Nondo nne za Kinana CCM

            

Maneno haki na demokrasia yametawala katika hotuba ya Makamu mwenyekiti wa CCM (Bara), Abdulrahman Kinana aliposimama kwa mara ya kwanza baada ya kuchaguliwa kwenye nafasi hiyo.

Masuala hayo pamoja na madai kwamba Serikali imekuwa na nguvu dhidi ya chama ni miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa yakitajwa kukisumbua chama hicho, hivyo uamuzi wa Kinana kuyaeleza hadharani kunaweza kuwa suluhisho la tatizo hilo.

Kinana amebainisha nondo hizo jana jijini Dodoma, wakati akitoa neno la shukuran baada ya wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM kumchagua kwa kura za ndiyo 1,875 zilizopigwa na wajumbe 1,875 ambazo ni sawa na asilimia 100 ya kura zote zilizopigwa.

Kinana, ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa CCM mwaka 2012 hadi 2018 alipojizulu wadhifa huo, anachukua nafasi ya Philip Mangula aliyeng’atuka.

Hata hivyo, Kinana anarejea kwenye uongozi wa juu wa chama hicho baada ya kuwa nje kwa takribani miaka minne tangu alipojiweka pembeni na kauli yake kubwa na ya kwanza kuitoa na kutaka ifuatwe ni haki, usawa na demokrasia.

Akizungumza kwenye mkutano huo ambao agenda yake kubwa ilikuwa kupitisha mabadiliko ya Katiba ya CCM uliofanyika Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Kinana, ambaye bado anasifika kwa kukijenga chama hicho ambacho kilipita kwenye mawimbi makali mwaka 2012 wakati wa falsafa ya kujivua gamba, aliahidi kukijenga na kukiimarisha.

Alisema kazi hiyo ataifanya kadiri atakavyoweza ili chama kiwe imara na kiheshimike miongoni mwa Watanzania.

Kinana alisema ili chama kiwe imara ni lazima demokrasia iwe imara na ili kutimiza hilo ni lazima kusimamia haki.

Alisema kila mwanachama ana haki ya kuchaguliwa, haki ya kuchagua na kugombea bila upendeleo, mizengwe, bila umaarufu na rushwa.

Kinana ambaye amekuwa mbunge wa Arusha Mjini kwa miaka 10 na kulitumikia Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa miaka takribani 20 hadi alipostaafu akiwa na cheo cha kanali, alisema hakuna mtu mwenye haki miliki ya mawazo na kwamba, viongozi wawe tayari kumsikiliza kila mwanachama.

“Ili demokrasia iwe imara ni lazima tusimamie haki ndani ya chama na baadaye itasambaa hadi kwingine nje. Lazima tuwe tayari kumsikiliza kila mwanachama na ndivyo tunavyoweza kuwa tayari kumsikiliza kila mwananchi. Hata uamuzi ukitolewa na hujaupenda basi kajipange baadaye ujenge hoja yako.

“Wanachama wakimchagua mtu kwani sisi nani wa kupinga. Tusimamie demokrasia na tulinde haki. Tukiweza kuimarisha haki ndani ya CCM, tutaimarisha haki nje ya CCM.

“Nimemsikia mara kadhaa Mwenyekiti wetu (Rais Samia) akizungumzia haki mara kwa mara...namfuatilia sana,” alisema Kinana ambaye ameonekana kuendelea kukubalika ndani ya chama hicho.

Mkongwe huyo alisimama kwa mara ya kwanza mbele ya wajumbe wa Mkutano Mkuu baada ya kupitia misukosuko ya ndani ya chama iliyosababisha Februari 10, 2020 aitwe mbele ya kamati ya maadili na kuonywa baada ya kuelezwa kuwa yeye na wenzake walikuwa wamekwenda kinyume na maadili ya chama.

Aliahidi kuwa katika kipindi cha uongozi wake, atamsaidia Mwenyekiti kusimamia haki na demokrasia ndani ya chama hicho kikongwe barani Afrika, huku akieleza nia ya kuruhusu mawazo kwa wanachama.

Alisema CCM ni chama pendwa ambacho licha ya kuwepo kwa wanachama, kuna watu wengine ambao si wanachama lakini wanakipenda, hivyo chama kiwe sikio la watu.

Jambo jingine ambalo alilizungumza na kushangiliwa na wajumbe ukumbini, ni nia yake kuwa angetamani kuona mtu aliyeshinda uchaguzi ndiye apewe nafasi, kwani ameonekana kupendwa na watu hivyo ukataji wa majina ya walioshinda utakuwa kwa sababu maalumu tu na si vinginevyo.

Alisema ili kufanya chama kiwe na demokrasia pasiwepo na mizengwe, upendeleo, rushwa wala umaarufu, bali haki ndiyo itazamwe zaidi kwa wakati wote kwani ndiyo msingi katika kujiiimarisha kwao.

“Lazima CCM kibaki kuwa sikio la Watanzania, tutajenga demokrasia ndani ya chama, tutatoa nafasi ya kumsikiliza kila mtu kwa nafasi yake, hayo yote tutafanya ili kutoa uhuru wa kidemokrasia kwa chama chetu, ili watu wakifurahie,” alisema Kinana.

CCM haiagizwi na Serikali

Kuhusu Serikali kukisimamia chama, alipinga kuwa jambo hilo siyo sahihi kwa kuwa Serikali haizai chama, bali chama ndicho kinazaa Serikali, kwani ndicho kilichoomba kura kwa wananchi, siyo Serikali.

“Serikali haiwezi kuiagiza CCM kwa kuwa yenyewe ni zao la chama, CCM ndiyo inayoiagiza Serikali na kuisimamia kuhusu utekelezaji wa ilani, sera na ahadi walizotoa viongozi wakati wakijinadi kwenye kampeni... Mzee Mkapa alikuwa akisema Serikali ya CCM lakini kauli hizo siku hizi hazisikiki,” alisema.

Katibu Mkuu huyo wa zamani wa CCM alisisitiza kuwa ni wajibu wa chama kuikosoa Serikali pale inapobidi, ingawa ukosoaji lazima uwe wa staha kwa kutumia njia za vikao badala ya kuzungumza mahali pasipostahili.

Waziri wa zamani wa Kilimo, Stephen Wasira alisema CCM ni chama kinachokwenda na wakati, kinatazama hali ya ndani ilivyo na kinajirekebisha kwa ajili ya kujiandaa kwenda mbele.

“Kwa mfano tuliondoa makatibu wa mikoa tumeona athari yake, utekelezaji wake unakuwa ni dhaifu kwa sababu inabidi kila wakati kuandika barua kwa makatibu kuwaeleza halmashauri kuu imesemaje,” alisema.

Wasira alisema mabadiliko hayo yatawawezesha makatibu wa mikoa kupata taarifa katika vikao vya halmashauri ili atakayezembea afukuzwe hapo hapo.

Waziri wa zamani wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi na Mbunge wa Ismani, alisema mabadiliko yaliyofanyika katika Katiba ya CCM yalihitajika ili kuziba mapengo yaliyokuwepo awali.

Bulembo: CCM itaimarika

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi, Abdala Bulembo alisema ni vitu adimu kumpata Makamu Mwenyekiti kama Kinana ambaye sasa atafanya kazi za CCM na hivyo Rais Samia Suluhu Hassan kufanya shughuli za Serikali.

“Tutegemee kuwa sio CCM ya bahati mbaya. Ni CCM ambayo inaelewa kwasababu Kinana anaijua nchi nzima, anaijua mikoa yote, sasa huwezi kusema Bulembo ametokea Katavi. Huko tulikotoka walikuwepo watu ndani ya chama ambao hawafahamu historia yetu imetoka wapi. Ukiifuta historia unatakiwa kufa,” alisema.

Katiba kubadilishwa

Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan alisema sababu ya mabadiliko ya Katiba ya chama hicho ni kuongeza kasi na ufanisi wa chama.

“Tumerudisha makatibu wa chama ndani ya NEC ili kuongeza kasi ya utekelezaji. Makatibu wa mikoa wapate maelekezo ya mikoa ndani ya NEC na siyo kusubiri maelekezo ya Katibu mkuu.”

Alisema mengine ni kuwezesha chama hicho kupata viongozi bora na wenye uwezo mkubwa wa kusimamia utendaji wa Serikali za Mitaa.

Kudhibiti viongozi na kusimamia ilani ya chama, akisema hata uteuzi wa mameya utafanywa na Kamati Kuu.

Alitaja pia suala la kudhibiti rushwa na vitendo vya ufisadi na kupandisha hadhi za wajumbe

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments