Rais Wa Zambia Hajapokea Mshahara Wowote Tangu Aingie Madarakani

Hakainde Hichilema
Mijadala imepamba moto hususan katika mitandao ya kijamii baada ya kubainika kuwa Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema, hajapokea mshahara wowote tangu ashike hatamu za uongozi miezi minane iliyopita.

Wizara inayosimamia mshahara na posho za Rais wa Zambia imesema Hakainde Hichilema binafsi ameamua kutopokea mshahara wowote, na ameamua atangulize mbele maslahi ya wananchi kwa kuwahudumia.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Rais wa Zambia amesema mshahara hakikuwa kichocheo na sababu ya yeye kugombea nafasi hiyo, na anachotaka zaidi, ni kulihudumia taifa lake.

Aidha Hichilema, mchumi mwenye umri wa miaka 59 amekadhibisha ripoti zinazodai kuwa serikali haina nia ya kumlipa mshahara na kusisitiza kuwa: Sijaitilia maanani kadhia hiyo (yamshahara). Azma na motisha yangu ni kutazama namna tunavyoweza kuboresha maisha ya wananchi.

 Hakainde Hichilema
Hatua ya Hichilema kujizuia kupokea mshahara na marupurupu yake imepongezwa na watu wengi hususan Wazambia katika mitandao ya kijamii, ambao wanaiona kuwa ni kitendo cha utu, wakati huu ambapo nchi hiyo inakabiliwa na mdororo wa uchumi.

Hichilema ambaye alitangazwa kuwa mshindi katika uchaguzi wa rais uliofanyika Agosti mwaka uliopita, akimuangusha vibaya Rais Edgar Lungu wa chama tawala, alisema wakati huo kuwa amerithi 'hazina tupu', huku kukiwa na taarifa za kiasi kikubwa cha fedha kuibiwa katika hazina ya taifa ya nchi hiyo.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments