Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jana alikuwa na mazungumzo na Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Haris, kwa lengo la kufufua sekta ya utalii nchini Tanzania na kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili.
Kabla ya kufanya mazungumzo katika jengo la ofisi ya serikali la Eisenhower mjini Washington karibu na ikulu ya White House, Makamu wa Rais wa Marekani Bi Kamala Haris alibainisha wazi ajenda za mazungumzo ambapo alisema: Ziara ya Rais wa Tanzania nchini Marekani inatoa mwanya kwa Marekani kutafuta fursa za uwekezaji kwa kuzingatia kwamba suala hilo lina mahusiano na uchumi kwa ujumla, na pia katika sekta ya utalii.

Makamu wa Rais wa Marekani ameeleza kuwa, ziara ya Rais Samia pia itahamasisha uwekezaji mpya wa karibu dola bilioni moja kutoka kwa makampuni mbalimbali ya Marekani.
Ameongeza kuwa ziara hiyo itachangia ukuaji uchumi wa Tanzania na wakati huo huo itasaidia kukuza uchumi na kuongeza ajira huko Marekani.
Katika mazungumzo hayo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametilia mkazo jitihada zinazofanywa na nchi yake kwa lengo la kurahisisha ushirikiano na sekta binafsi. Amesema, serikali yake, kwa kushirikiana kwa karibu na sekta binafsi, imeweka mazingira mazuri ili kustawisha sekta hiyo. Ameiomba Marekani kuzidisha ushirikiano wa sekta yake binafsi nchini Tanzania. "Ombi langu la pekee hapa ni kuitaka serikali ya Marekani kuhimiza zaidi sekta binafsi kufanya kazi nasi,” amesema Rais Samia akimwambia Kamala Haris jijini Washington DC, siku ya Ijumaa.
0 Comments