Mwenyekiti CCM Mara Awataka Watanzania Kumuunga Mkono Rais Samia Kwa Nguvu Zote

 MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa Mara,Samwel Kiboye (Namba Tatu) amesema kuwa,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anafanya kazi kubwa na ngumu, hivyo anastahili kupongezwa ikiwemo kuungwa mkono kwa nguvu zote maana Watanzania ni mashahidi kwa miradi ya kihistoria ambayo inaendelea kutekelezwa hapa nchini.

Ameyasema hayo leo wakati akizungumzia namna ambavyo, Mheshimiwa Rais Samia ameonesha ujasiri wa kipekee katika kusimamia, kufuatilia, kutafuta fursa na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ile ya kimkakati ambayo inafanyika maeneo mengi nchini.

"Niwaombe Watanzania tuzidi kumuombea Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kumuunga mkono kwa kufanya kazi kwa bidii ili mipango ambayo ameiweka kupitia Serikali ya Awamu ya Sita kwa manufaa ya umma iweze kufanikiwa kwa haraka,"amesema Kiboye.

Pia amewapa pole wataalamu wa kutengeneza makundi ndani ya chama kwa maslahi yao binafsi, kwani amesema kupitia uongozi imara wa Mwenyekiti wa chama Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan na Makamu Mwenyekiti, Abdulrahman Kinana mambo hayo yamefikia mwisho.

"Na waliokuwa wamejipanga kutumia pesa na kutumia makundi kwenye uchaguzi, sasa ndiyo mwisho wao, Kinana ni mtu ambaye hataki watu wapate uongozi kwa sababu ya pesa zao kwa kweli chama hiki kitanyooka chini ya Mwenyekiti, mama hodari, jasiri na mchapa kazi, Rais Samia Suluhu Hassan,"amesema

Aidha, amewashauri Watanzania wakiwemo wafuasi wa CCM kuendelea kuitumia mitandao ya kijamii kwa manufaa ikiwemo kushirikishana fursa mbalimbali za ajira, kazi, elimu, afya njia bora ya kufanya kazi kwa bidii ili kuwezesha maendeleo ya haraka kati ya mtu na mtu, jamii na Taifa kwa ujumla.

"Tukifanikiwa kwa hilo, tutakuwa tumetambua vema siri ya mafanikio iliyopo nyuma ya hii mitandao ya kijamii, Serikali ya Awamu ya Sita imetoa uwanda mpana kwa Watanzania kushirikishana taarifa njema kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii ili waweze kusonga mbele na si mitandao hiyo kutumika kuumiza watu, kupotosha taarifa au wakati mwingine kufanyia vitendo vya kitapeli, tukifahamu faida hizi na kuzifanyia kazi, hakika tutayafurahia maisha,"amesema Kiboye.

"Pia tuandike habari kwenye mitandao ya kijamii ambazo hazina chembechembe za uongo, harufu ya kuwagawa watu, migawanyiko katika jamii au kuwakosea adabu wakubwa zetu waliotangulia katika nyadhifa mbalimbali kwa nyakati tofauti tofauti, heshima ni jambo kubwa sana kwa mtu, jamii na hata Taifa,"amesema Kiboye.

Wakati huo huo, Kiboye amekemea wanaotukana viongozi waliotumikia Taifa kwa uzalendo kama vile Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt.Jakaya Kikwete.

"Hawa ni viongozi wetu ambao tunawaheshimu na wamelisaidia taifa hili katika kipindi cha uongozi wao,"amefafanua Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara.

Chanzo Na Diramakini

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments