo ni suala muhimu. Niwatake wajitokeze kwa wingi katika kufanya mashindano ya kucheza mpira ili watakaoonekana wanafaa waweze kupiga hatua" alisema RC Mrindoko.

Kuhusu uwanja wa Uhuru, Mrindoko amesema serikali ya mkoa iko tayari kubeba jukumu la kujenga uwanja huo angalau kwa kuanza kujenga upande wa majukwaa huku ikiendelea kutafuta wadau na wafadhili kusaidia ujenzi wa sehemu zingine za uwanja huo.

Mkurugenzi Wa Ufundi Wa shirikisho La Mpira Wa Miguu Nchini (TFF) Oscar Mirambo

Mkuu Wa Mkoa Wa Katavi Mwanamvua Mrindiko

 Na Haruna Juma, Katavi.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments